Jumanne, Novemba 24, 2015

Rais Magufuli ateue mawaziri waadilifu na wachapakazi


Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona Baraza la Mawaziri litakalotangazwa na Rais Dk. John Magufuli, ambaye wiki iliyopita alimteua Waziri Mkuu mpya, Majaliwa Kassim Majaliwa.

Watu wengi wanaamini kuwa mawaziri hao ndiyo watatoa picha kamili ya dhamira na utendaji wa Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa letu.Tangu nchi yetu ipate uhuru, imekuwa katika vita ya kukabiliana na maadui watatu ujinga, umaskini na maradhi.
 
Hata hivyo, pamoja na kupita awamu nne za uongozi, lakini bado vita hiyo haijafanikiwa kwa kiasi kinachotarajiwa na wengi.
 
Mathalani, Tanzania ilikuwa haipishani kiuchumi na nchi za bara la Asia za Korea Kusini, Hong Kong, Taiwan na Singapore katika miaka ya 1950 na 1960.
 
Hata hivyo, nchi hizo zimeipita Tanzania kiuchumi kutokana na kufanya mapinduzi makubwa ya elimu, huduma za afya na kuinua maisha ya raia wake.
 
Nchi hizo nne hizi hujulikana na jina la `Asia Tigers’ (Chui wa Asia) kutokana na kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi.
 
Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa Tanzania iko nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na rasilimali nyingi kama ardhi yenye rutuba, madini na gesi.
 
Wananchi walio wengi wanaamini kuwa viongozi na watendaji wa serikali, ndiyo chanzo cha nchi kushindwa kupiga hatua kimaendeleo kutokana na utendaji wa kiwango cha chini.
 
Rais Magufuli amekuja na mbiu ya `Hapa Kazi tu’ na ameanza kuitekeleza kwa vitendo kama ambavyo imejidhihirisha katika maeneo mbalimbali.
 
Mathalani, kitendo chake cha kufanya ziara za kushtukiza katika Wizara ya Fedha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Rais Magufuli pia amefanya uamuzi mgumu wa kuweka utaratibu wa viongozi kusafiri nje ya nchi.
 
Moja ya maeneo ambayo imekuwa ikikamua fedha za serikali ni safari kutokana na viongozi kila uchao kwenda nje ya nchi.
 
Pia kitendo chake cha kufuta shamrashamra za sherehe za Uhuru na badala yake kuagiza kufanyika kwa usafi nchini, kunadhihirisha serikali ya awamu yake haina mchezo.
 
Wananchi wanataka kuona mawaziri watakaoteuliwa ni wenye sifa na siyo uteuzi uendeshwe kwa misingi ya kubebana.
 
Katika awamu ya nne, kuna mawaziri waliotuhumiwa kuwa ni mizigo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao. Hatutegemei jambo hili litajirudia kwa mawaziri kuitwa mizigo halafu kibaya zaidi kuachwa kuendelea na kazi zao bila kuwajibishwa.
 
Watanzania wanataka kuona mawaziri wachapakazi, waadilifu na wazalendo au kwa maneno mengine, wenye dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
 
Katika miaka ya karibuni, imeshuhudiwa mawaziri wakiingia mikataba mibovu ya kutoa rasilimali za nchi kwa wawekezaji.
 
Pamoja na ukweli kuwa kipindi hiki kinaitwa cha sayansi na tekinolojia, lakini bado baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita walifanya vitendo sawa na Chifu wa zamani wa Mvomero, Mangungo, ambaye alitoa maeneo ya utawala wake kwa wakoloni baada ya kupewa zawadi ndogo ndogo kama shanga.
 
Tunamwomba Rais Magufuli kuteua mawaziri watakaoendana na mbiu yake ya `Hapa Kazi tu’ ili kubadili maisha ya Watanzania waliochoka kuishi maisha ya kimaskini wakati wamezungukwa na rasilimali nyingi. 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom