Kuna mgogoro umeibuka katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.
Watu wanaodaiwa kuwa ni wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama
'machinga' wamevamia eneo hilo na kuanza kuuziana maeneo ya viwanja kwa
ajili ya kufanyia biashara zao.
Taarifa zinaeleza zaidi kuwa wahusika wanagawiana maeneo hayo kwa
kuuziana kila kipande kwa kati ya Sh. 50,000 na kuendelea. Kutokana na
hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ameingilia kati na kutangaza
kusimamishwa mara moja kwa mpango huo huku akiwataka wote waliopo
kuondoka mara moja.
Kadhalika, Mkurugenzi huyo amekaririwa akikiri kuwa awali, wao
(Manispaa ya Ilala) na serikali walikubaliana kugawa sehemu ndogo ya
eneo hilo kwa wafanyabiashara wadogo ili walitumie kwa shughuli zao,
lengo likiwa ni kupunguza msongamano katika eneo la Soko la Kariakoo.
Kwamba, hao waliovamia sasa kabla ya utaratibu kutolewa wanatakiwa
kuondoka mara moja kwa vile wanakiuka sheria kwa kujimilikisha eneo hilo
kinyemela, tena bila kusubiri kuwekwa kwa miundombinu muhimu kama ya
vyoo.
Hakika, taarifa hii ya kuligawa eneo la Jangwani kwa Wamachinga
inashangaza. Sisi hatudhani kwamba ni jambo lenye manufaa kwani eneo
hilo hukumbwa na mafuriko mara kwa mara. Kwa sababu hiyo, tunashauri
kuwa mpango huu usitishwe siyo kwa wavamizi tu bali kwa yeyote. Badala
yake, mkurugenzi na viongozi wengine wa Ilala waendelee kukamilisha
mipango yao ya kuandaa maeneo sahihi ya kuwapeleka wafanyabiashara hao,
yakiwamo yanayotajwa kuwa katika maandalizi ya Mchikichini, Kisutu na
Buguruni.
Tunatoa tahadhari hii kutokana na ukweli kuwa eneo la Jangwani siyo
salama hata kidogo. Kijiografia, Jangwani ni mojawapo ya eneo la
mapitio ya maji yaendayo katika Bahari ya Hindi. Hukumbwa na mafuriko
karibu katika kila msimu wa mvua. Hata aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, aliwahi kutoa
tahadhari juu ya matumizi ya ardhi kwa shughuli za aina hiyo kwenye eneo
lote la Bonde la Msimbazi kwa maelezo kuwa ramani ya mipango miji ya
Dar es Salaam inalitaka liwe huru kupitisha maji yanayokwenda baharini,
tena yakitokea katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Vingunguti na
kwingineko.
Ipo
mifano mingi juu ya athari ambazo hutokea kila mara kwa wote wanaokiuka
ukweli huu kuhusu eneo la Jangwani. Kwa mfano, Desemba 2011, taifa
lilipatwa na msiba mkubwa baada ya watu zaidi ya 10 kufariki dunia na
wengine kadhaa kukosa mahala pa kuishi baada ya kukumbwa na mafuriko
katika maeneo wanayoishi yaliyo kwenye mapitio ya maji jijini Dar es
Salaam. Wengi miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo walikuwa ni
wakazi wa maeneo ya Jangwani na kwingineko katika ukanda wa Bonde la
Msimbazi. Maafa mengine yaliyotokana na mafuriko katika maeneo ya
Jangwani na maeneo mengine ya mabondeni jijini Dar es Salaam yalitokea
pia Mei mwaka huu.
Kwa kuzingatia yote hayo, sisi tunaona kuwa uamuzi wowote ule wa
kuwapeleka wamachinga Jangwani haufai. Ni kwa sababu unawaweka wahusika
katika hatari kubwa ya kupoteza maisha yao na mali zao, hasa kutokana
na ukweli kuwa wakati mwingine, mafuriko hayo hutokea ghafla kutokana na
mvua kubwa ambazo hunyesha mbali na jiji la Dar es Salaam.
Sisi tunadhani kuwa badala ya kufikiria mipango ya kuwahamishia
Wamachinga Jangwani, Manispaaa ya Ilala iangalie uwezekano wa kuwaondoa
watu wote walio katika eneo hilo ili kuepusha maafa ya kujitakia. Kama
hiyo haitoshi, itafute pia uwezekano wa kuwatumia wataalamu wa mazingira
kuishauri serikali juu ya umuhimu wa kuhakikisha kuwa eneo lote la
mapitio ya maji jijini Dar es Salaam linaachwa huru, hasa kwa kuzingatia
maelekezo ya ramani za mipango miji. Kinyume chake, ni sawa na
kukaribisha maafa ya mafuriko yatakayoleta kilio siku moja.
Aidha, sisi tunatambua kuwa katika kipindi hiki cha kukaribia
uchaguzi mkuu huwa kuna baadhi ya maamuzi hufanywa na wanasiasa kwa
minajili ya kuwafurahisha wapiga kura wao. Tunahofia kuwa uamuzi huu wa
kutaka kuwahamishia Wwafanyabiashara katika maeneo ya Jangwani unaweza
ukawa ni miongoni mwa nguvu za siasa katika kipindi hiki. Na kama hivyo
ndivyo, basi tunashauri kuwa harakati hizo ziachwe mara moja. Mkurugenzi
na watendaji wengine wa Manispaa ya Ilala watangulize weledi wao katika
kila wanachoamua ili kuepusha maafa yanayoweza kuepukika kirahisi. Hili
lizingatiwe.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni