Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alifanya uteuzi wa
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya
kumteua aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
Uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi kama ilivyo kwa majaji uko chini
ya mamlaka ya rais kisheria na kikatiba. Rais hataomba ruhusa kwa mtu
yeyote katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba. Ni haki na mamlaka
yake kumteua yeyote kwenye nafasi zilizotamkwa hivyo kisheria. Tunajua,
tunaheshimu na kutambua kuwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi alioufanya
mwishoni mwa wiki na kumuapisha siku hiyo hiyo, ni kwa mujibu wa
mamlaka yake.
Pamoja na kutambua mamlaka hayo ya kisheria ya rais, pia pamoja na
kutambua kuwa hakuna mwenye uwezo wa kuhoji, lipo jambo ambalo
limetusumbua kidogo na kwa kweli limesumbua wadau wengi wa uchaguzi
nchini.
Tangu kufanyika kwa uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi mwishoni mwa
wiki, wapo wadau wa aina mbalimbali waliojitokeza kuhoji ulazima wa
mabadiliko hayo katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye joto kubwa
la maandalizi ya uchaguzi mkuu. Ikumbukwe hoja hapa siyo uwezo wa
aliyeteuliwa, ila ni muda.
NEC ilianza kazi ya kuandilisha wapigakura katika Daftari la Kudumu
la Wapigakura kwa mfumo wa utambuzi wa alama za mwili (Biometric Voters
Registration BVR) Februari mwaka huu. Hadi sasa kazi inaelezwa
kukamilika kwa asilimia kubwa katika mikoa yote kasoro Dar es Salaam
ambako uandikishaji unaendelea. Mipango ya upatikanaji wa BVR, ratiba ya
kuandikisha na hata zabuni mbalimbali zilikwisha kutangazwa na kutolewa
kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi mkuu. Yote hayo yamefanyika chini ya
Mkurugenzi aliyeondolewa.
Kwa
maneno mengine maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa zaidi ya asilimia 70
yamefanywa chini ya uongozi wa Mkurugenzi anayeondoka. Tunajua,
uchgaguzi ni mchakato. Mkurugenzi ambaye ameteuliwa kuwa jaji ameshiriki
katika uandikishaji wa wapigakura kwa zaidi ya asilimia 90; ameshiriki
kupanga ununuzi wa vifaa na vitendea kazi vingine kwa zaidi ya asilimia
90; atakuwa ndiye mtu wa katikati kabisa wa maandalizi ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015 kwa maana ya kusimamia wataalam wote wa uchaguzi. Kwa
kifupi ndiye mtendaji mkuu wa mambo yote yanayohusu uchaguzi.
Katika mazingira ya namna hiyo, uamuzi wa kufanya mabadiliko ikiwa
imebakia takribani miezi mitatu tu wananchi wapige kura ya kuwachagua
madiwani, wabunge na rais, kwa kweli inaibua shaka kubwa. Shaka hii ni
kwa nini mabadiliko dakika hizi za majeruhi? Je, uteuzi huu usingeliweza
kusubiri walau aliyekwisha kuanza kufanya kazi hii muhimu na nyeti kwa
taifa aikamilishe?
Tunajua Mkurugenzi aliyeondolewa siyo kwa sababu ya kushindwa
kumudu majukumu yake. Ingelikuwa ndivyo, hasingepandishwa kuwa Jaji wa
Mahakama Kuu. Kwa maoni yetu utendaji wake ulitosheleza aliyotakiwa
kutimiza, kwa maana hiyo kuondolewa kwake kungeliweza tu kusubiri
akamilishe kazi ambayo alikuwa amekwisha kuianza, yaani mchakato mzima
wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Ni dhahiri kumekuwa na madai na malalamiko mengi juu ya maandalizi
ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kumekuwa na maswali mengi juu ya mfumo wa
BVR, kumekuwa na na hoja juu ya NEC kutokupatiwa rasilimali fedha kwa
wakati na ndiyo maana leo hii miezi mitatu kabla ya wananchi kupiga kura
bado dafrati la wapigakura halijakamilika. Wananchi na wadau wa
uchaguzi wamekuwa wakijiuliza hivi hali hii ni makusudi au kuna njama
ndani yake. Hakuna majibu juu ya hoja hizi.
Wananchi wamekuwa wakijiuliza ilikuwaje kwa mfano mwaka mmoja kabla
ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 daftari la wapigakura lilikuwa
limekwisha kukamilika, lakini mwaka huu mambo yamekuwa ni kinyume
kabisa? Swali hili limekuwa likisumbua wengi siyo kwa sababu nyingine
yoyote, ila ni kutokana na kutokufurahiswa na mchakato wa maandalizi ya
uchaguzi kwa ujumla wake.
Tunafikiri pamoja na ukweli kwamba uteuzi uliofanywa na Rais
Kikwete kwa kumuondoa Mkurugenzi wa Uchaguzi na kumweka mwingine ni
halali kisheria, katika mazingira ya sasa kuelekea uchaguzi mkuu wa
mwaka huu maswali mengi zaidi yanaibuka juu ya uamuzi huo wa lalasalama.
Ni kwa maana hiyo, sheria pekee haitoshi katika kufanya maamuzi, kwani
mazingira, nyakati na hata hisia za wananchi ni muhimu pia kuzingatiwa
ili kuendeleza hali ya amani, kuaminiana na kuheshimiana iliyodumu
katika taifa hili tangu uhuru wake ili pia kuujengea uchaguzi mkuu
uhalali pasi na shaka yoyote.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni