Wabunge wawili, Elibariki Kingu, wa Singida Magharibi (CCM) na Zitto
Kabwe, wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), wamezua mjadala kwa kitendo chao
cha kuamua kutochukua posho za vikao vya Bunge (sitting allowances).
Kingu alizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo na pia
Kabwe amekuwa akielelezea msimamo wake kupitia maandiko yake kwenye
mitandao ya kijamii.
Wanaona kuwa si sawa kwao kuchukua posho hiyo wakati wanalipwa
mshahara wa kila mwezi na posho ya kujikimu wanapokuwa kwenye vikao vya
Bunge.
Kwa hatua hiyo, wabunge hao katika miaka yao mitano, watakuwa
wameachia Sh. milioni 200 kila mmoja na wametaka zielekezwe kufanya
shughuli za maendeleo.
Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
Dk. John Magufuli, ikichukua hatua kali za kubana matumizi ya serikali.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alizuia viongozi kusafiri nje akitaka
badala yake fedha hizo zielekezwe kufanya shughuli za maendeleo.
Pia Rais Magufuli alipunguza fedha zilizochangwa kwa sherehe ya
kuwapongeza wabunge na kuelekeza fedha zilizobaki zikanunue vitanda na
dawa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pia alifanya uamuzi mgumu wa
kufuta gwaride na shamrashamra za sherehe za Uhuru na kuagiza kufanyika
usafi nchini nzima ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Hatua ya wabunge hawa wawili, pia tunaishauri serikali iangalie
utoaji posho kwa wabunge pamoja na watendaji wa serikali. Hii inatokana
na ukweli kwamba, siku za karibuni umezuka mtindo wa kulipana posho
miongoni mwa watendaji wa serikali hata kama ni kazi zao za kila siku
wanazolipwa mshahara. Moja ya vitu vinavyokwamisha maendeleo ya nchi
yetu, ni kutokana na serikali kuwa na matumizi
makubwa yasiyokuwa ya lazima.
Na jambo la kusikitisha zaidi fedha nyingi zimekuwa zikipotea
kutokana na matumizi makubwa tena yasiyokuwa na tija kwa wananchi.
Mathalan, fedha nyingi zimekuwa zikielelezwa kwenye masuala ya posho na
safari na pia kwenye manunuzi. Itakuwa jambo zuri ikiwa Serikali na
Bunge vitaangalia madai haya ya wabunge na kupima ulazima kwa posho za
vikao kwao.
Serikali inapaswa kuweka mkazo kwa kuhakikisha kuwa mapato yake
yanaelekezwa kuinua hali za wananchi na si vinginevyo. Wananchi
wanapenda kuona wakinufaika na maendeleo ya nchi yao na siyo
kuwanufaisha wachache.
Wakati wa kampeni, watu hupita sehemu mbalimbali kuomba kura huku
wakiahidi kuinua hali za maisha ya wananchi. Kila kunapokuwa na hali
ngumu ya uchumi, viongozi wetu wamekuwa mstari wa mbele kuwaomba
wananchi kuvumulia huku wakiahidi hali itatengemaa.
Mathalan, wengi wanakumbuka kuwa mwaka 1979, mara baada ya
kumalizika kwa vita vya kumng’oa dikiteta Nduli Iddi Amini, wa Uganda,
Nduli Iddi Amin, wananchi walipoombwa kujifunga mkanda kwa miezi 18.
Tunashauri Bunge na Serikali kuangalia kwa mapana na marefu suala
hili la posho kwa kupima hali ya uchumi wetu na uwezo wa serikali ili
kupunguza masuala ya kulipana posho nyingi wakati wananchi wakiteseka na
ugumu wa maisha.
Itakuwa jambo jema ikiwa viongozi wetu watakuwa tayari kujibana na
kukumbuka kuwa wakati wao wakifaidi vinono, kuna watu wanapata shida
kupata hata mlo mmoja kwa siku.
CHANZO:
NIPASHE
Maoni 1 :
AMA KWELI TANZANIA SI NCHI MASIKINI
ANGALIA POSHO YAO KWA SIKU MIE WAKATI MWINGINE SIJUI NTAWALISHA NINI WANANGU
Chapisha Maoni