Ni kama mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa, ametuma salamu kwa jeshi la polisi kutokana na utitiri
wa wakazi wa jiji hili ‘waliokaidi’ katazo la maandamano na kuja
kumpokea kwa maandamano yaliyosimamisha jiji la Mbeya.
Pamoja na askari polisi waliotanda barabara nzima kuanzia uwanja wa
ndege Songwe hadi viwanja vya Ruanda-Nzovwe, ambao walizuia msafara wa
Lowasa mara tatu, walishindwa kudhibiti waandamanaji.
Maandamano ya jana yanatokea siku moja tu baada ya Jeshi la Polisi
nchini kutoa amrri inayopiga marufuku maandamano nchi nzima mpaka baada
ya uchaguzi mkuu, haikufua dafu wakati mgombea wa urais kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa alipoliteka jiji la
Mbeya kwa saa kadhaa.
Wananchi hao waliandamana kutoka uwanja wa Ndege wa Songwe,
walimsindikiza mpaka katika Uwanja Ruanda Nzovwe (Uwanja wa Dk. Slaa)
ambako alifanya mkutano wa utambulisho na kuwashukuru wakazi wa Mbeya
waliojitikeza kumdhamini katika harakati zake za urais.
Polisi walijaribu kuuzuia msafara huo mara tatu bila mafanikio,
kwani mbali na waliokuwa wakisindikiza msafara, karibu kila alipokuwa
akipita mamia ya wananchi walikuwa wamesimama pembeni mwa barabara
wakimshangilia Lowassa na kumtaka awasalimie.
Utitiri wa polisi ulianza kuonekana nje ya uwanja wa Ndege wa Songwe, wakiwa nje na silaha yakiwamo mabomu ya machozi.
Jaribio la kwanza la kuzuia wafuasi wa Chadema lilitokea eneo la
Ifisi baada ya gari ya Lowassa na viongozi waandamizi wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupita.
Lowassa aliambata na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mgombea
Mwenza, Juma Haji Duni, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
Mwenyekiti wa NLD, Emanuel Makaidi, lilionekana kutozaa matunda kwani
wale wenye pikipiki waliufuata nyuma msafara huo mara naada tu ya
kuingia kwenye barabara ya Mbeya –Tunduma.
Awali ndani ya uwanja wa ndege, yaliruhusiwa kuingia takribani
magari 20, ambayo yalipangwa kuwa kwenye msafara huo ili utembee haraka
na kufima Mbeya mjini mapema.
Msafara ulipofika eneo la Ifisi kilometa chache kutoka uwanja wa
ndege Songwe, polisi walilazimika kuziba barabara kwa magari mawili
yaliyokuwa na askari wenye silaha za moto lakini waendesha bodaboda
waliwapiga chenga askari na kupita mashambani kuunga msafara.
Baada ya muda magari yaliyozuiwa pia nayo yalifuata na msafara
ukaenendelea kuwa na msururu mrefu wa magari, pikipiki, baisikeli na
majaji huku watu wengine wakitembea kwa miguu.
Msafara huo ulipofika Mbalizi, wananchi waliuzuia tena wakitaka
awasalimie na baada ya kufanya hivyo walishangilia kwa nguvu huku
wengine wakiimba, ‘Rais, Rais.’
Kutoka na kusimamishwa kila mara, msafara ulifika Lyunga saa 9:36
ambapo pia ulisimamishwa na mamia ya wananchi ambao walijipanga
barabarani karibu njia yote hasa maeneo yenye shughuli za kibiashara.
Wakati wote msafara ulipotoka Uwanja wa Songwe mpaka uwanja wa
Ruandanzovwe, ulipofanyika mkutano, askari polisi walikuwa wakiufuata
wakiwa na magari matatu ambayo yalikuwa yakitumika kutawanya wananchi
ili msafara utembee haraka.
Mbali na magari hayo, kulikuwa vijana wa kikosi cha ulinzi cha
Chadema ambao baadhi walikuwa kwenye magari mawili ya wazi huku wengine
wakitembea kwa miguu kujaribu kuwatanya wananchi ili msafara huo
utembee.
Licha ya jududi zote hizo, msafara huo uliwasili uwanjani hapo saa
10:15, ikiwa ni takribani saa tatu zilizotumika kutembea kilomita 21.
LOWASSA
Baada ya kukaribishwa na mgombea mwenza, Duni Haji, Lowassa alisema
amefarijika kwa mapokezi makubwa na kuwashukuru wadhamini waliomdhamini
katika safari yake.
Alisema mara ya mwisho kuja Mbeya alikuwa CCM akiomba wadhamini na kulikuwa na umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza.
Alisema kutoka na umati huo, maasimu wake wa kisiasa walisema
amehonga watu hao. “Sasa niulize hapa, kuna mtu amepewa hela?” alihoji
Lowassa huku baadhi wananchi wakiitika “Haongwi mtu hapa.”
Baada ya kauli hiyo nayo Lowassa alisema “Asanteni sana, walie tu, hawatuwezi.”
Lowassa alisema akipata ridhaa ya kuwa Rais, ahadi yake kwa wananchi wa Mbeya ni kuufanya mkoa huo kuwa wa kibiashara.
“Nina
ndoto na Mbeya, nataka kuugeuza Mbeya uwe mji wa kimataifa uwe kama
Nairobi.Nitaanza na uwanja wa Songwe, ndege kutoka sehemu nchi jirani za
Zambia na DRC zije kuanzia safari yao hapa,” alisema.
Kadhalika, alisema kutokana na idadi kubwa ya vijana aliyoiona;
ataunda serikali rafiki kwa masikini hasa waendesha bodaboda, mama
ntilie na wamachinga.
Kuhusu walimu, wakulima alisema ataunda serikali rafiki kwa masikini na kuwa mtu atakayanya uzembe atamuweka pembeni.
Alisema kwenye serikali yake, watu watafanyakazi saa 24 ili kuhakikisha uchumi unakuwa na maendeleo yanapatikana kwa haraka.
Alisema lengo lake la kuwania nafasi hiyo kufanyakazi na sio kufanya mchezo.
Hata hivyo, alisema wananchi wote wenye sifa za kupigakura wanapaswa kwenda kupigakura na kuzilinda ili wahakikishe ushindi.
Wananchi walipomtaka kuzungumzia suala la polisi kuzuia msafara na
kuzonga wananchi, alisema polisi wengi wanakabiliwa na hali duni na
wanataka mabadiliko lakini baadhi yao wanawarudisha nyuma.
MBOWE
Mbowe alisema wanatarajia kuwa na uchaguzi huru na wa haki, lakini
akasema wanataka daftari la kudumu la wapiga kura lifanyiwe uhakiki kwa
uwazi.
Alisema anataka iundwe tume shirikishi itakayojumuisha vyama vya
upinzani ili kuona mchakato mzima wa kuhakiki daftari hilo unakuwa wa
haki.
CHANZO:
NIPASHE
Maoni 1 :
Mmh! Uchaguzi wa mwaka huu unaonekana utakuwa wa kihistoria. Maana upinzani unazidi kushika kasi.
Chapisha Maoni