Ndipo nilipokutana na Jesca,
niliwahi kuwa mwanafunzi hivyo nilijua kila kitu, Jesca hakuwa na nia ya kuja
chooni lakini nia yake ilikuwa kufuata majibu aliyokuwa ameyahifadhi chooni, nilimuona alipoyahifadhi na hata
alipoenda kuyachukua nilimuona pia. Lakini licha ya kumuona yeye pia kuna kitu
nilikigundua, kuwa kuna mwalimu alikuwa ameyaona yale majibu na alikuwa
anategea amwone aliyeyaweka, nilimtambua mwalimu Temba maana alikuwa anaogopwa
sana na kuna wakati alikuwa akitugeuzia kibao hata sisi ambao aliamini
tunaokota mabaki ya chakula kile kwa ajili ya bata nyumbani, hakujua mimi
nilikuwa nakula chakula kile.
Yule binti alivyotoka darasani nami nikasimama
ilimradi tu nipishane naye, nikajifanya namuulizia kitu, akanitazama kwa hasira
kali. Bila shaka hakuvutiwa na ombi langu!! Sikutaka apige hatua mbele zaidi,
“dada mwalimu Temba amekutegea ameyaona majibu yako!! Usiende!” nilimwambia na
kuhakikisha amesikia kisha nikachukua hamsini zangu nay eye nikamwacha bila
kumtazama tena……sikujua nini kiliendelea lakini jioni Jesca alinitafuta!! Huo
ukawa mwanzo wa urafiki wetu, urafiki ulioniingiza katika jina jipya na MATESO
MAPYA!!
USIKU ulikuwa mrefu sana nikijiuliza ni nini
kilimsibu Nadia hadi kufikia hatua ya kuitwa Mariam. Hakika nilijaribu kuumiza
kichwa lakini hata kubabia nini kimemsibu nilishindwa. Nikatwaa dawa za maumivu na kujidunga kisha
nijilaza kitandani na kupitiwa na usingizi.
Asubuhi niliwahi sana kuamka nikajiandaa kisha
nikaenda chumbani kwa Nadia, siku hii niliamua kumfuata katika namna ya kuanzia
pale tulipoishia usiku uliopita, niliamua kukiuka kila ambacho nilikuwa
nimejipangia katika kuandaa maandiko haya kutoka katika maisha ya Nadia.
Nilifika na kugonga mlango ukafunguliwa, Nadia
alikuwa amechanuka na tabasamu jepesi usoni.
Nikamjulia hali, naye kanijulia hali yangu!!
Nikaketi, kisha nikanyanyua mkonga wa simu na
kuwapigia wahusika wa hoteli ile tayari kwa kutuandalia kifungua kinywa.
“Nimewaambia tayari kama ni chai au kuna jingine.”
Alinikatisha baada ya kuigundua nia yangu.
Nikamtazama akanikonyeza!!
“Silali fofofo kama wewe….”aliniambia na hapo
mlango ukagongwa akaenda kufungua.
Kwa mara nyingine tena ilikuwa ni kapuchino!!
Vikombe viwili!! Sijui alijuaje kama nami ningefika
kwa wakati.
Kila mmoja akatwaa kikombe chake!! Kimya kikatanda
wakati tukifungua kinywa!!
Nadia alipoona kimya kimetanda sana alichukua
rimoti na kuwasha luninga. Akakutana na muziki akaacha katika chaneli hiyohiyo.
Mara muziki ukamalizika kikafuata kipindi kingine, Nadia hakujishughulisha kubadili
chaneli badala yake akatabasamu akitazama ile luninga nami nikatazama nini
kinamfanya atabasamu!!
Kilikuwa ni kipindi cha kawaida tu!! Basi
nikajiongeza kuwa alikuwa na lake la ziada. Mara akatua kikombe chini
akanitazama. “Hivi na wewe umewahi kuingia studio?” aliniuliza.
Nami nikakitua kikombe changu chini. Kisha kwa kujiamini kabisa nikamjibu,
“Yaani mwandishi mzima kama mimi hadi leo niwe sijaingia studio?”
“Umenijibu ama umeniuliza swali?” aliniambia, mara
tukajikuta tumecheka wote kwa pamoja. “Nimewahi kuingia mara kwa mara Nadia.”
Nilijirekebisha hatimaye. “Mwenzangu, yaani namuangalia huyu mdada hapa
hajiamini kabisa sijui ni mara yake ya kwanza kuingia studio huyu?...maana dah!
Mi mwenyewe mara ya kwanza kuingia studio nilikuwa natetemeka kweli, yaani
studio bwana haijalishi wewe una degree wala nini yaani unaweza kuaibika. Mara
ya kwanza niliingia katika studio ya redio moja hapo Musoma inaitwa Victoria FM
ebwana wee mimi nilimwambia Jesca ukweli kuwa sijawahi kuingia studio,
akalazimisha kweli hadi tukaenda, sema hakuwa na nia mbaya, aliamua kunisaidia
kutokana na ukarimu wangu kwake.
Maana aliniapia kuwa laity kama angekamatwa
anaangalizia kwenye ule mtihani angewekewa sifuri kisha angefukuzwa shule na
kutakiwa kurudi na mzazi wake shuleni baada ya adhabu atakayokuwa amepewa
kumalizika. Ni katika maongezi hayo Jesca akanieleza kuwa anasomeshwa na mjomba
wake na ni mkali sana huku shangazi yake akiwa hampendi hata kidogo. Jesca
akataka kujua kidogo kuhusu mimi pia, hakuamini hata kidogo kuwa nimemaliza
chuo kikuu, akajiroga na kuanza kuzungumza nami kiingereza hapo nikampoteza
vibaya. Yaani alipotea kweli maana alikuwa na kiingereza cha kuungaunga huku
mimi nikiifurahia lugha ile.”
Hapa Nafia akasita kisha akatabasamu, bila shaka
aklifurahia sana kumbukumbu ile. Kisha akaendelea, “nilimweleza mengi sana
kuhusiana na masomo, naam Jesca akaniona mimi kuwa wa muhimu kwake,
akaniunganisha kwa rafiki yake mtaani nikaanza kuishi hapo huku akinipatia
shilingi kama elfu kumi na tano hivi na vifaa kadha wa kadha nikaanza kuuza
mihogo ya kukaanga. Hakika lilikuwa jambo jema, nilikuwa makini sana na yule
niliyeishi naye pia nilikuwa makini nisiropoke lolote zito kwa Jesca asije kuwa
kama waliotangulia, waliishia kunijua tu lakini mwisho wakanitenda.
Nilivuta
subira hadi nilipomzoea kisha nikamwamini Jesca ndipo nikaanza kumshirikisha
mambo yangu, na nilifanya hivyo kwa sababu tu alikuwa mtu wa kutafiti sana,
alikuwa akiniuliza maswali mengi na mara nyingine ni kama alikuwa akinirudisha
darasani kwani aliniomba nimsaidie mambo kadha wa kadha, nilipoweza nikasaidia
na niliposhindwa nikamweleza. Jesca akawa rafiki mwema!!
Swali lake gumu nililoshindwa kulijibu ni moja tu!!
Kwanini nipo hivyo wakati nimesoma hadi chuo kikuu??
Nilipomjibu kuwa baba yangu alichoma vyeti vyangu
na sasa sikuwa na ushahidi wowote wa elimu yangu likazaliwa swali jingine la
kwanini ilikuwa hivyo nikamweleza tena sababu moja baada ya nyingine, na
hatimaye nikajikuta nimemweleza juu ya Desmund!!
Simulizi ya maisha yangu ikambamba na kumliza
Jesca, akaamua kutafuta namna ya kunisaidia na mwisho akakutana na Abraham
Swea, mtangazaji wa redio Victoria katika vipindi mbalimbali kimojawapo
kikiwemo MAPITO.
Siku moja Jesca akanieleza kuwa Abraham alikuwa
akihitaji kufanya kipindi na mimi. Kipindi ambacho kitaniwezesha kupata msaada
wowote ule kwani yeye Jesca alikuwa anakaribia kumaliza shule hivyo lazima
ningeteseka sana. Hakika alikuwa amesema jambo la maana, nikakubaliana naye
lakini nikamweleza kuwa jina la Nadia ni jina chafu tayari linaweza kuniingiza
matatani. Sipo tayari kulitumia na watu walifahamu!! Sikutaka kumweleza
kiundani juu ya kesi ya mauaji niliyoamini kuwa inanikabili. Lakini alinielewa,
akazungusha kichwa huku na kule na mara akaanguka na jina ‘MARIAM’ akaniambia
kuwa nitumie jina la hilo badala ya Nadia.
“Ni jina la marehemu mama yangu!! Nilimpenda sana,
japo sikuwahi kumwona na siiikumbuki sura yake lakini niliambiwa na jamaa zake
kuwa nililia siku tatu mfululizo baada ya kufariki kwake.” Jesca alinipa sababu
ya kulitumia jina lile. Kwa sababu zake zile sikuweza kumpinga. Nikakubali kuwa
Mariam.
Siku mbili baadaye nikaingia studio kwa mara ya
kwanza, katika kipindi cha mapito. Kipindi ambacho kiliibadilisha tena historia
ya maisha yangu. Nilijieleza kwa umakini sana huku nikikwepa kulitaja jina la
Desmund, nikayaelezea magumu niliyopitiakatika jiji la Mwanza nikamtaja Jadida
kama dada yangu wa kuzaliwa, nikasimulia juu ya utata wa Musoma vijijini
nilipotaka kubakwa na akina Mwita. Hata kabla sijamaliza kusimulia Abraham alikuwa
anatokwa na machozi, waliopiga simu wote walikuwa wanalia. Hapo sasa nikagundua
kuwa mambo ambayo nilikuwa nimeyapitia hakutakiwa kuyapitia mwanadamu wa
kawaida. Huenda Nadia mimi sikuwa wa kawaida!!!
Nilipata misaada mbalimbali, lakini msaada moja mkubwa
ulikuwa ni kazi! Mzee mmoja alipiga simu akajitambulisha kama mzee Matata,
alikuwa ananingoja nitoke studio aweze kuonana nami aangalie uwezekano wa
kunipa ajira baada ya usaili. Maana nilisema kuwa eleimu yangu ni ya chuo kikuu
lakini vyeti vyangu viliungua katika ajali ya moto ambayo iliondoka na uhai wa
wazazi wangu wote wawili. Mzee Matata akawa ameguswa.
Nikiwa palepale studio nilipata msaada wa takribani
shilingi laki moja. Jambo jema kabisa.
Nilipotoka nje nilimkuta Jesca akiwa analia kwa
furaha na huzuni, alikuwa kikifuatilia kipindi kile moja kwa moja katika redio
ndogo aliyokuwa amekuja nayo.
Wakati nazungumza na Jesca, ndipo nikaitwa katika
gari moja ya kifahari kiasi. Aliyeniita alikuwa mzee Matata. Alikuwa na sura
iliyojaa majonzi tele! Akajitambulisha nami nikajitambulisha, mara akafika
Abraham tukaungana katika maongezi, maongezi juu ya ajira. Baada ya mazungumzo
akanipatia namba zake za simu, akanisihi nimpigie simu siku inayofuata.
Siku iliyofuata nikafanya kama alivyoagiza,
akanielekeza ofisi yake ilipokuwa, maeneo ya Mwisenge nje kidogo ya mji wa
Musoma. Ilikuwa ofisi iliyojishughulisha na mambo ya usafirishaji, nikawekwa
kama mwanafunzi wa majuma mawili nikawa mwepesi wa kuelewa na baada ya hapo
nikahamishiwa katika ofisi zilizokuwa maeneo ya Nyasho!!
Huku nikaanza kufanya kazi, huku kila siku
nikiamini kuwa kuna jambo sijalitimiza. Nilikuwa nadaiwa suala la kumkomoa
Desmund!! Nikaliweka kiporo hili huku kila siku nikiombea nisikutane naye, yeye
wala mkewe.
Ilikuwa kazi nzuri iliyonilipa vyema, mkurugenzi
alinipatia chumba katika nyumba yake, huko nikawa naishi na msichana wake wa
kazi. Yeye alikuwa akiishi nyumba kubwa pamoja na familia yake. Nilichezwa machale tangu mwanzo kuwa nikianza kula
vizuri tu nitapendeza, na hapo matatizo yataanza tena. Naam ukafikia ule wakati
wa Nadia ambaye wakati huo niliitwa Mariam kuanza kuumiza akili yangu.
Bosi alikuwa akinitaka kimapenzi!
Haya yalianza baada ya kuniandalia safari ya kikazi
kwenda Mwanza kwa ajili ya kuwafundisha kazi katika ofisi ya usafirishaji
jijini huko. Akanipangia hoteli nzuri, na baada ya siku mbili alifika usiku
kunijulia hali. Kwa sababu alikuwa mtu mzima sana mimi nilimkaribisha chumbani
kwangu. Huko akapata nafasi ya kunitamkia kuwa alihitaji kunioa.
Nilipepesa macho huku na kule na kutamani atoweke
mbele yangu, lakini alikuwa akingoja jibu langu.
Nikamtazama na bila kusita NIKAMKATAA!!
Hakuniaga akaondoka kisha akanitumia ujumbe kuwa
nifikirie mara mbili!! Lakini sikuwa na haja ya kufikiria mara mbili wala
kuhoji juu ya familia yake italichukuliaje jambo hilo, nilikuwa nimesimamia
hapo hapo kuwa SIMTAKI!!!
Hilo lilikuwa kosa klililonitupa katika kinywa
kingine kisichokuwa na huruma!!
Lakini labda kosa hilo lilikuwa dogo sana,
nikafanya dhambi kwake nikamweleza mfanyakazi mwenzangu juu ya jambo hilo,
sidhani kama nilifanya jambo sahihi.
Juma moja baadaye akanitumia ujumbe “NASIKIA
UMEWATANGAZIA WATU KUWA UMENIKATAA”….Nikajua yule mfanyakazi mwenzangu
amewasambazia watu wengine jambo hilo, ni mimi nilitakiwa kujilaumu.
Nilimpigia simu Jesca na kumweleza kila kitu,
akanitoa hofu na kunambia kuwa mzee yule ni mtu wa watu sana na anaheshimika
kutokana na moyo wake wa kujitolea, hawezi kunifanyia jambo lolote baya kitu
cha msingi nilitakiwa kumwomba msamaha!!!
Msamaha?? Nikajiuliza, msamaha kwa lipi sasa, yaani
amenitongoza nimemkataa nimwombe msamaha looh!….nikaamua kupuuzia. Huku
nikimdangaya Jesca kuwa nitamuomba msamaha mzee Matata.
Ni heri ningejifanya mjinga nimwombe msamaha kuliko
ukaidi nilioufanya!!!!
Usiku wa siku hiyo nikavamiwa pale chumbani,
sikuchukua dakika nikakutana na giza nene!! Bila shaka waliniwekea madawa
wanayojua wao!!
Nilipokuja kufumbua macho nikajikuta katika chumba
kikubwa sana na sikuwa peke yangu, tulikuwa wengi lakini ni mimi pekee nilikuwa
na afya tele. Wenzangu walikuwa wamekonda na walikuwa uchi wa mnyama, hawakuwa
wakijiweza hata kidogo japo macho yao wengine yalikuwa wazi na wengine walikuwa
wamesinzia. Hakuna aliyejishughulisha na mimi, chumba kilikuwa kina mwanga
lakini ni kama hawakuwa wakiona lolote.
Nilipogeuka kushoto nikakutana na kikaratasi.
“WAULIZE WENZAKO NINI KILIWASIBU…KISHA UJIANDAE NA
WEWE”
Mwandishi nilichanganyikiwa ujue yaani muda mfupi
uliopita nilikuwa katika chumba cha hoteli jijini Mwanza, sasa nipo katika
chumba cha ajabu sana na watu nisowafahamu tena wakiwa katika hali ya
utatanishi! Uchi wa mnyama!!, nilichanganyikiwa sana. Nikasimama niweze
kutafuta pa kutokea, nikajikuta nimekanyanga mkono wa mtu, sijui ulivunjika
ule!! Alilia sana..alilia na hakuwa na la kufanya, kama alidhani kuwa alinipiga
basi alikuwa amenipapasa tu!!
Nikahaha huku na kule!
Sikuupata mlango hata nilipofanikiwa kuzurura kila
kona!!!
MARA KIZA !! NILIPAGAWA
Niliita jina la Jesca, ni huyu aliyekuwa ndugu wa
pekee katika himaya yangu kwa wakati ule, ningeweza kuita mama lakini mama huyo
alikuwa amenimwagia laana tayari, mzee Matata ambaye alikuwa ameniajiri sijui
kama ndo huyu alikuwa ameniweka katika himaya hii ya kutisha ama vipi? Nilikosa
majibu mara nikauona mkoba wangu upesi nikaupapasa na kukutana na simu yangu ya
mkononi, nikaichukua upesi nikataka kupiga, nikakutana na neno ‘insert sim
card’, nikajiuliza ni muda gani niliitoa kadi yangu ya simu!! Sikukumbuka hata
kidogo!!....mwandishi kuna wakati niliwahi kuombea kifo lakini hapa nilikiogopa
sana, kifo cha kufa kimateso namna ile, haikutamanisha hata kidogo kuwatazama
watu wale waliokuwa kando yangu!! Bila shaka kabla ya kuwa vile walipitia
magumu sana!!!........” Nadia akanyamaza kisha akaangaza huku na kule. Kisha
akaniambia, “Tutelemke chini tukanunue maji nina kiu sana.”
Nikavaa makubadhi yangu nay eye akajitanda kiremba
chake tukafunga chumba na kutelemka chini!!! Huku nikiwa nina wahka wa kujua
nini kilijiri??? USIKOSE SEHEMU YA 16
Maoni 1 :
Dah!! Inasisimua sana, dada della uwe unaweka hadithi hii hata mara 3 kwa wiki, inasikitisha sana
Chapisha Maoni