ILIPOISHIA
Nilisogea haraka na kumshika kwa nguvu. "Mungu wangu yaani Tumaini unampiga dada yako, wewe mtoto umechanganyikiwa" Nilimtizama katika midomo yake alikuwa amebaki na damu wakati nikiwa nataka kumfuta ile damu nilishangaa alinitoa mkono wangu huku akiilamba ile damu na kuimeza, Renata alikuwa analia sana nilibaki nimepigwa na butwaa nikimshangaa Tumaini kile alichokifanya kwani alionekana kama mtoto tofauti kabisa na Tumaini ambaye tulikuwa tumemzoea.
INAPOENDELEA
SEHEMU YA 30
Tumaini alikimbia na
kutoka nje, Nilimsogelea Renata na kuanza kumbembeleza ili anyamaze na asiendelee kulia, kwani
alikuwa analia sana kutokana nakuumia sana maeneo ya kwenye shingo ambapo Tumaini
ndiyo alikuwa amemn'gata, nilimshika mkono na kwenda kumpaka dawa ili damu
isiendelee kutoka, Wakati huo Tumaini alikuwa amejifungia chumbani kwake,
moyoni mwangu nilikuwa najiuliza maswali mengi sana kutokana na kile kitendo kilivyotokea, kwani nilishindwa kuelewa
kwanini Tumaini amemuumiza Renata kiasi kile, na kilicho nishangaza zaidi ni kile
kitendo cha kuilamba ile damu iliyokuwa imetapakaa kwenye mdomo wake na kisha
kuimeza.
Nilipatwa na mawazo mengi sana siku hiyo. Baadaye Renata alinyamaza
nilimpa na vidonge vya kumeza ili kutuliza maumivu, baadaye alipitiwa na
usingizi. Mimi niliendelea na kazi zangu kwani kwa wakati huo Tumaini alikuwa
amejifungia chumbani hata nilipojaribu kuugonga mlango kwa nguvu alikataa
kufungua.
Nilikwenda jikoni
kwaajili ya kuandaa chakula, ilipita kama nusu saa nikiwa naendelea na kazi
zangu ghafla nilisikia sauti kali sana, ya Renata akiniita “Dada Kandidaa,
nakufaaa Dada Kandidaaa njoooo” Nilishtuka na kukimbia sana hadi chumbani kwa
Renata nilimkuta akiwa amejikunyata kama mtu aliyemwagiwa maji ya baridi, kwani
alikuwa anatetemeka na jasho lilikuwa likimtoka kwa wingi, nilisogea karibu na
kumuuliza “Kuna nini Renata, mbona unapiga kelele, umepatwa na kitu gani?”
Renata alishuka kutoka kitandani na kunifuata kisha kunikumbatia kwa nguvu sana
aliendelea kulia huku akisema “Dada nimemuona mbwa mkubwa mweusi, alikuwa
anataka kuniuma, lakini wakati nataka kukimbia Yule mbwa alibadilika na
nikamuona Tumaini akiwa amesimama ananicheka, Dada mimi naogopaTumaini anataka
kuniua”
Aliongea Renata huku akionekana kuwa na hofu
nyingi sana, nilimshika mikono yake yote miwili na kumtizama usoni huku
nikisema “Wewe Renata, unasemaje? Yawezekana umeota ndoto mbaya, kwani Tumaini
ni mdogo wako hawezi kukudhuru, achana na hayo mawazo kabisa, nyinyi ni ndugu
inabidi mpendane, sasa huyo mbwa yuko wapi? Ulikuwa unaota mdogo wangu hakuna
kitu chochote kibaya” Nilimueleza Renata aliyekuwa ananitizama na macho yake
yakiwa yamejaa machozi alinijibu na kusema “Hapana dada, mimi naogopa siwezi
kulala peke yangu.” Niliendelea kumbembeleza, na hatimaye alinyamaza.
Tukiwa tumeendelea kukaa pale chumbani Tumaini
alikuja na kuchungulia, chumbani baada ya Renata kumuona Tumaini alishtuka
sana, na kunisogelea, Tumaini aliingia huku akionekana kuwa na hofu, nilimuita
kwa sauti ya upole “Tumaini, njoo mdogo wangu, njoo nikuambie mtoto mzuri”
Tumaini alisogea huku akionekana kutaka kuongea neno nilimkumbatia na kusema
“Tumaini kwanini umekuwa mtoto mtukutu, siyo vizuri kumpiga dada yako, sasa
inabidi umuombe msamaha unasikia mtoto mzuri, wewe na Renata ni ndugu
haipendezi mkiwa mnagombana, na Mungu hapendi kuona watu wakigombana, tizama
ulivyomuumiza dada yako, tafadhali usirudie tena sawa Tumaini”
Alinyamaza kimya kidogo
na kisha alimtizama Renata na kusema “Nisamehe Dada Rena, sintorudia tena,
nisamehe dada nitakuwa mtoto mzuri kuanzia leo” Renata alionekana kumuogopa
sana Tumaini niliwashika wote na kuwataka washikane mkono ikiwa ni ishara ya
kuwapatanisha. Ndipo Renata alikubali na walikumbatiana, na sasa waliendelea
kucheza pamoja bila matatizo.
Baada ya wiki moja Siku
moja Tumaini na Renata waliondoka asubuhi kwenda shule, ambapo Tumaini alikuwa anasoma darasa la tatu kwa
wakati huo, na Renata alikuwa darasa la tano, wote walikuwa wakisoma shule moja
iliyokuwa jirani na maeneo tuliyokuwa tunaishi inatwa (Kibo Academy) . Ilipofika jioni muda ambao walikuwa wakirudi
kutoka shule, alirudi nyumbani Renata peke yake, nilipomuuliza mbona Tumaini
hakuongozana naye alinijibu kuwa Tumaini aliwahi kuondoka kabla yake. Sikuwa na
wasiwasi sana kwani nilijua kuwa atarudi bila matatizo.Kwa wakati huo mume
wangu alikuwa hajarudi hivyo pale nyumbani tulikuwepo mimi na Renata.
Kama kawaida nikiwa
nimekaa na Renata alianza kuzungumza “Dada unajua mimi nahisi shemeji
anamfundisha Tumaini tabia mbaya, kwani ….” Kabla hajamaliza kuzungumza
nilimkatisha na kusema “Unajua wewe Renata, huwa unahisi mambo ya ajabu sana,
na umri ulionao, siyo kitu kizuri, jifunze kuwa na heshima, sasa shemeji yako
anawezaje kumfundisha tabia mbaya Tumaini, au wewe ndiyo umeanza tabia mbaya.
Sikiliza nikuambia kuanzia leo sitaki kusikia maneno yako yasiyokuwa na kichwa
wala miguu, nadhani tumeelewana” Renata alinitizama kisha alisimama na kusema
“Sawa dada nimekusikia, ila ipo siku Mungu atakufungua macho, utaona kile
ninachokiona”.
Nilibaki namtizama huku akiwa anataka kuelekea
chumbani ghafla mlango ulifunguliwa alikuwa ni Charito akiwa ameongozana na
Tumaini. Renata aligeuka na kumtizama shemeji yake kisha akasema “Shemeji,
umetoka wapi na Tumaini, Mbona Tumaini aliniaga kuwa anakuja nyumbani?”
Nilishangaa kumuona Renata akiuliza swali lile tena akionekana kuwa na jazba,
nilisimama na kusema, “Hivi wewe mtoto una akili kweli? Funga bakuli lako na
kwenda zako chumbani, mjinga mkubwa, unaongea na shemeji yako kama unaongea na
mtoto mdogo, nitakuja kukubamiza sikumoja hadi ushike adabu yako” Niliongea kwa
jazba kwani niliona sasa Renata anataka kuniaibisha. Charito alitabasamu na
kusema “Kandida usimgombeze mtoto kiasi hicho anayo haki ya kuuliza, Nimemkuta
Tumaini anacheza njiani wakati nakuja nikamchukua na kuja naye nyumbani”.
Tuliendelea na mzungumzo na baadaye
niliandaa chakula cha usiku.
Kesho yake asubuhi na
mapema alikuja mwalimu aliyekuwa anafundisha katika shule wanayosoma wadogo
zangu, wakati huo wadogo zangu pamoja na Charito walikuwa wamekwi shaondoka.
Mwalimu huyu alikuja kunipa taarifa ya msiba uliotokea shuleni “Dada ujio wangu huu ni kuhusu taarifa za
msiba, jana kuna mtoto alifariki baada ya kun’gatwa na mbwa, wakati akiwa anacheza
na watoto wenzake, pia alikuwepo na mdogo wako Tumaini, nimekuja kukujuza
kwasababu kwa niaba ya wanafunzi waliokuwa pamoja wanasema kuwa walimuona
Tumaini akiwa ameongozana na mbwa huyo, sasa sijui huyo mbwa yupo hapa
nyumbani” ? JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 31.
Maoni 2 :
Adela simulizi ya Bado mimi sehemu ya 31 iko wapi?
Adela am still waiting to know the chapter 31 of Bado mimi...........
Chapisha Maoni