Jumapili, Agosti 02, 2015

Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kesho wanalo jipya?


Kuanzia kesho hadi Agosti 8, mwaka huu, itakuwa ni Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani.
Ni wiki ambayo itawashirikisha wadau mbalimbali likiwamo Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) na Shirika la Viwango Tanzania(TBS).

Mwaka huu, maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika katika viwanja vya Tangamano Jijini Tanga, ambapo pia yatashirikisha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo Stadi(VETA), Scania Ltd, Serengeti Ltd na Tanzania Breweries, Puma energy Ltd, SGS(T) Ltd, na Be Forward, Vodacom Tanzania.


Wadau wote hawa watasaidia pamoja na mambo mengine kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara kwa lengo la kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika kabla ya kutokea.

Kila mwaka, katika maadhimisho ya aina hii, huwa inatolewa kaulimbiu itakayotoa ujumbe kwa watumiaji wote wa barabara nchini. Mwaka huu kauli mbiu inasema; “Endesha Salama Okoa Maisha”.

Kauli mbiu hii inasimamia hali ya halisi ya kile ambacho kila Mtanzania na hata raia wa kigeni walioko nchini wanapaswa kukizingatia.

Lakini Swali hapa ni je, upo usimamizi makini katika utekelezaji wa kauli mbiu hii?

Watanzania na mamlaka husika wamekuwa wepesi sana katika kupanga mikakati madhubuti ya usimamizi na utekelezaji wa jambo fulani.

Lakini mikakati hii mingi ikiishia hawani. Na hii inajidhihirisha kutokana na namna ajali za kutisha zinavyotokea wakati mamlaka za usimamizi zipo.

Zipo ajali nyingi mbaya zilizotokea nchini na bado zinaendelea kutokea. Lakini nyingi utasikia chanzo ni mwendo kasi wa dereva.

Hivi hili la mwendo kasi limeshindikana vipi kulipatia ufumbuzi wa kudumu?

Upo wakati mabasi, kwa mfano yalifungwa kifaa kinachoitwa spidi gavana kuzuia mabasi ya abiria yasiende mwendo mkali.

Japo utaratibu huo ulionyesha nafuu lakini baadaye kutokana na kutokuwepo usimamizi mzuri ukafia mbali kwa madereva/wenye mabasi kuviondoa.

Lakini pia, tunadhani kwamba hizo zilikuwa ni nguvu za soda. Hata kama vifaa vile vingeonyesha mafanikio, bado yapo malori ya mizigo, malori yanayosafirisha mafuta mikoani, na magari yote haya yanatumia barabara hizo hizo.

Malori hayo nayo kwa sehemu kubwa yanachangia ajali mbaya za barabarani kama ambavyo matukio ya hivi karibuni yamedhihirika. Tutafungaje spidi gavana mabasi ya abiria, tunaacha malori ambayo nayo baadhi yamekithiri kwa mwendo kasi? Hizi ni changamoto.

Katika Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kama hii inayoanza kesho, polisi wa usalama barabarani wanapaswa kujipanga sawa sawa pamoja na wadau wote wanaosimamia usalama wa raia na mali zao.

Pamoja na kutoa elimu, pia vinatakiwa viwepo vyombo vya ukaguzi ndani ya Jeshi la Polisi kuhakikisha magari yote  hasa mabasi ya abiria na malori ambayo yamekuwa chanzo kikubwa cha ajali, yanakaguliwa.

Yapo mabasi ya abiria au malori ya mizigo ukiyatizama kwa nje tu yanaashiria kuchoka lakini bado yanaruhusiwa kutembea barabarani. Hata inapotokea ajali, ukitizama gari lililohusika utaona ni chakavu na pengine lilikuwa na hitilafu lukuki kabla hata ya safari lakini bado limo barabarani.

 Pamoja na ukweli huo, bado tunaona kasoro nyingine. Wapo baadhi ya polisi wetu wasio waaminifu ambao pamoja na kuona hitilafu kwenye gari, hufumbia macho na kudai rushwa, kisha kuliachia liendelee na safari. Hii ni dhambi kubwa kwani gari hilo litakapoendelea na safari likasababisha ajali, lawama hiyo haitafutika mbele ya polisi huyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu ikapewa uzito mkubwa. Kamera za kudhibiti mwendo kasi ziongezwe barabarani ili sheria na kanuni za usalama barabarani zizingatiwe na kuheshimiwa.

Adhabu kazi zitolewe kwa wanaokiuka na hata wale wanaosababisha ajali ambazo wangeweza kuziepuka kuokoa roho za watu na mali zao.

Hata hivyo, kikubwa hapa kinachotakiwa ni waandaaji wa wiki hizi kuja na mikakati mipya ya kuzuia ajali za barabarani.

Kama kauli mbinu ni hiyo, je, ni mikakati gani tofauti na huko nyuma ambayo mwaka huu itabadilisha na kupunguza matukio mabaya ya ajali ambayo yamekuwa yakipoteza maisha ya Watanzania?

Tusiishie tu kusema tutatoa elimu, bali elezeni mbinu mpya za kuzuia ajali. Kama mlikuja na spidi gavana zikashindikana, ni mbinu gani nyingine? Lazima polisi wetu wawe wabunifu, waache kubweteka!
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom