Jumatano, Agosti 20, 2014

SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 30


 ILIPOISHIA
Nilisogea haraka na kumshika kwa nguvu. "Mungu wangu yaani Tumaini unampiga dada yako, wewe mtoto umechanganyikiwa" Nilimtizama katika midomo yake alikuwa amebaki na damu wakati nikiwa nataka kumfuta ile damu nilishangaa alinitoa mkono wangu huku akiilamba ile damu na kuimeza, Renata alikuwa analia sana nilibaki nimepigwa na butwaa nikimshangaa Tumaini kile alichokifanya kwani alionekana kama mtoto tofauti kabisa na Tumaini ambaye tulikuwa tumemzoea. 

INAPOENDELEA
SEHEMU YA 30
Tumaini alikimbia na kutoka nje, Nilimsogelea Renata na kuanza kumbembeleza ili anyamaze na asiendelee kulia, kwani alikuwa analia sana kutokana nakuumia sana maeneo ya kwenye shingo ambapo Tumaini ndiyo alikuwa amemn'gata, nilimshika mkono na kwenda kumpaka dawa ili damu isiendelee kutoka, Wakati huo Tumaini alikuwa amejifungia chumbani kwake, moyoni mwangu nilikuwa najiuliza maswali mengi sana  kutokana na kile kitendo  kilivyotokea, kwani nilishindwa kuelewa kwanini Tumaini amemuumiza Renata kiasi kile, na kilicho nishangaza zaidi ni kile kitendo cha kuilamba ile damu iliyokuwa imetapakaa kwenye mdomo wake na kisha kuimeza. 

Nilipatwa na mawazo mengi sana siku hiyo. Baadaye Renata alinyamaza nilimpa na vidonge vya kumeza ili kutuliza maumivu, baadaye alipitiwa na usingizi. Mimi niliendelea na kazi zangu kwani kwa wakati huo Tumaini alikuwa amejifungia chumbani hata nilipojaribu kuugonga mlango kwa nguvu alikataa kufungua.

Nilikwenda jikoni kwaajili ya kuandaa chakula, ilipita kama nusu saa nikiwa naendelea na kazi zangu ghafla nilisikia sauti kali sana, ya Renata akiniita “Dada Kandidaa, nakufaaa Dada Kandidaaa njoooo” Nilishtuka na kukimbia sana hadi chumbani kwa Renata nilimkuta akiwa amejikunyata kama mtu aliyemwagiwa maji ya baridi, kwani alikuwa anatetemeka na jasho lilikuwa likimtoka kwa wingi, nilisogea karibu na kumuuliza “Kuna nini Renata, mbona unapiga kelele, umepatwa na kitu gani?” Renata alishuka kutoka kitandani na kunifuata kisha kunikumbatia kwa nguvu sana aliendelea kulia huku akisema “Dada nimemuona mbwa mkubwa mweusi, alikuwa anataka kuniuma, lakini wakati nataka kukimbia Yule mbwa alibadilika na nikamuona Tumaini akiwa amesimama ananicheka, Dada mimi naogopaTumaini anataka kuniua”

 Aliongea Renata huku akionekana kuwa na hofu nyingi sana, nilimshika mikono yake yote miwili na kumtizama usoni huku nikisema “Wewe Renata, unasemaje? Yawezekana umeota ndoto mbaya, kwani Tumaini ni mdogo wako hawezi kukudhuru, achana na hayo mawazo kabisa, nyinyi ni ndugu inabidi mpendane, sasa huyo mbwa yuko wapi? Ulikuwa unaota mdogo wangu hakuna kitu chochote kibaya” Nilimueleza Renata aliyekuwa ananitizama na macho yake yakiwa yamejaa machozi alinijibu na kusema “Hapana dada, mimi naogopa siwezi kulala peke yangu.” Niliendelea kumbembeleza, na hatimaye alinyamaza.

 Tukiwa tumeendelea kukaa pale chumbani Tumaini alikuja na kuchungulia, chumbani baada ya Renata kumuona Tumaini alishtuka sana, na kunisogelea, Tumaini aliingia huku akionekana kuwa na hofu, nilimuita kwa sauti ya upole “Tumaini, njoo mdogo wangu, njoo nikuambie mtoto mzuri” Tumaini alisogea huku akionekana kutaka kuongea neno nilimkumbatia na kusema “Tumaini kwanini umekuwa mtoto mtukutu, siyo vizuri kumpiga dada yako, sasa inabidi umuombe msamaha unasikia mtoto mzuri, wewe na Renata ni ndugu haipendezi mkiwa mnagombana, na Mungu hapendi kuona watu wakigombana, tizama ulivyomuumiza dada yako, tafadhali usirudie tena sawa Tumaini” 

Alinyamaza kimya kidogo na kisha alimtizama Renata na kusema “Nisamehe Dada Rena, sintorudia tena, nisamehe dada nitakuwa mtoto mzuri kuanzia leo” Renata alionekana kumuogopa sana Tumaini niliwashika wote na kuwataka washikane mkono ikiwa ni ishara ya kuwapatanisha. Ndipo Renata alikubali na walikumbatiana, na sasa waliendelea kucheza pamoja bila matatizo.

Baada ya wiki moja Siku moja Tumaini na Renata waliondoka asubuhi kwenda shule, ambapo  Tumaini alikuwa anasoma darasa la tatu kwa wakati huo, na Renata alikuwa darasa la tano, wote walikuwa wakisoma shule moja iliyokuwa jirani na maeneo tuliyokuwa tunaishi inatwa (Kibo Academy) . Ilipofika jioni muda ambao walikuwa wakirudi kutoka shule, alirudi nyumbani Renata peke yake, nilipomuuliza mbona Tumaini hakuongozana naye alinijibu kuwa Tumaini aliwahi kuondoka kabla yake. Sikuwa na wasiwasi sana kwani nilijua kuwa atarudi bila matatizo.Kwa wakati huo mume wangu alikuwa hajarudi hivyo pale nyumbani tulikuwepo mimi na Renata.

Kama kawaida nikiwa nimekaa na Renata alianza kuzungumza “Dada unajua mimi nahisi shemeji anamfundisha Tumaini tabia mbaya, kwani ….” Kabla hajamaliza kuzungumza nilimkatisha na kusema “Unajua wewe Renata, huwa unahisi mambo ya ajabu sana, na umri ulionao, siyo kitu kizuri, jifunze kuwa na heshima, sasa shemeji yako anawezaje kumfundisha tabia mbaya Tumaini, au wewe ndiyo umeanza tabia mbaya. Sikiliza nikuambia kuanzia leo sitaki kusikia maneno yako yasiyokuwa na kichwa wala miguu, nadhani tumeelewana” Renata alinitizama kisha alisimama na kusema “Sawa dada nimekusikia, ila ipo siku Mungu atakufungua macho, utaona kile ninachokiona”.

 Nilibaki namtizama huku akiwa anataka kuelekea chumbani ghafla mlango ulifunguliwa alikuwa ni Charito akiwa ameongozana na Tumaini. Renata aligeuka na kumtizama shemeji yake kisha akasema “Shemeji, umetoka wapi na Tumaini, Mbona Tumaini aliniaga kuwa anakuja nyumbani?” Nilishangaa kumuona Renata akiuliza swali lile tena akionekana kuwa na jazba, nilisimama na kusema, “Hivi wewe mtoto una akili kweli? Funga bakuli lako na kwenda zako chumbani, mjinga mkubwa, unaongea na shemeji yako kama unaongea na mtoto mdogo, nitakuja kukubamiza sikumoja hadi ushike adabu yako” Niliongea kwa jazba kwani niliona sasa Renata anataka kuniaibisha. Charito alitabasamu na kusema “Kandida usimgombeze mtoto kiasi hicho anayo haki ya kuuliza, Nimemkuta Tumaini anacheza njiani wakati nakuja nikamchukua na kuja naye nyumbani”. Tuliendelea na mzungumzo na baadaye  niliandaa chakula cha usiku.


Kesho yake asubuhi na mapema alikuja mwalimu aliyekuwa anafundisha katika shule wanayosoma wadogo zangu, wakati huo wadogo zangu pamoja na Charito walikuwa wamekwi shaondoka. Mwalimu huyu alikuja kunipa taarifa ya msiba uliotokea shuleni  “Dada ujio wangu huu ni kuhusu taarifa za msiba, jana kuna mtoto alifariki baada ya kun’gatwa na mbwa, wakati akiwa anacheza na watoto wenzake, pia alikuwepo na mdogo wako Tumaini, nimekuja kukujuza kwasababu kwa niaba ya wanafunzi waliokuwa pamoja wanasema kuwa walimuona Tumaini akiwa ameongozana na mbwa huyo, sasa sijui huyo mbwa yupo hapa nyumbani” ? JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 31.

Maoni 2 :

Unknown alisema ...

Adela simulizi ya Bado mimi sehemu ya 31 iko wapi?

Unknown alisema ...

Adela am still waiting to know the chapter 31 of Bado mimi...........

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom