Alhamisi, Januari 14, 2016

NI KWELI "Tusiruhusu wachache kupandikiza mbegu za ubaguzi katika nchi"



Wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar juzi, lilitokea jambo la kufedhehesha kwa kitendo cha baadhi ya waandamanaji kubeba bango lenye ujumbe wa kashfa za kibaguzi.
 
Kundi la waandamanaji hao lililobeba bango lililosema ‘Machotara Hizbu Zanzibar ni nchi ya Waafrika’ na kupita mbele ya viongozi wakuu wa kitaifa.
 
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa waandamanaji hao walipita na bango hilo mbele ya vyombo vya dola ambavyo havikuthubutu kuchukua hatua yoyote.
 
Hata hivyo, tunavipongeza vyama vya CCM na Chadema kwa kukemea maneno hayo ya kibaguzi
Kitendo kilichofanywa na waandamanaji hao ni kinyume kabisa cha tabia na hulka ya Watanzania wanaofuata misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa.
 
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume, walipokuwa wanapigania uhuru,walihakikisha kila mwananchi anaheshimiwa.
 
Viongozi hawa hawakutaka kuona binadamu akiheshimiwa kwa misingi ya rangi yake au kubaguliwa.
 
Tanzania tangu kupata uhuru, imekuwa ikihimiza umoja wa taifa na kila binadamu kuheshimiwa.
 
Ndiyo maana miongoni mwa imani za chama cha Tanu kilicholeta uhuru ilikuwa inasema `binadamu wote ni sawa.’
 
Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema `katika nchi ya Tanganyika, uovu mkubwa ni kitendo cha binadamu kukosa uungwana na kumheshimu mtu mwingine kwa misingi ya rangi yake.’
 
Aliyatoa maneno hayo mazito wakati akihutubia Bunge la Tanganyika baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Madaraka mwaka 1960.
 
Na kwa maana hiyo, ndiyo maana Tanzania ilikuwa inaunga mkono harakati za kukomboa wote waliokuwa wanakandamizwa kwa misingi ya rangi zao.
 
Ikumbukwe kuwa Tanzania ndiyo iliyokuwa kitovu cha harakati za ukombozi barani Afrika na kuwahifadhi wapigania uhuru wengi kama Sam Nujoma, Samora Machel, Dk. Augustino Neto, Oliver Tambo, Thabo Mbeki, Hifikipunye Pohamba na wengineo.
 
Pia hata Marekani weusi wa huko walipokuwa wakibaguliwa, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono wanaharakati weusi kama Martin Luther King, Jesse Jackson na Malcolm X.
 
Kitendo kilichotokea Zanzibar ni cha fedheha na hakikubaliki katika jamii ya waungwana.
 
Ikumbukwe kuwa moja ya shabaha kubwa za Mapinduzi ya Zanzibar, ilikuwa kuleta usawa miongoni mwa wananchi wake.
 
Ndiyo maana kwa miaka mingi jamii za asili tofauti katika visiwa vya Zanzibar, zimekuwa zikiishi kwa amani na utulivu.
 
Inasikitisha kuona kuwa kila inapotokea suala la uchaguzi Zanzibar, basi joto la kisiasa hupanda kiasi cha kutishia amani.
 
Mvutano zaidi huhusisha vyama viwili vya CCM na CUF, ambavyo viongozi wake wamekuwa wakivutana kiasi cha kusababisha kutoelewana miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
 
Ni jambo la kushangaza kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia historia ya kisiasa kujaribu kupandikiza chuki na mgawanyo miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
 
Ni ukosefu wa uungwana kuona baadhi ya wanasiasa wanakumbushia siasa za vyama vya zamani vya ASP, ZNP na ZPPP, ambavyo vilikuwa na mvutano mkubwa katika miaka ya 1950 na 1960 na kuleta mambo hayo katika kipindi hiki.
 
Viongozi na vyombo vya dola hawapaswi kuachia hali hii ya watu kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu kwani athari zake ni kubwa kwa umoja wa kitaifa.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom