Pages

Alhamisi, Julai 16, 2015

HONGERA KWA WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI MATOKEO KIDATO CHA SITA

Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Feza Boys, Yonazi Senkondo (katikati) aliyeshika nafasi ya nane kitaifa katika  matokeo ya Kidato cha sita yaliyotangwa jana akipongezwa na Mama yake mzazi Janette Senkondo nyumbani kwao Mbezi Beach Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Shule Msaidizi, Ally Nungu. Picha na Venance Nestory  
 Wanafunzi 38,853 wamefaulu mitihani yao ya kidato cha sita kati ya watahiniwa 40,753 waliofanya mtihani huo mwaka huu, huku matokeo yakionyesha kuwa shule za Serikali na binafsi zimeenda sambamba.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) jana, wanafunzi 35 walishindwa kufanya mitihani hiyo baada ya kuugua ghafla.

Akitangaza matokeo hayo mjini Zanzibar jana, katibu mtendaji wa Necta, Charles Msonde alisema kati ya wahitimu waliofaulu, wasichana ni 11,734, sawa na asilimia 98.56 na wavulana ni 27,119, sawa na asilimia 97 ya watahiniwa.

Kwa mujibu wa Msonde, Shule ya Sekondari ya Feza ya jijini Dar es Salaam iliongoza katika orodha ya shule 10 bora inayojumuisha pia shule za Runzewe (Geita), Feza Girls (Dar), Sumbawanga (Rukwa), Ivumwe (Geita), St Mary’s Mazinde Juu (Tanga), Vwawa (Mbeya), Kisimiri (Arusha), Namabengo (Ruvuma) na Scolastica (Kilimanjaro). 

Orodha ya shule kumi zilizofanya vibaya inaongozwa na Shule ya Sekondari ya Meta ya Mbeya, iliyoshika mkia ikifuatiwa na Kwiro (Morogoro), Mtwara Tech (Mtwara), Iwalanje (Mbeya), Lugoba (Pwani), Kaliua (Tabora), Kilangalanga (Pwani), Lwangwa (Mbeya), Ilongero (Singida) na Bariadi ya Simiyu.
Msonde alisema kwamba kiwango cha ufaulu kwa matokeo ya kidato cha sita kimekuwa kikiongezeka kila mwaka kutokana na juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha kiwango cha elimu kwa maendeleo ya Taifa na wananchi wake.
Waliofanya vizuri katika masomo ya  ni Ramadhani Gembe (Feza Boys), Lesian Lengare (Ilboru), Hunayza S Mohamed (Feza Girls), Riosemary Osian Chengula (St Mary’s Mazinde Juu), Kevin Fidelis Rutahoile (St Joseph Cathedral), Anderton A Masanja (St Joseph Cathedral) Joseph Pasia (Ilboro) Lupyana Kinyamagoha (Mzumbe), Yonazi Charles Senkondo (Feza Boys) na Meghna Solanki kutoka Shule ya Shaaban Robert.

Aliwataja wasichana kumi bora wa kitaifa waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kuwa ni Hunayz S Mohamed (Feza Girls), Rosemary Osian Chegula (St Mary’s Mazinde Juu), Meghna Vipul Solanki (Shaaban Robert), Nice Robert Mathew (St Mary’s Mazinde Juu), Atumpoki Francis Mwakyoma (St Mary’s Mazinde Juu), Irene Godlove (Feza Girls), Kuduishe Kisowile (St Mary’s Mazinde Juu),  Aziza Ramadhan Mkwizu (St Mary’s Mazinde Juu), Zaituni Rashid Langi (Iringa Girls pamoja na Fatma Moshi (Feza Girls).
Upande wa wavulana waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi ni, Ramadhan Gembe, (Feza Boys), Lesian Lengare (Ilboru), Kevin Fidelis Rutahoile, Anderton Masanja, Joseph Pasian, Lupyana Kinyamagoha  (Mzumbe),  Yonazi Charles Senkondo (Feza Boys), Erickson Muyungi (Nyegezi Seminary), Malonja Yona (Ilboru) na Amani Pelesi Fungo kutoka Feza.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Shule za Zanzibar zimeshindwa kuingia miongoni mwa shule zilizotoa watahiniwa kumi bora kitaifa pamoja na shule kumi bora zilizofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Mei mwaka  huu.
Katibu huyo mtendaji aliwatangaza wanafunzi bora wa masomo ya biashara, lugha na sanaa pamoja na matokeo ya mitihani ya ualimu iliyofanyika mwaka huu. CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom