Jumatatu, Julai 15, 2013

SIMULIZI....BADO MIMI......SEHEMU YA .....27........


ILIPOISHIA
Nilimshika  mikono huku nikimbembeleza kwasababu alikuwa na hofu sana nilimchukua na kwenda naye sebuleni kisha nikamuuliza taratibu. Kilichonishangaza Renata alinisimulia ndoto aliyokuwa anaiota ilikuwa inafanana vilevile na ndoto ya kutisha niliyokuwa nikiota.Nikiwa na hofu kubwa  na wasiwasi Charito alinitizama na kusema "Usiwe na wasiwasi mke wangu, haya ni majaribu ya shetani, kuwa na imani na Mungu kila kitu kitaenda sawa , usiogope chochote kwani shetani atashindwa kwa nguvu zake Mungu". JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE ....SURA YA ........27...

INAPOENDELEA
Nilikuwa na wasiwasi na mawazo mengi sana kichwani,  na hata kujiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu kwani sikuelewa ni kwanini, maisha yangu yanaendelea kupata majaribu na wakati nimekwisha mpokea Mungu katika maisha yangu. Siku zilienda huku nikiwa naota ndoto za ajabu kila kukicha wakati mwingine nilikuwa nashindwa kulala kabisa, kutokana na hofu.

Siku moja nilikuwa nimeketi sebuleni huku nikiwaza “Hivi  inawezekana hii nyumba ya Mama Bilionea imezindikwa na nguvu za giza ambazo haziwezi kuisha, na sasa mbona tunasali na kukemea nguvu za giza kila siku  kwanini hali hii inajirudia, yaani mimi nimechoka na hii hali, haya ni mateso jamani ni bora nimwambie mume wangu tuondoke katika hii nyumba vinginevyo na wasiwasi linaweza kutokea tatizo”. Nilikuwa na mawazo mengi sana siku hiyo, nikiwa naendelea kuwaza, Renata alikuja na kuketi karibu yangu huku akiwa amenyamaza kimya bila ya kuzungumza chochote.

Nilimtizama  Renata na kusema “Renata mbona upo kimya sana, na tena unaonekana mnyonge vipi una matatizo mdogo wangu?” Renata alinyama kimya kidogo na kisha akanijibu “Dada, hata nikikueleza matatizo niliyonayo, wewe hauniamini, mimi usiku naona vitu vya ajabu, halafu kinachonishangaza wakati mwingine namuona shemeji Charito akija chumbani kwangu usiku huku akionekana kuwa katika umbo la ajabu na pia....” Kabla Renata hajamaliza kuzungumza nilimkatisha na kusema  “Sikiliza nikuambie Renata, hizo ni ndoto tu na hazina maana mbaya, na pia kumbuka kusali kabla ya kulala kwani hayo ni majaribu ya shetani, anaweza kukufanya wewe umchukie  shemeji yako” Renata alinyanyuka kwa hasira pale alipokuwa amekaa na kusogea karibu yangu “Nilijua tu, hauwezi kuniamini lakini dada kumbuka usilolijua ni sawasawa na usiku wa kiza kinene, mimi naongea ukweli na wala siyo ndoto”.

 Nilishangaa kumuona Renata katika hali ile, ikanibidi niwe mkali kidogo “Unajua Renata wewe ni mtoto mdogo sana kuzungumza na mimi kwa sauti kali kiasi hicho, mimi ni dada yako mkubwa na inabidi uniheshimu lakini sasa naona unapoelekea nitakuja kukupiga nikuumize vibaya, sijaipenda kabisa tabia yako, embu toka hapa sitaki kukuona nisije nikakunyofoa huo mdomo wako mchafu.” Renata aliondoka huku akisema “Sawa dada lakini ipo siku utaniamini”.


Nilibaki pale sebuleni huku nikizungumza na nafsi yangu “Sijui huyu mtoto amepatwa na pepo gani jamani, yaani Renata ni wa kunipandishia sauti kana kwamba tunalingana, mjinga sana.” Nilikuwa najisemesha peke yangu, baadaye niliingia jikoni kuandaa chakula.

Baada ya miezi miwili kupita, siku moja niliamka nikiwa najisikia nimechoka sana  huku mwili wangu ukiwa na joto kali sana, nilijihisi naumwa hivyo ilinibidi niende Hospitali kupima. Nikiwa nimeongozana na mume wangu Charito  tulifika hospitali na Daktari alinitaka nipime haja ndogo pamoja na damu. Baada ya vipimo nilikaa takribani robo saa na kwenda kuchukua majibu.

Vipimo vilionyesha kuwa nilikuwa nina ujauzito. Nilifurahi sana huku nikimkumbatia mume wangu kwa furaha “Charito, hatimaye sasa na mimi nitakuwa mama na wewe utakuwa Baba, namshukuru sana Mungu  leo ni siku ya furaha sana” Charito alionyesha tabasamu usoni huku akisema “Nimefurahi pia mke wangu, Mungu ni mwema”. Baadaye Daktari alinishauri, nipendelee kunywa maji kwa wingi na kula mbogamboga na matunda.

Tulirudi nyumbani tukiwa na furaha sana. Baada ya kuingia ndani nilimkuta Renata akiwa ameketi chini ya mti uliokuwepo pale nyumbani, huku akilia na kutetemeka, niliogopa sana kumuona katika ile hali na  haraka nilisogea karibu na kumuuliza ana matatizo gani “Umepatwa na kitu gani Renata?” Renata alinijibu huku akiendelea kilia “Tumaini, Tumaini, Dada Kandida Tumaini” Nilishindwa kumuelewa ikanibidi nimshike mikono “Tumaini kafanya nini? Yuko wapi Tumaini”  Nilihisi kuna jambo baya litakuwa limepata mdogo wangu Tumaini.  “Tumaini amepotea, alitoka nje akiwa anakimbia na hajarudi tena, na mimi nilikuwa nilimfuata na kumtafuta bila mafanikio” Nilinyamaza kimya kidogo na kutafakari “Inamaana Tumaini atakuwa ameenda wapi? Na pia hajawahi kutoka akiwa peke yake hata siku moja, na kwanini amekimbia? Au kuna mtu amemtorosha  mdogo wangu”

 Nilikuwa nawaza huku Renata akinitikisa mkono kwa nguvu na kunivuta “Dada twende tukamtafute Tumaini, twende dada” Wakati huo Charito alikuwa amesimama pembeni na kusema “Inawezekanaje mlinzi alikuwepo hapa getini halafu mtoto anakimbia anashindwa kumrudisha, sasa atakuwa amekimbilia wapi, si unajua Dar es salaam ni kubwa” Alisema Charito huku akiwa anaelekea kumtafuta mlinzi na mimi nikawaza kuwa hawezekani Tumaini akawa ameenda  sehemu ya mbali labda atakuwa maeneo ya karibu, haraka nilitoka nje na kuanza kuwauliza majirani JE NINI KITAENDELEA USIKOSE...... SEHEMU YA........28.........

Maoni 5 :

Bila jina alisema ...

Tatizo la kandida ni libishi sana kama moursin mbaraka wa misri, hataki kuckia wala kuambiwa na mdogo wake. atakiona kitakachofuatia.

Bila jina alisema ...

Kadinda ananiuz ntamn nimnase vbao,htimae.linazaa jini,jitu gn bishi?????

Bila jina alisema ...

Daaah! tokea awali kaambiwa na renata lkn kandida hataki kusikia la mdogo wake. akumbuke kuwa kuckia kwa kenge mpaka avuje damu sikioni.

Bila jina alisema ...

Bora wahame kwenye hiyo nyumba ya huyo mama wakatafute nyumba nyingine, la sivyo wataanza kufa mmoja mmoja.

Unknown alisema ...

kadinda

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom