Lowassa alisema pamoja na kuwa viongozi waliopita wameliongoza taifa hili vizuri, bado linahitaji kiongozi mwenye uthubutu na uongozi madhubuti unaoweza kufanya maamuzi magumu.
“Kuamini kama una uwezo na shauku, hakuna budi kwenda sambamba
na uwezo wa kusimamia yale unayoyaamini. Na kwangu haya mawili ni
dhahiri. Nina ari, nina shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu
inavyothibitisha,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.
“Tunapomtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano ni
lazima tukumbuke kwamba tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia ni Amiri
Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika nchi yetu. Na kwa
Chama cha Mapinduzi tunamtafuta mtu ambaye atakuwa pia mwenyekiti wa
chama chetu.
“Naamini kwa vigezo vyote, nina kila sifa ya
kubeba dhamana hizo nzito. Katika mambo ambayo najivunia, na sitayasahau
katika historia yangu ni kushiriki kwangu kuilinda nchi yetu pale
nilipohitajika. Nilishiriki kikamilifu katika Vita vya Kagera nikiwa
miongoni mwa askari wa mstari wa mbele wa mapambano.”
Lowassa pia alikumbusha tukio la mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais kwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete.
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja
tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na
waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo
halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita
kati yetu, mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono,” alisema na
kuongeza:
“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
“Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika
hili… nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize
wajibu wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia.”
Nchemba aliyekuwa ameongozana na mkewe, Neema na
watoto wake watatu, Isaack, Grecious na Joshua pamoja na ndugu jamaa na
marafiki, alisisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo, lazima nchi iwe na
mfumo wa uwajibikaji utakaowezesha kulinda rasilimali za Taifa na
kuongeza Pato la Taifa.
Huku akitumia kauli mbiu ya ‘Mabadiliko ni
Matendo, Wakati ni Sasa’, ambayo ataitumia katika safari yake ya
kuelekea Ikulu, Nchemba aliyetumia dakika 115, kuanzia saa 10.10 jioni
hadi saa 11.25 jioni, alisema atapambana na tabia za watu kufanya kazi
kwa mazoea, rushwa, ufisadi na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
atakayoiongoza endapo atachaguliwa, itakuwa ya uadilifu na uaminifu.
Alisema iwapo atachaguliwa, ataifanya nchi kuwa ya
kipato cha kati sambamba na watu wake, kujenga Taifa linalojitegemea
kibajeti na kuwajengea uwezo wananchi kumiliki uchumi wao wenyewe.
Huku akieleza jinsi atakavyomaliza kilio cha
ukosefu wa ajira, wanafunzi, wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na
watu wa kada mbalimbali nchini, Nchemba alianza hotuba yake kwa
kuwashukia baadhi ya watu wenye dhana potofu juu ya mtu anayestahili
kuwa rais wa nchi.
“Nimeamua kutangazia nia hapa Dodoma kwa sababu
ndipo makao makuu ya nchi na kama nikiwa Rais nitaapishiwa hapa. Pia
sikutaka kutangazia nia nyumbani Iramba ili kuondokana na umimi,”
alisema na kushangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.
Awajibu wanaomponda
“Uzoefu ni mazoea ya starehe. Mtu aliyekaa katika uongozi ni mtu aliyesahau shida za Watanzania.
Jambo la kwanza na la msingi ni kuitambua ajenda
ya Watanzania, Watanzania watamuunga mkono kiongozi kwa kuitambua ajenda
yake,” alisema.
“Kwanza ni haki yangu. Raia wote wana haki ya kugombea, ni haki
ya kikatiba. Lakini ninayo sababu nyingine ambayo ni kubwa zaidi,
naifahamu vizuri Tanzania kwa muda mrefu tangu miaka ya 1970
nimeshirikishwa katika uongozi wa Taifa hili nikiwa na miaka 25,”
alisema Wasira akibebwa na historia ya utendaji ya muda mrefu.
Wasira alitamba kuwa iwapo atateuliwa na CCM na
kushinda urais, Serikali yake itasimamia uadilifu na kupambana na rushwa
na amedhamiria kupandisha viwango vya maendeleo. Aliwaonya Watanzania
kutothubutu kuukabidhi urais kwa mla rushwa, kwani kuna siku atauza
Ikulu.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa
lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya
kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea
anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea.”
Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
mara kwa mara, Wasira alisema kiongozi huyo aliwahi kusema kuwa rais wa
Tanzania ni lazima achukie rushwa na anatakiwa aonekane kwa vitendo
akiichukia... “Siku hizi kila kiongozi anakemea rushwa kama fasheni hata
wala rushwa wanaikemea kwa sababu bila kufanya hivyo wanaona mambo yao
hayatawanyookea.”
Kauli hiyo ya Wasira iliwafanya wafuasi wa chama hicho kusimama na kumshangilia huku wakiimba ‘Wasira sema usiogope.’
Alisema: “Mwalimu Nyerere aliwahi kuniuliza
ninataka nini kati ya utajiri na kuongoza watu, alisema nikitaka utajiri
nichague kuwa mfanyabiashara kwani nitanunua kwa bei rahisi na kuuza
aghali.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni