Katika dakika za
mwishomwisho wakati wa mchakato wa kuwania urais kwa tiketi ya CCM,
habari za mmoja wa wagombea aliyekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro
hicho, Edward Lowassa kwamba angeenguliwa zilivuma mno na kuibua swali
la atakatwa hakatwi?
Baada ya Kamati Kuu ya chama hicho
(CC), kutangaza majina matano ya waliopitishwa katika hatua ya awali,
bila ya jina lake kuwamo, likaibuka swali la pili; atatoka hatoki?
Sasa jibu la swali hilo la pili limepatikana. Ametoka na sasa ni rasmi kwamba atakuwa mgombea urais kupitia Ukawa.
Usiku
wa kuamkia jana, Waziri Mkuu huyo wa zamani alihudhuria rasmi kikao cha
Kamati Kuu ya Chadema katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutambulishwa
pamoja na kujadiliana mikakati ya kuing’oa CCM madarakani.
Baada
ya jana mchana, viongozi wa Ukawa, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James
Mbatia; Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti wa Chadema
Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walikutana
na waandishi wa habari Dar es Salaam na kumkaribisha rasmi Lowassa
kwenye umoja huo huku wakitumia muda mrefu kumsafisha dhidi ya tuhuma
mbalimbali ambazo amekuwa akihusishwa nazo.
Atinga Kamati Kuu Chadema
Mwandishi wetu alimshuhudia mbunge huyo wa Monduli akihudhuria kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema juzi usiku.
Awali
kikao hicho kilianza saa 9.30 alasiri katika Hoteli ya Ledger Bahari
Beach, Dar es Salaam ambacho Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho
walipata taarifa ya kufanyika kwa kikao hicho ghafla Jumamosi kati ya
saa nne na tano usiku kwa kupigiwa simu, lakini hawakuambiwa ukumbi wala
madhumuni ya kikao hicho zaidi ya kuambiwa kuwa wanatakiwa wawepo Dar
es Salaam siku hiyo.
Lowassa kikaoni
Lowassa
alialikwa kuhudhuria kikao hicho na aliwasili katika lango la kuingia
kwenye hoteli hiyo saa 3.02 usiku akiwa ndani ya gari jeusi aina ya
Toyota Lexus, akiwa amevalia suti nyeusi na shati jeupe na kupokewa na
viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Baada
ya hapo aliongozwa kuelekea katika Chumba cha Wageni Mashuhuri (VIP) na
kukutana na viongozi wachache wa chama hicho wakiwamo Mbowe na Makamu
Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohammed.
Mazungumzo
hayo yalidumu kwa takribani dakika 18 na ilipofika saa 3.20 usiku,
walitoka na kuingia katika ukumbi ambao kikao cha Kamati Kuu ya Chadema
kilikuwa kinafanyika.
Lowassa alishiriki kikao hicho
kwa takriban dakika 98 na ilipofika saa 4.58 usiku, alitoka katika
ukumbi huo akisindikizwa na Mbowe, Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa,
Makamu Mwenyekiti (Bara), Profesa Abdallah Safari, Mohammed na Naibu
Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu ambao baadaye walirejea ukumbini
kuendelea na kikao.
Habari za ndani
Taarifa
kutoka ndani ya kikao hicho zinasema baada ya Lowassa kuwasili na
kutambulishwa kwa wajumbe, alipewa nafasi ya kuzungumza.
Miongoni
mwa mambo anayodaiwa kuwagusia ni pamoja na kashfa ya Richmond ambayo
ilimlazimu kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008. Pia, inaelezwa kuwa
wajumbe walitaka kujua utajiri wake na baada ya kupewa majibu,
walijadiliana jinsi ya kuiangusha CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Ukawa wampokea, wamtetea
Saa
18 baada ya Lowassa kutambulishwa katika Kamati Kuu ya Chadema,
viongozi wengine wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari jana mchana
na kumkaribisha rasmi katika harakati za kuing’oa CCM huku wakimsifia
kuwa ni mchapakazi na mfuatiliaji wa karibu wa majukumu anayokabidhiwa.
Hatua
hiyo Ukawa juu ya mtazamo kwa Lowassa ambaye amekuwa akituhumiwa kwa
kashfa mbalimbali na viongozi hao wa upinzani, inaonyesha dhahiri kwamba
ameshapata baraka za kujiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Wakati
wa sakata la Richmond, viongozi wa upinzani walikuwa wakimponda
kiongozi huyo na Dk Slaa aliwahi kumuweka kwenye orodha aliyoiita ‘list
of shame’.
Viongozi hao walimtetea na kusema kuwa
hakuna aliyewahi kuthibitisha tuhuma dhidi ya Lowassa na kuongeza kuwa
mfumo wa CCM ndiyo wenye matatizo ya rushwa na si mtu.
Profesa
Lipumba alisema suala la ufisadi ni mfumo na si la mtu mmojammoja...
“Sisi tunaponda ufisadi na mfumo wa kifisadi na chanzo kikubwa cha
ufisadi ni mfumo ndani ya CCM, kwanza tuing’oe CCM, hapo ndipo
tutakapoweza kuondoa ufisadi na kujenga msingi wa kupambana na ufisadi
na rushwa iliyopo.
“Lowassa alikumbwa na tuhuma za
ufisadi mwaka 2008, leo ni 2015 lakini ufisadi umeongezeka au umepungua?
Lowassa hayupo serikalini, Tegeta Escrow Akaunti imetokea wakati gani,
Lowassa alikuwapo? Tatizo ni mfumo na jambo la kwanza ni kuing’oa CCM,”
alisema.
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji
alihoji: “Mbona CUF iliwahi kupigana na kuuana na CCM mwaka 2000 lakini
leo wameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa?
“Makaburu
waliuana wakamfunga Mandela (Nelson) lakini alitoka gerezani na kukaa
chini akazungumza nao, kipi cha ajabu? Msumbiji walipigana vita miaka
18, lakini walikubaliana, basi kama Lowassa anakubali kwamba Ukawa ni
muhimu kwa Watanzania, amezinduka na kuona hata bora aende Ukawa
akafanye mabadiliko.”
Alisema kwenye siasa hakuna adui
wa kudumu wala rafiki wa kudumu, bali kuna kudumu kwa hoja ambazo zina
masilahi kwa Taifa... “Wacha Mzee Lowassa aje, tumechoka kuonewa.”
Dk
Makaidi alisema kama Lowassa angekuwa mbaya kiasi hicho, basi angekuwa
amekwisha shtakiwa kama ilivyo kwa viongozi wengine ambao tayari
wameshahukumiwa vifungo kwa matumizi mabaya ya madaraka au rushwa.
“Hata
Lowassa mwenyewe aliwahi kuuliza mwenye uthibitisho kuwa yeye ni fisadi
ajitokeze na kumhukumu lakini mpaka leo hakuna aliyefanya hivyo.”
Alisema
iwapo Lowassa ataamua kujiunga na Ukawa, wanamkaribisha kwa moyo wote
kwani hakuna mwenye uthibitisho kuwa ni fisadi... “Mimi nasema sina
wasiwasi, tunamkaribisha, sijaona ubaya wake.”
Mbatia
alisema Ukawa inamwalika kila Mtanzania aliye tayari kuuondoa mfumo
kandamizi na dhalimu wa CCM na kwamba watashirikiana naye kujenga Taifa
imara na kwamba Lowassa ni miongoni mwa wanaokaribishwa.
“Tunachukua
fursa hii kipekee kumwalika Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la
Monduli, mheshimiwa Edward Lowassa ajiunge na Ukawa na tuko tayari
kushirikiana naye kuhakikisha tunaiondoa CCM madarakani katika Uchaguzi
Mkuu ujao.
“Tunaamini mheshimiwa Lowassa ana uwezo wa
kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo isiyotenda haki. Ni
mchapakazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji katika majukumu
anayokabidhiwa.”
Katika mkutano huo uliodumu kwa dakika
30, Mbatia alisema Ukawa inaamini kwa masilahi mapana ya Taifa
inamhitaji kila Mtanzania ambaye yupo tayari kujiunga nao kuhakikisha
Taifa linakuwa salama na lenye amani ya kweli ambayo msingi wake ni
haki.
“Katika kutafakari kwa kina masilahi mapana ya
Taifa letu, Ukawa tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi katika
kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za Taifa kwa masilahi ya
Watanzania wote.
“Viongozi wa aina hii hawawezi kuwa
ndani ya CCM, maana mfumo wake haumpi kiongozi kutumia vipaji vyake au
ubunifu wake katika kusimamia masilahi ya Taifa letu,” alisema.
Katika
mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kuhudhuriwa
na wenyeviti na makatibu wote wa Ukawa kasoro Dk Slaa, Mbatia alisema:
“Hatutakubali kunyamaza pale sauti zetu zinaponyamazishwa kwa lazima
bila sababu. Tusikubali kunyimwa fursa ambazo tuna uwezo nazo… tuwe
tayari kushiriki michakato ya kidemokrasia ya kuleta mabadiliko na
kupata viongozi bora.”
Akizungumzia uamuzi wa kumpokea
Lowassa, Profesa Lipumba alisema huo ni wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF
na ambao uliafikiwa na Ukawa kwa ujumla.
“Msimamo wa
chama chetu tangu kwenye Baraza Kuu ni mmoja, kuwa sisi kuendelea
kushirikiana na Ukawa na tupate mgombea mmoja. Tuna wagombea wazuri wa
urais lakini tunataka kupata mgombea mmoja atakayeweza kutusaidia kupata
rais na kuiondoa CCM,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema hata tamko la jana la Ukawa limetokana na baraka za Baraza Kuu la Uongozi la hicho.
Alipoulizwa
kuhusu chama chake kusuasua katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea
wa urais kupitia Ukawa, Profesa Lipumba alisema chama hicho kilikuwa
kinajadili suala hili kwa mujibu wa kanuni na taratibu zake.
“Wakati
wote nilipochukua fomu, nilieleza wazi kuwa nipo tayari kugombea urais
na nitagombea kupitia Ukawa na iwapo atatokea mgombea mwingine
nitashirikiana naye na huu ndiyo msimamo hata wa chama,” alisema.
Kuhusu
siku watakayomteua mgombea wa urais, Profesa Lipumba alisema mchakato
huo utafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao kulingana na makubaliano ya
Ukawa.
‘Ruksa’ kuchagua chama
Haji alisema Lowassa atachagua chama cha kujiunga nacho na huko atafuata taratibu iwapo atachagua kugombea nafasi ya urais.
“Kama
atajiunga na chama A, B au C, basi chama hicho kitafuata taratibu zake,
kama atajiunga na Chadema basi atafuata taratibu za huko lakini sisi
vyama vingine tutamuunga mkono,” alisema.
Alipoulizwa
iwapo Ukawa inakaribisha kwa sababu anaonekana kuwa na nguvu ya
kuiangusha CCM, Haji alisema Ukawa ndiyo yenye uwezo wa kuiangusha CCM
na mgombea wa umoja huo ndiye anayeshika bendera.
Mbowe kimya
Tofauti
na mikutano ya nyuma ya umoja huo, Mbowe jana hakuzungumza chochote
licha ya kuulizwa maswali moja kwa moja kuhusu kauli zake za awali
zilizowahi kuonekana bayana kumshambulia Lowassa.
Hata
alipofuatwa na wanahabari baada ya mkutano huo hakuzungumza chochote
zaidi ya kueleza kuwa mambo yote yameelezwa kwa kina na wenzake.
Makamu
Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Mohamed alipotakiwa kuthibitisha
taarifa za Lowassa kushiriki vikao vya Chadema na kwamba ameshajiunga na
chama chao, alisema kwa kifupi: “Sitaki kuzungumzia lolote juu ya
hilo.”
Mgombea bado bado kwanza
Akizungumzia
sababu za kuahirisha kumtangaza mgombea mara kwa mara ikiwamo jana,
makamu mwenyekiti huyo wa Chadema alisema wamekubaliana vyama vimalize
utaratibu wa vikao vya kikatiba ili kupata wagombea na baadaye wakae
pamoja na Ukawa kupitisha jina moja na kumtangaza mgombea mmoja.
Alisema
vyama vya siasa vinatakiwa kubadilika kulingana na hali halisi, hivyo
kuna mambo ambayo yalitakiwa kufikiriwa zaidi kabla.
Pamoja
na suala la kumpata mgombea wa urais, alisema bado kuna masuala yaliyo
mezani yakiwamo kuachiana majimbo mapya 26 na yale ya Mkoa wa Dar es
Salaam yaliyoonekana kuwa na mvutano mkubwa wa nani atayawakilisha.
Imeandikwa na Edwin Mjwahuzi, Nuzulack Dausen na Florence Majani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni