Jumamosi, Julai 11, 2015

HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA "MCHUJO URAIS 2015"


Dodoma. “Anakatwa, hakatwi” ndilo swali lililokuwa linaulizwa nchi nzima jana, lakini hatimaye Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba Edward Lowassa amekatwa, huku kukiwa na wingu zito baada ya wajumbe watatu kupingana na uamuzi huo.
Muda mfupi baada ya kikao hicho, pamoja na kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikataa kutaja majina yaliyopitishwa, akaunti ya Twitter ya CCM, iliwataja waliopitishwa kuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali na kuwatupa wengine 33 akiwamo Lowassa.
“Kikao cha Kamati Kuu kimeisha salama. Kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuanzia saa 4:00 asubuhi,” alisema Nape baada ya kikao hicho.

Alipotakiwa kutaja majina ya makada watano waliopitishwa, Nape alisema: “Nimeambiwa mchakato bado unaendelea na kesho (leo) Halmashauri Kuu itakutana kuendelea na kazi. Kwa hiyo nawakaribisha kesho kuanzia saa 4:00 asubuhi mje mchukue picha, habari, karibu sana.” Mkutano Mkuu utafanyika saa nane mchana leo.”
Dakika chache baada ya kikao hicho kumalizika, wajumbe watatu wa Kamati Kuu, wakiongozwa na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa wanapinga uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
Dk Nchimbi, akiongozana na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba waliwaeleza waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano wa Kamati Kuu kuwa kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, wajumbe hao wanafahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Baada ya kikao hicho taarifa za wagombea hao zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mijadala ya wazi ilianza kuhusu uamuzi wa kumtosa Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mmoja wa makada watano waliopitishwa kwenye mchujo huo aliithibitishia Mwananchi kuwa jina lake limepita, lakini akasema hataki akaririwe na badala yake akamshauri mwandishi aangalie akaunti ya twitter ya CCM baada ya nusu saa.
Habari za jina la Lowassa kukatwa zilizagaa tangu jana asubuhi, ilipoelezwa kuwa CCM ilifanya majadiliano na wadau mbalimbali kuangalia jinsi ya kudhibiti watu wanaounga mkono baada ya kupata taarifa kuwa ameenguliwa.
Lowassa azua mjadala
Awali wakati Kamati Kuu ya CCM ikikutana jana usiku kupitisha majina ya makada watano walioomba kuwania urais, jina la Edward Lowassa ndilo lililotawala mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii, likiambatana na swali moja; amekatwa, hajakatwa?
Hali hiyo iliendelea zaidi jana usiku wakati CCM ilipotangaza mabadiliko ya tatu ya ratiba za vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
Watu wengi walikuwa wamefurika kwenye jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu kama White House na walioruhusiwa kuingia walikuwa waandishi wa habari na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu, ambao walikuwa wakifuata makabrasha na vitambulisho.
Mapema jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama ingekutana kuanzia saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na Kamati Kuu saa 8:00 mchana, lakini baadaye akatangaza mabadiliko mengine ambayo yalionyesha kuwa Kamati Kuu ingekutana kuanzia saa 10:00 jioni na Halmashauri Kuu baada ya futari.
Majira ya saa 2:00 usiku, Nape alitangaza kuwa kikao cha Kamati Kuu kingeanza muda huo na kwamba kingechukua muda mrefu na hivyo Halmashauri Kuu itakutana leo kuanzia saa 4:00 asubuhi na orodha ya makada watano waliopita kwenye mchujo itatangazwa muda huo.
Wakati Nape anawaambia waandishi wa habari jana asubuhi kuhusu sababu za kuahirishwa kwa vikao, tayari kulikuwa na habari kuwa Lowassa ameenguliwa baada ya vikao vya maridhiano kabla ya vikao hivyo vya juu kuhusu namna ya kudhibiti wanachama wanaomuunga mkono.
Habari hiyo ndiyo iliyokuwa mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. “Amekatwa au hajakatwa?” ndilo swali lililoulizwa na wengi kwenye mitandao hiyo kutaka kujua kama kada huyo, aliyeonyesha kuungwa mkono na wengi wakati wa kusaka wadhamini.
Akizungumza na waandishi jana asubuhi, Nape alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo muhimu kulitokana na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kuwa na vikao na watu mbalimbali kupata ushauri kuhusu namna ya kumaliza mchujo kwa usalama.
“Mwenyekiti alikuwa na vikao mbalimbali vya consultation (mashauriano) na wadau ili kuhakikisha vikao vinakwenda salama,” alisema Nape na kuongeza kuwa hiyo ndiyo ilisababisha ratiba ya vikao kubadilishwa.
Hata hivyo, Nape hakuelezea vikao vya mashauriano kati ya Rais Kikwete na Serikali vilihusisha makundi gani.
Nape alisema mabadiliko hayo pia yalitokana na shughuli za kiserikali na kichama ambazo Kikwete alikuwa nazo mjini Dodoma, ambako Julai 9 mwenyekiti huyo wa CCM alifanya kazi mbili za kuzindua jengo jipya la mikutano la chama hicho na baadaye kulihutubia kwa mara ya mwisho Bunge la 10, siku ambayo alitakiwa kuongoza kikao cha Kamati Kuu.
Awali Kamati ya Usalama na Maadili, ambayo inachambua wagombea na kutoa mapendekezo ya kila mmoja, ilipangwa kukutana Julai 8, na kufuatiwa na Kamati Kuu (Julai 9), Halmashauri Kuu ya Taifa (Julai 10) na Mkutano Mkuu ambao ungefanyika Julai 11-12.
Lowassa ndiye anayeonekana kuwa kinara miongoni mwa makada 38 walioomba kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akionekana kuwa na wafuasi wengi ndani na nje ya chama, hali ambayo aliionyesha kwenye harakati za kutafuta wadhamini.
Mbunge huyo wa Monduli aliungwa mkono na takriban wenyeviti 15 wa mikoa, wabunge kadhaa waliojitokeza bayana kueleza misimamo yao kwake na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.
Jana, baada ya kusogezwa mbele kwa kikao cha Halmashauri Kuu, watu wengi waliondoka kwenye viwanja vya makao makuu ya CCM, na hakukuwapo na makada wanaowania kugombea urais kwenye eneo hilo ambako Kamati Kuu ilikuwa ikiendelea na kikao chake.
Kwa kawaida Kamati Kuu hupitisha majina matano kwa makubaliano licha ya kwamba katiba ya CCM inaruhusu maamuzi kufikiwa kwa kupiga kura.
“Mara nyingi hakuna upigaji kura kwenye vikao vya Kamati Kuu,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya alipoongea na Mwananchi nje ya jengo hilo jana saa 2:40 usiku baada ya kuarifiwa kuwa kikao cha Halmashauri Kuu kimeahirishwa hadi leo.
“Mara nyingi uamuzi huwa ni kwa maridhiano licha ya Katiba kuruhusu upinzani kura pale mnaposhindwa kukubaliana,” alisema Profesa Mwandosya ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu. CHANZO MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom