Wakati huo mchungaji alikuwa akiendelea kusali sana “Nasema utatoka tu, muachie huyu mtoto uondoke zako, sasa hivi natuma moto, ukutokomeze kabisa toka kwenda zako, huu ndiyo mwisho wako nimesema toka katika jina la Mungu Baba muumba Mbingu na Nchi. Tumaini aliendelea kutapatapa na mara ghafla alinyamaza na kutulia kimya kabisa, nilikuwa na hofu sana huku nikitetemeka lakini mchungaji James alinisihi nisiwe na hofu na kunitaka niketi, kwani kuna mambo ambayo alikuwa akitaka kuniuliza kuhusu maisha yangu. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 34
INAPOENDELEA
Bado nilikuwa
nikimtizama Tumaini, akiwa amelala chini kwenye zulia, huku
nikiwa na wasiwasi sana, lakini mchungaji aliendelea kunisisitiza nisiwe
na hofu “Usiogope Kandida Tumaini amepumzika kutokana na uchovu, wa shetani
aliyekuwa ndani yake, sasa akiamka atakuwa hana tatizo kabisa kwani shetani
amekwisha ondoka na sasa atakayezinduka atakuwa ni Tumaini mdogo wako,usiwe na
hofu kabisa kwani Mungu ni mwema na ametenda maajabu yake.
Jambo nililokuwa nataka
kufahamu ni kuhusu maisha ya familia yenu kwa ufupi, kwani inavyoonekana kuna
mambo mengi ambayo yanahusisha nguvu kali za giza” Aliuliza mchungaji huku
akinitazama, nilishusha pumzi kidogo na kuanza kumsimulia maisha yangu yote
tangu kufariki kwa wazazi wangu, pamoja
na maisha niliyokuwa nikiishi na Mama Bilionea, na pia sikusita kumueleza
kilichonisibu nilipoenda kwenye hekalu la Bibi Bilionea.
Mchungaji alinisikiliza kwa umakini sana huku
akiwa anatikisa kichwa akasema “Inamaana huyo Bibi bilionea aliyekuwa anatajwa
wakati namuombea Tumaini wewe unamfahamu? Mungu wangu, Umeishi na nguvu za giza
sikunyingi sana Kandida, sasa huyo mchungaji ambaye amekuwa akiwasaidia siku
zote mlikutana naye wapi? Aliuliza mchungaji kwa masikitiko makubwa “ Mchungaji
Mkombozi nilikutana naye siku niliyokuwa nakimbia pamoja na wadogo zangu kutoka
katika nyumba ya Mama Bilionea, ndipo nilipoanza kupata msaada kutoka katika
kanisa lake, na nikiwa katika kanisa hilo nilikutana na Charito ambaye ndiye
mume wangu aliyekuwa ameongozana na Tumaini muda mfupi uliopita”.
Mchungaji
alinisikiliza na baadaye alinyanyuka na kisha akamtizama Renata aliyekuwa
ameketi huku amemshika Tumaini, na moja kwa moja akamuuliza “Kwanini ulikuwa
unasema Mchungaji Mkombozi, pamoja na shemeji yako siyo watu wazuri, je kuna
kitu chochote kibaya ulishawahi kukiona?” Renata bila ya kusita akaanza kusema
“Ndiyo, Mchungaji Mkombozi alinijia kwenye ndoto akiwa ameshika kitambaa
chekundu kinachovuja damu, huku akinitizama kwa hasira na kusema kuwa zamu
yangu ikifika atanichukua, na ndoto hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara, vivyo
hivyo kwa shemeji Charito amekuwa akinijia na kutaka kuniua, lakini kila
nikishtuka simuoni na kitu ninachokiona ni mbwa, hali hii inanitisha sana
Mchungaji kwani wakati mwingine mimi huwa naona shemeji anabadilika na kuwa
kama mbwa kabisa, nimekuwa nikimueleza dada Kandida lakini aniamini kile ninachomueleza”.
Renata akiwa anazungumza nilimtizama huku nikiwaza “Hivi huyu mtoto anajua
anachokizungumza kweli, yaani Charito awe mbwa, na tena mchungaji Mkombozi
atake kumuua mmmh sijui jamani haya ni mauzauza gani?” Haraka nilimtizama
mchungaji na kusema “Hapana mchungaji hizo ni ndoto tu, kwani mimi hata
sikumoja sijawahi kumuona mume wangu
akibadilika na kuwa mbwa….na pia…”
Mchungaji alinikatisha kabla sijaendela
kuzungumza na kusema “Kandida, kandida, kandidaaaaa,, fungua macho yako, mkaribishe
Mungu katika maisha yako, kumbuka ndoto mara nyingi huelezea ukweli wa mambo
ambayo yanaweza kutokea, ama yamekwishatokea, na siyo kila jambo ni la
kupuuzia, vilevile inawezekana wewe usione chochote kwasababu tu huamini na
moyo wako umefungwa, na macho yako ndiyo kabisa hayaoni mbele wala nyuma, hivyo
usiseme Renata ni muongo kwani huwezi kujua ukweli bila ya kumshirikisha Mungu
wetu wa kweli ambaye ni Muumba wa mbingu na nchi, ni wakati wako sasa kusali
sana, huku ukichunguza kile anachokueleza mdogo wako, pia nakukaribisha
kanisani uje pamoja na wadogo zako ikiwezekana mlete na mume wako, kwani njia
pekee ya kuepuka nguvu za giza ni kusali tafadhali usiache kusali hata maramoja”.
Alisisitiza
Mchungaji, Baada ya Muda Tumaini alishtuka huku akiwa anashangaa huku na kule
alinifuata huku akisema “Dada Kandida, njaa inaniuma, naomba chakula” Mchungaji
alimtizama huku akitabasamu na kusema
“Kandida ni vyema ukampa mdogo wako chakula sasa, huyu ndiye Tumaini wa kweli”
Renata alikuwa akifurahi na mimi nilinyanyuka na kwenda jikoni kuchukua
chakula, Baadaye mchungaji aliondoka huku akiendelea kusisitiza tusali sana.
Kwa wakati
wote ule, Charito hakurudi nyumbani hadi ilipofika majira ya saa mbili za usiku
ambapo alifika akiwa ameongozana na mchungaji Mkombozi, alipoingia alitukuta
tukiwa tumeketi sebuleni moja kwa moja mchungaji Mkombozi alianza kuzunguka
huku na kule bila ya kuketi akiwa anasema “Kandida kwanini unamjaribu Mungu
wetu, nimepata taarifa zako kuwa umemleta mchungaji mwingine kuja kuwaombea
hapa nyumbani, inamaana huniamini mimi? Aliuza mchungaji huku akinitizama kwa
kunikazia macho, Renata kama kawaida yake alikuwa wa kwanza kujibu kabla ya
mimi kuzungumza chochote “Samahani mchungaji, mimi sioni tatizo la Mchungaji
James kuja kutuombea, kwani yeye pia ni mtu wa Mungu, hata na hivyo kila mtu
anaruhusiwa kusali na kumuomba Mungu wakati wowote?”
Aliuliza Kandida huku
akimtizama mchungaji. Ghafla nilishangaa Charito alimsogelea Renata na kumpiga kibao katika
paji la uso wake “Mjinga mkubwa wewe, nilishakueleza kuwa ujifunze kufunga
bakuli lako, mtoto mdogo unajibizana na watu wakubwa kama wanalingana na wewe,
kaa chini na nisikusikie ukiongea chochote” Nilishtuka sana kuona kile kitendo na wakati huu nilipata ujasiri wa kuzungumza, na sasa sikumjibu mchungaji bali
niliamua kupambana na mume wangu Charito kwa kitendo chake cha kumpiga mdogo
wangu Renata “Sijapenda ulichokifanya Charito, sipendi kabisa mdogo wangu
anyanyasike, unawezaje kumpiga kiasi hicho, tena mimi sijaona kosa lake
alichokizungumza ni kitu cha kawaida”.
Charito alinitizama na kusema “Kumbe wewe
ndiye unayemfundisha Renata tabia mbaya aliyonayo, sasa sikiliza mimi ni mume
wako, kile ambacho nakiona hakipo sahihi na sipendezwi nacho lazima nikiweke
sawa, huyu mtoto hana adabu ndiyo maana nimempiga, na pia usitake kujibizana na
mimi wakati leo umenikera sana kuleta mtu nisiyemfahamu hapa nyumbani, huyo anayejiita
mchungaji James, au ni hawara yako unaficha” Aliongea Charito kwa kujiamini
nilinyamaza kimya bila kujibu chochote huku moyoni mwangu nikisema “Mungu
naomba unipe ujasiri, niepukane na haya majaribu” Mchungaji Mkombozi
alinigeukia tena na kusema “Nimekuuliza
swali Kandida,”.
Nilimtizama kwa dakika chache na kisha nilimjibu
“Namuamini Mungu pekee aliyejuu, mchungaji mimi naweza kusali popote alimradi
Mungu wetu ni mmoja ambaye tunamtumikia kwa nguvu zote na si kwamba kwasababu
nimeombewa na mchungaji James, basi nitashindwa kusali katika kanisa lako
hapana, mimi naamini Mungu yupo nasi popote pale tulipo na sioni tatizo
kuombewa na mchungaji James.” Mchungaji alinyamaza kimya kidogo kana kwamba kuna jambo anatafakari kisha akasema.
“Sawa Kandida, lakini kumbuka kuwa makini, kwani unaweza kujiona upo sahihi lakini, madhara yake ni makubwa sana”
Aliongea mchungaji huku akiniaga na kusema “Mimi naondoka, lakini
nakusisitiza tena kuwa makini, kwani jambo ulilolifanya ni kosa kubwa sana katika kanisa letu,
nakutakia usiku mwema” Aliondoka mchungaji na kutuacha. Siku hiyo Charito
alikuwa amekasirika sana, niliwasindikiza wadogo zangu kwenda kulala, na mimi
nikarudi chumbani kwangu kupumzika Charito alikuwa amenyamaza kimya bila ya
kunisemesha kwa usiku huo.
Kwa upande wa
Renata akiwa amelala usiku majira ya saa nane alimuona mchungaji akiwa
ameongozana na Charito, wakiwa chumbani kwake huku wakiwa wamevalia mavazi ya
rangi nyekundu, Renata aliwauliza “Mnataka nini chumbani kwangu?” Charito
alicheka sana huku akimwambia “Bado wewe, Bado wewe Renata” Kwa hofu kubwa
Renata alijikunyata pale kitandani na kuuliza tena “Bado Mimi, Bado mimi wapi?
Kwenye nini? Aliuliza huku akitetemeka “Tumekula nyama ya Baba yako na Mama
yako, pamoja na nyama ya Mtoto wa dada yako akiwa tumboni sasa ni zamu yako,
Bado wewe Renata, Bado weweeeeeeeee”.
Sauti ilizidi kupaa juu kwa ukali
ikiambatana na kicheko cha cha ajabu, Renata alipata hofu zaidi na wakati huu
Charito alikuwa ameshikilia kisu kilichokuwa kinatiririsha damu mithili ya maji
yaliyofunguliwa bombani, alikuwa akimsogelea Renata ambaye alipiga kelele
kuomba msaada “Mamaaaa nakufaaa, nisaidieni jamani nakufaaaaa Mungu wangu
nisaidieeeeee mamaaaaaa” Ilikuwa ni sauti kali sana, Kandida aliisikia sauti ya Renata akiwa
chumbani na alishtuka moja kwa moja alikimbilia chumbani kwa Renata.JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA 35.
Maoni 1 :
Ooh jamani Renata
Chapisha Maoni