Kuna taarifa kuwa Tanzania na nchi nyingine za ukanda wa Afrika
Mashariki ziko katika hatari ya kukumbwa na mvua kubwa za El-Nino katika
kipindi cha kuanzia mwezi ujao hadi Desemba, 2015.
Taarifa iliyomkariri Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)
ilieleza jana kuwa tishio hilo linatokana na kuwapo kwa ongezeko la joto
katika Bahari ya Pacific na kwamba, wananchi wanapaswa kuwa macho
kuanzia Septemba Mosi kwa kufuatilia taarifa zao (TMA) ili kujua hali
itakavyokuwa.
Sisi tunawapongeza TMA kwa kutoa taarifa hii mapema, tukiamini kuwa
kwa kufanya hivyo, wananchi na wadau wengine wa masuala ya hali ya hewa
watakuwa na nafasi ya kujipanga kukabiliana na mvua hizo.
Hata hivyo, pamoja na tahadhari hiyo itokanayo na taarifa za
kitaalam, bado kuna uwezekano wa kutofanyiwa kazi kwa taarifa hiyo.
Uzoefu unaonyesha kuwa siyo wananchi wote huchukulia kwa uzito
unaostahili tahadhari za aina hii. Vilevile, siyo mamlaka zote
zinazopaswa kutumia taarifa hizi zitatekeleza wajibu wao kwa kujiandaa
mapema ili kupunguza makali ya El-Nino.
Ni katika kutambua ukweli huo, ndipo sisi tunapoona kuwa sasa kuna
kila sababu kwa wananchi na wadau wengine wote wanaoguswa na taarifa za
TMA kuanza kujiandaa katika kukabiliana na athari za El-Nino.
Tunakumbushia jambo hili huku tukiamini kuwa athari za mvua hizi
siyo ngeni. Ziliwahi kutokea nchini na kusababisha maafa makubwa.
Madaraja yalibomolewa, miundombinu ya barabara iliharibiwa vibaya na
mazao ya chakula yaliangamizwa na mvua hizi zinazonyesha mfululizo, kwa
kasi na kwa wingi. Uchumi wa nchi na pia wa watu mmoja mmoja uliwahi
kutikiswa na mvua za El-Nino. Siyo jambo dogo.
Sisi hatuombei balaa hili kujirudia. Bali, tunadhani kwamba kipindi
hiki ambacho El-Nino bado haijatua kitumiwe kwa maandalizi kabambe.
Tunasisitiza
kuwa tishio hili la El-Nino lisifanyiwe mzaha. Watu wanaoishi maeneo ya
bondeni ni vyema wakawa wa kwanza kujiandaa kwa kuhakikisha kuwa
wanahama mara moja, hata ikibidi wafanye hivyo kwa muda ili kujinusuru
na baa la mafuriko linaloweza kuzimeza nyumba zao na kutishia uhai wao.
Kadhalika, wakulima watumie pia taarifa hizi kwa kuhakikisha kuwa
wanachukua hatua za kukabiliana na njaa itakayotokana na baadhi ya mazao
yao kusombwa na mvua. Mamlaka za serikali, zikiwamo halmshauri za
wilaya, manispaa, miji, majiji na taasisi nyingine za umma
zinazoshughulikia miundombinu ya barabara kama Wakala wa Ujenzi wa
Barabara (Tanroads) zinapaswa kujiandaa mapema vilevile ili kuhakikisha
kuwa madhara yatokanayo na mvua hayawi makubwa kiasi cha kuligharimu
taifa fedha nyingi.
Muhimu kuzingatia ni kuhakikisha kuwa yale yote yanayoweza kufanywa
sasa ili kukabiliana na athari za mvua za El-Nino yafanyike mapema ili
hali itakapokuwa mbaya tayari kuwe na majawabu ya namna ya kuikabili.
Mathalan, kama kuna mitaro ya maji ya barabara imeziba, ni vyema
ikasafishwa sasa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi pindi mvua
zitakapoanza kunyesha na hivyo kujiepusha na ukubwa wa mafuriko utokanao
na tatizo hili.
Shime, taarifa za TMA kuhusiana na tishio la mvua za mafuriko zifanyiwe kazi sasa ili kupunguza madhara. Tujipange.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni