Ijumaa, Julai 11, 2014

SIMULIZI FUPI "AHADI FEKI"

"Unajua Sara mimi nakupenda sana na wewe ndiye chaguo la moyo wangu, siku zote nitakupenda bila kusikiliza maneno ya watu, usijali kuwa mimi nasafiri na kwenda nje ya nchi, kumbuka kamwe siwezi kukusaliti, nakupenda na siku moja tutakuja kufunga pingu za maisha" Alizungumza Yona huku akiwa anamtizama Sara aliyekuwa anaonekana kuwa na huzuni sana kutokana na maneno aliyokuwa akizungumza Yona. 

Kwa sauti ya upole akasema "Naumia sana moyoni, kila nikifikiria unaondoka na kwenda mbali huku nikiwa sijui lini tutakuja kuonana tena mpenzi, nakosa raha siwezi kuwa mbali na wewe, nitakukosa sana barafu wa moyo wangu" Sara aliongea huku machozi yakiwa yanamlengalenga, Yona alisogea karibu na kumkumbalitia kwa nguvu huku akimfariji. Zilikuwa zimebaki kama siku mbili Yona aanze safari ya kwenda nchini Uingereza. 


Mipango ya safari ilikamilika na siku hiyo Sara pamoja na ndugu zake na Yona walimsindikiza hadi Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere, wakiwa wanasubiri muda wa Yona kuingia ndani Sara alimsogelea Yona na kusema "Nakupenda sana Yona natamani usiondoke lakini sina namna, nakutakia safari njema na masomo mema tafadhali usinisaliti, kumbuka umeniacha Tanzania nakusubiri na..." Kabla hajamaliza kuongea machozi yalimdondoka na kuanza kulia kwa uchungu huku Yona akiwa amemkumbatia "Usijali Sara, mimi nakwenda kukaa mwaka mmoja tu halafu narudi, tafadhali usihuzunike sana, mimi nipo kwa ajili yako, na siku zote siwezi kusahau, ahadi yetu ya kuja kuishi pamoja, ubaki salama mpenzi wangu".

 Basi waliagana kwa huzuni na hatimaye muda wa safari kuanza ulifika na Yona aliondoka. Sara alikuwa katika kipindi kigumu sana kwani alikuwa amemzoea sana mpenzi wake muda mwingi walikuwa pamoja, hivyo ilimuwia vigumu sana kukubaliana na ile hali ya kubaki mpweke. Maisha yaliendelea na sasa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu pamoja na mitandao ya kijamii. Maisha ya Yona akiwa nchini Uingereza alikuwa ni mtu ambaye muda mwingi anautumia akiwa darasani kujisomea. Baada ya miezi saba kupita huku  wakiwa wanaendelea kuwasiliana, na Sara alikuwa akijitahidi kwenda kuwatembelea ndugu zake na Yona mara kwa mara.

 Ndugu zake na Yona siku zote waliamini kuwa Sara ndiye atakuja kuwa mke wa Yona pindi atakaporudi kutoka masomoni. Siku zilienda hatimaye ulibaki mwezi mmoja Yona arudi nchini Tanzania, kwa kipindi hicho cha mwezi huo wa mwisho mawasiliano kati ya Sara na Yona hayakuwa mazuri sana kwani kwa kipindi hicho Yona alikuwa ametingwa sana na mitihani. Ulipita muda kidogo hatimaye siku ya kurudi Tanzania ilifika sikuhiyo nduguzake na Yona waliandaa sherehe ya kumpokea Yona na moja kwa moja walimtumia kadi ya mwaliko Sara ili kuja kujumuika pamoja. 

Sikuhiyo Yona alifika usiku majira ya saa nne ambapo moja kwa moja alipokelewa na ndugu zake, kuelekea nyumbani, njiani Yona alikuwa akiwauliza mbona Sara hakufika kumpokea. Walimweleza kuwa atakuwepo nyumbani kwani wameandaa sherehe ndogo ya kumpokea, basi Yona alikuwa na shauku la kumuona mpenzi wake kwani ilikuwa ni muda mrefu hawakuonana, walipofika walipokelewa vizuri sana kwani kulikuwa na ndugu jamaa na marafiki, ambao walifika usiku ule, muda wote Yona alikuwa akipepesa macho huku na kule kutizama wapi alipo Sara, lakini hakumuona, hivyo ilibidi amuulize dada yake kwanini Sara hayupo.

 Ndipo dada yule akaamua kupiga simu ya Sara lakini kwa bahati mbaya hakupatikana hewani hata walipojaribu kupiga tena mara kwa mara bila mafanikio, Yona alipatwa na wasiwasi na sasa aliwaza kwenda nyumbani kwa kina Sara usiku uleule, ndipo moja kati ya marafiki zake akasema "Sara si anaishi maeneo ya Kijitonyama kuna siku nilimuona akiwa anatoka nje ya geti akaniambia pale ndiyo anapoishi." Basi Yona akaongozana na rafiki yake hadi kijitonyama usiku uleule kwani hakutaka kusubiri kesho alipofika walibisha hodi akafungua dada mmoja ambaye alibaki akiwashangaa ni kina nani? Na wanataka nini? Usiku ule ilikuwa ni majira ya saa tano usiku.

Walipomuulizia Sara yule dada akaingia ndani na kumuita, "Wifi, wifi kuna wageni huku," Alisema yule dada huku Sara akitoka ndani na kusema "Akina nani jamani usiku huu, jamani saa hizi nimechoka,....halafu, nina....pia" Alipata kigugumizi alipokutana uso kwa uso na Yona, huku Yona akiwa amepigwa butwaa kumuona Sara akiwa amejifunga kanga huku tumbo lake likiwa kubwa kuonyesha kuwa ni mjamzito. "Sara ni wewe, au naota jamani, kweli ni wewe siamini mimi jamani" Wakiwa wanaendelea kuongea ghafla alitokea kaka mmoja akiwa amejifunga taulo na kusema "kuna nini huko nje usiku huu jamani"

 Sara alimsogelea yule kaka mwenye taulo na kusema "Hakuna tatizo mume wangu, hawa ni wageni, wamepotea njia kwani walifikiri huyo mtu wanayemtafuta anaishi hapa" Basi yule kaka aliwataka waondoke kwani muda ule ulikuwa ni usiku sana, ndipo Yona na rafiki yake waliondoka huku Yona akiwa mwenye mawazo sana na hakutaka kurudi nyumbani aliamua kwenda bar kunywa pombe usiku kucha asubuhi alirudi nyumbani na kuwaeleza kila kitu ndugu zake walisikitika sana, "Siamini, kama Sara, amenitenda kiasi hiki, yaani kumbe ahadi zake ni feki imeniuma sana. Najuta kumpenda na kumuamini. "ZOTE NI AHADI FEKI"

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom