Alhamisi, Januari 17, 2013

MALIPO NI HAPAHAPA SURA YA ........11........

 
ILIPOISHIA“Jamani za siku nyingi.” Aliendelea kumsemesha Julieth. Mwanzo Julieth hakumtambua lakini alivyozidi kumwangalia akamkumbuka.
“Oh! Kumbe Zubeda! Mambo vipi rafiki yangu? Nimefurahi sana kukuona habari za hapa?” Zubeda alikuwa ni rafiki yake Julieth, kwani walikuwa wakiuza chapati pamoja wakati Julieth akiwa Arusha. Domina alianza kulia, haraka Zubeda alimchukua Dominiki ili Julieth amnyonyeshe Domina. USIKOSE SURA YA 11
 
INAPOENDELEA 
“Habari za hapa ni nzuri kiasi.” Aliongea Zubeda huku akimshika vizuri mtoto.
“Nzuri kiasi!” Alihamaki Julieth huku akimkazia macho Zubeda.
“Ndiyo! Nzuri kidogo.” Alisisitiza Zubeda huku akiyakwepa macho ya Julieth.
 “Vipi mwenzangu mbona ulikuwa kimya sana? Wakati mama yako akiwa anaumwa tulikupigia simu mara nyingi lakini haikupatikana na …”
“Ehe! Sasa anaendeleaje?” Julieth alimkatisha Zubeda na kuuliza akiwa katika hali ya kushtuka.

 Zubeda aliwachukua watoto wa Julieth na kukaa nao pembeni wakati yule dereva akiondoka. Julieth alitaka kuingia ndani moja kwa moja lakini Zubeda alimzuia.
 “Julieth wadogo zako na mama yako hawapo hapa.” Zubeda alianza kueleza.
Kama nilivyokudokeza mama yako aliugua sana, tulikutafuta kwenye simu yako ili utume fedha za matibabu bila mafanikio. Kwa vile mama yako alikuwa hana pesa ikabidi auze simu yake ili apate pesa za matibabu.”
“Oh! Samahani sana. Simu yangu iliharibika nikawa na simu nyingine. Lakini namba ya mama ninayo, ila nilishawahi kumpigia lakini haikupatika.  Labda ndo kipindi alipoiuza. Aliongea Julieth kwa masikitiko.”


 “Lakini mbona hata mume wako tulimpigia simu hakupokea, tuliamua kumtumia ujumbe lakini hakujibu. Hivi kwa nini mlikuwa mnafanya hivi?” Aliendelea kuhoji Zubeda huku Julieth akimsikiliza kwa makini sana.

“Ni histora ndefu hebu nitulie kwanza nitakusimulia siku nyingine wewe ni rafiki yangu sitakuficha kitu. Eh! Hebu niambie mama na wadogo zangu wanaishi wapi sasa?” Julieth alihoji zaidi.

 “Wadogo zako waliondoka kutokana na kushindwa kulipa kodi ya nyumba, kwa sasa sijui watakuwa wapi.” Alijibu Zubeda.
“Eh! Na mama?. Aliuliza Julieth.
Zubeda alimwangalia usoni Julieth ambaye alikuwa akionyesha uso wenye maswali mengi sana. Kwa muda wa dakika moja hivi Zubeda aliwaza na kutaka kumdanganya Julieth kuhusu aliko mama yake. Lakini mwisho aliamua kumwambia ukweli.
“Baada ya kuugua kwa muda mrefu mama yako ali…” Alisita kidogo Zubeda.
“Alifanya nini?.” Julieth aliuliza.
“Alifariki dunia.” Zubeda alijibu huku akimpa pole Julieth.
Julieth aliyekuwa amesimama alipiga kelele na kuanguka chini puu! Huku nguvu zikimwishia. Alilia sana kama mtoto aliyeungua moto.
 “Mamaaa! Mamaaa! Mama yangu wee! Upo wapa mama! Siamini nipeleke nikamwone. Nipeleke! Nipeleke!” Aliendelea kulia, kugagaa chini na kutamka maneno mbalimbali kwa uchungu sana. Hata hivyo haikusaidia kitu mama yake alikuwa ameshafariki na kuzikwa siku nyingi sana.

 Julieth alikuwa ameishiwa nguvu kabisa hivyo Zubeda aliwabeba watoto wote. Ilikuwa yapata kama saa mbili hivi za usiku, Julieth alinyanyuka kwa nguvu za ajabu na kugonga geti la nyumba aliyokuwa akiishi mama yake huku akiita ;
“Mama fungua mimi mtoto wako Julieth nimerudi.”
Hapo kuna mpangaji mwingine Julieth unawasumbua watu bure.” Zubeda alimkataza Julieth. Lakini Julieth hakutaka kumsikiliza. Kutokana na geti kugongwa kwa nguvu alitoka kaka mmoja na kufungua.
“Vipi dada una matatizo gani?” Aliuliza yule kaka.
“Yuko wapi mama yangu, namtaka mama yangu.” Aliuliza Julieth huku akilia na akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa.

Yule kaka hakumwelewa anachozungumza akabaki anamshangaa. Ghafla Julieth alianguka chini na kuzimia. Yule kaka na Zubeda walisaidiana kumnyanyua Julieth na kumwingiza ndani kisha wakamlaza chini huku feni ikimpepea. Yule kaka akamuuliza Zubeda aliyekuwa amewabeba watoto wa Julieth.

 “Vipi huyu mwenzio ana matatizo gani?” Aliuliza yule kaka.
Zubeda akamwelezea kila kitu yule kaka ambaye ndiye mpangaji mpya katika ile nyumba, alimwonea huruma sana Julieth. Baada ya Julieth kuzinduka aliendelea kulia asijue nini cha kufanya kwa yote yaliyomkuta. ITAENDELEA SURA YA 12......................

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

mmmh! jamani very sad!

Bila jina alisema ...

So sad jamani...... Mungu akupe nguvu na afya njema uendelee kutupa burudani sambamba na kutuelimisha. wasimuliaji wengine au wamechoka au hawataki tu kutusimulia bali wewe pamoja na umri wako mdogo Mungu akuongoze uzidi kutupa raha mpendwa

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom