Kazi ya uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki
(BVR) inatarajiwa kuanza jijini Dar es Salaam kesho na kukamilika
kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), uandikishaji jijini Dar es Salaam utahitimisha kazi hiyo
iliyoanzia mkoani Njombe, Februari mwaka huu na kuendelea katika mikoa
mingine yote ya Bara na visiwani, Zanzibar.
Sisi tunaitakia NEC mafanikio mema katika kufanikisha kazi hii
jijini Dar es Salaam, tukiwa na matumaini makubwa kuona kuwa hakutakuwa
na vikwazo vikubwa kiasi cha kuathiri shughuli hii ambayo ni mwanzo wa
hatua muhimu za kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka
huu.
Kati ya mambo tusiyotarajia kuyashuhudia kuwapo kwa kasoro
zilizowahi kuripotiwa katika mikoa mingine. Ni imani yetu vilevile kuwa
NEC ingali na taarifa za kutosha juu ya jiji la Dar es Salaam na hivyo
imejipanga vya kutosha kuhakikisha kuwa hakuna changamoto isiyopatiwa
suluhisho kungali mapema.
Kwa mfano, taarifa iliyotolewa jana ilieleza kuwa NEC inatarajia
kuandikisha watu milioni mbili jijini Dar es Salaam. Idadi hii ya watu
wenye sifa za kupiga kura ni kubwa kuliko mikoa mingine yote ambayo
tayari kazi hii imeshakamilika. Kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa tayari
NEC imeshajipanga kuandikisha kila mwananchi mwenye sifa jijini Dar es
Salaam.
Ni imani yetu vilevile kuwa NEC wanatambua kuwapo kwa changamoto ya
foleni za magari barabarani zinazoathiri usafiri wa kutoka sehemu moja
ya jiji hadi nyingine. Kwa kutambua hilo, siku zote maafisa wao
watalazimika kujihimu mapema ili hatimaye wafungue vituo kwa muda
uliopangwa, ambao ni saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Tunaamini
kuwa NEC wamejipanga vya kutosha pia kukabiliabna na watu wengi
watakaokuwa wakijitokeza kila uchao katika vituo vya uandikishaji huku
kila mmoja akitaka ahudumiwe yeye kabla ya wengine. Hili linatarajiwa
kutokea kwa vile uelewa wa watu wa jiji la Dar es Salaam kuhusiana na
masuala ya uchaguzi mkuu, na hasa umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya
kupiga kura, ni mkubwa kuliko ilivyo katika maeneo mengine mengi
nchini.
Ni wazi kwamba kwa kutambua hili, ndipo NEC ilipoamua kuwa idadi ya
BVR zitakazotumika jijini Dar es Salaam ni mbili kwa kila kituo huku
maafisa wa uandikishaji wakiwa zaidi ya 3,300, mgawanyo wake ukiwa ni
maafisa 1,144 watakaokuwa katika Manispaa ya Temeke, Kinondoni (1,412)
na Ilala maafisa 792. Huu ni mgawanyo mzuri wa vifaa na rasilimali watu
kulingana na idadi ya watu katika kila manispaa na hivyo ni dhahiri
kuwa uandikishaji utakamilika kwa muda uliopangwa.
Inakumbukwa kuwa wakati NEC ikiandikisha wapiga kura katika mikoa
mingine, hasa ile ya mwanzo ya Njombe na mengine ya Nyanda za Juu
Kusini, kulikuwa na mfululizo wa taarifa za kuwapo kwa kasoro hizi na
zile. Na hata walipokuwa katika mikoa ya Arusha, Geita na kwenye visiwa
vya Zanzibar hivi karibuni, NEC walikumbana pia na changamoto
mbalimbali. Mojawapo ya kero ilikuwa ni mgawanyo usiozingatia wingi wa
watu kwenye maeneo na pia kuchelewa kufunguliwa kwa vituo.
Yapo maeneo pia yalikumbwa na tatizo la kuwapo kwa uhaba wa vifaa
na kwingineko, vituo vya uandikishaji vilidaiwa kuwa mbali na maeneo ya
makazi ya watu.
Ni imani yetu kuwa NEC imeshapata uzoefu wa kutosha kupitia maeneo
mbalimbali ilikokamilisha uandikishaji na hivyo kasoro hizi na nyingine
nyingi zilizoripotiwa hapo zimeshapatiwa majibu. Kamwe hazitakuwa chanzo
cha kukwamisha malengo ya uandikishaji jijini Dar es Salaam.
Kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ni muhimu kwao kujitokeza kwa
wingi ili watekeleze wajibu wao wa kujiandikisha na mwishowe kupata
fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu, lakini wakitambua kuwa wanapaswa
kuzingatia taratibu watakazoelekezwa, huku wakijua kuwa kila mmoja huwa
na haraka na angependa aandikishwe mapema kabla ya wengine.
Yote haya yakizingatiwa, ni wazi kwamba hakutakuwa na kasoro kubwa
zitakazokwamisha uandikishaji wa wapiga kura jijini Dar es Salaam.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni