Jumatatu, Machi 05, 2012

SIMULIZI MPYA,,, INAITWA DADA YANGU SURA YA ...1....

AUTHOR  ADELA DALLY KAVISHE
Mapenzi ni kitu ambacho kimechukua nafasi kubwa sana katika maisha ya watu kote duniani. Mapenzi haya yanaweza kuleta furaha sana endapo mtu atampata mtu sahihi ambaye atakuwa ni muwazi, mwenye mapenzi ya kweli na kuheshimu uhusiano huo. Lakini mapenzi yanaweza kuleta karaha au kukosa amani kabisa kama kutakuwa na migogoro ambayo unakuta inasababishwa na kukosa uaminifu na kuleta ugomvi kati ya wawili wapendanao. Mapenzi haya yanaweza yakasababisha ndugu kugombana, marafiki kukosana na hata kuuana.

                                                                   *****
Eliza na Upendo ni wasichana warembo waliozaliwa katika familia ya kitajiri mkoani Morogoro. Wasichana hawa waliishi katika maisha ya kifahari kutokana na Baba yao Mzee Bondi kuwa na uwezo mkubwa sana kifedha. Mzee Bondi aliwapenda sana mabinti zake na alipenda wasome kwa bidii ili baadaye waje kuwa na maisha bora. Eliza na Upendo walisoma katika hali nzuri sana hadi kufikia elimu ya chuo, ambapo Upendo alikuwa akisoma Chuo Kikuuu cha Dar es salaam na Eliza Chuo cha Uhasibu Arusha. Kutokana na masomo walitengana na kuonana mara chache kipindi cha likizo.  

Baadaye Eliza na Upendo walijikuta wakijiingiza katika uhusiano wa kimapenzi wote wawili kwa kijana mmoja mtanashati aliyeitwa James bila kujijua. Uhusiano wa kimapenzi kwa mwanamume mmoja ulileta migogoro katika familia yao.

                                                           *********

Baada ya kumaliza Kidato cha Sita Upendo alipangiwa kwenda kuendelea na masomo ya Chuo Mkoa wa Dar es salaam. Baba yake alifurahi sana na kumuahidi kuwa angempa zawadi nono kama angefanya vizuri akiwa Chuo. Kabla ya kujiunga na chuo Upendo alifanyiwa sherehe kubwa ya kumpongeza, ambayo ilihudhuriwa na watu wengi sana ndugu jamaa na marafiki. Wakati huo mdogo wake Eliza alikuwa Kidato cha Sita kwani walipishana mwaka mmoja tu na kwa jinsi walivyokuwa, walionekana kama mapacha. Wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kwa watu ambao walikuwa hawajawaona kujua mkubwa ni yupi na mdogo ni yupi.

Siku zilipokaribia za kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Upendo alijiandaa barabara kwa ajili ya  kuanza masomo ya Chuo. Siku moja kabla ya kuondoka Mama na Baba yake walimwita na kuzungumza naye mazungumzo ili kumwasa na kumpa ushauri.
“Upendo tumeishi wote kutoka ukiwa mdogo, hujawahi kuishi mbali nasi kuanzia masomo ya elimu ya shule ya msingi hadi elimu ya Sekondari. Umesomea Morogoro, sasa unakwenda Dar es salaam kuanza maisha mapya ya kuishi mbali na sisi. Ninakuomba ukasome kwa bidii ili ujiandalie maisha yako ya baadaye.” Mzee Bondi alimaliza kutoa nasaha zake, huku Upendo akisikiliza kwa makini kabisa.

“Umsikilize baba yako kwa makini kwa sababu dunia ya sasa imeharibika mwanangu. Magonjwa ni mengi na ukifika huko sio ndio ukasahau kilichokupeleka. Kumbuka kinachokupeleka ni masomo na sio starehe. Nadhani umenielewa.” Alisisitiza Mama yake.
“Jamani Mama nitasoma kwa bidii mbona unaongea hivyo.” Upendo alihamaki “Lazima niongee mwanangu vijana wa sasa mnakutana na mambo mengi na vishawishi vingi usipokuwa makini utapoteza kabisa mwelekeo na malengo yako.” Mama upendo aliendelea kutoa nasaha.
“Baba na Mama nimewasikia, kamwe sitoenda kutenda yasiyo sahihi, nitasoma na nitawafurahisha siku zote wazazi wangu.” Upendo alijibu kwa unyenyekevu.

Baada ya maongezi hayo wote walisimama na kuelekea kulala ili Upendo akaanze kujiandaa na safari. Upendo aliingia chumbani na kuanza kupanga vitu vyake akisaidiana na mdogo wake Eliza.
“Ndugu yangu si nilikuwa nimekaa na Mama na Baba sebuleni wananipa wosia namna ya kuishi huko Chuo.” Alisema Upendo.
“Eheh! Ilikuaje? Kwa sababu Mama naye akiamua kuongea ni balaa wamesemaje hao wazee?” Alidadisi Eliza.
 “Mwenzangu, Baba na Mama wameniambia nikienda nisisahau kilichonipeleka nisiendekeze starehe.” Alisema Upendo.
“Heh! Hao wazee nao inamaana ukakae tu unasoma hata disko usijichanganye? Aka mwaya sisi bado vijana lazima tujirushe we ngoja mi nimalize Kidato cha Sita nikienda chuo nitajirusha sana kwani hapa nyumbani hawa wazee wanatubania sana.” Alizungumza Eliza.
“Usiseme hivyo mdogo wangu mimi naona Baba na Mama wapo sahihi, kwani nikianza kujiingiza kwenye starehe nitajikuta nafeli mitihani halafu malengo yangu ya kuwa mwanasheria yasitimie, we mwenzangu unawaza kujirusha tu.”  Alijibu Upendo. 
“Kujirusha ni wajibu na kusoma nitasoma tu, haya bwana tufanye haraka tuwahi kulala hao wazee watakuamsha mapema kesho.” Alimaliza Eliza. Usikose muendelezo wa simulizi hii katika sura ya 2.................

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom