“Chris baba nimekwambia chukua
maamuzi kwanza.”
“Nadia chukua nguo zako na uiache nyuma hii. Huyu
ni mke wangu na kila kitu kwangu” alisema Chris kwa sauti yenye kitetemeshi,
bila shaka moyo ulikuwa unamsuta!!.
Wanawake wanne na mwanaume mmoja wakawa wananipinga
mimi!! Unadhani ningejiteteaje? Nilikuwa pake yangu katika hii dunia!!
Na hapo nikaulaani moyo wangu!! Moyo
uliodanganyika, uliodanganywa na mwanaume. Mwandishi bado nakuambia nyie wote
ni sawa unakataa, unapata chuki unataka kuondoka chumbani bila kuaga unaleta
hasira kwa kuambiwa ukweli.
Unakataa nini sasa unakataa nini nakwambia nyie
wote ni walewale!! Haya ondoka, endelea na hasira hizohizo, endelea ondoka
mlango upo wazi, niache nilie mwenyewe, nenda hata Desmund alienda, hata Chriss
aliniacha, Danny naye aliniacha, Jadida aliniacha, mama alinikataa akanilaani,
baba na ndugu zangu wote walienda na wewe nenda…nenda si nd’o ulichoamua…niache!!.....ne…ee…”
hakuweza kuendelea Nadia. Maneno yake yakanichoma, sikuweza kujizuia kulia,
nikamkimbilia Nadia na nikaweka uandishi pembeni nikalazimika kumuomba msamaha
Nadia. Haikuwa kazi ndogo!!
NADIA alilia sana kwa sauti ya juu huku machozi
yake yakiishia katika bega langu, niliendelea kumkumbatia labda ndo faraja
pekee aliyokuwa anahitaji kwa wakati ule. Sikujua nini nimwambie maana alikuwa
kama ananihukumu mimi pia kwani nilikuwa mwanaume pia. Mara nikajikuta
nauchukia sana uanaume japo sikutamani kuzaliwa mwanamke kisha kuteseka kama
Nadia.
Hatimaye Nadia alinyamaza kulia lakini hakutaka
hicho kilichomkaba kooni kiishie hapo!! Aliketi akanitazama usoni!!Ama!! Alikuwa amevimba macho yake haswa!! Na
yalikuwa mekundu, kama ilikuwa mara ya kwanza kumuona lazima utetereke na uhisi
kuwa huenda ni mgonjwa mahututi!! “Mwandishi, nilisimama wima nikataka kutembea
niondoke zangu bila kumtazama Chriss machoni lakini kizunguzungu kilinishika,
nikaanguka chini kama mzigo, ule mwili uliokuwa umepigwa sana sasa nikawa
nimejitonesha tena!!
Chris alinisogelea lakini nikasikia akipewa onyo
kali sana kutoka kwa yule mama. Ni hapo nilipogundua kuwa Chriss alikuwa
anawekwa kinyumba na yule mama nd’o maana alitakiwa kutii kila alichokuwa
anaambiwa!!
“Mletee chochote kilichokuwa chake atoke humu
ndani.” Sauti ya mwanamke iliamuru. Kimya kikatanda kisha nikaisikia tena ile sauti,
“Hizo nguo amezinunua yeye ama umemnunulia.” Nikawa nimetega masikio nimsikie
Chriss.
“Amezinunua yeye, sikuwahi kumnunulia chochote!!
Naapa.” Alidanganya Chriss bila shaka alifanya vile kwa sababu ya masalia ya
upendo aliokuwanao kwangu. Yule mama akasonya, Chriss akanifikishia lile begi
pale chini kisha akaninong’oneza jambo Fulani.
Nikasimama tena sasa nikajikongoja nikatoka nje.
Nilipogeuka kumtazama Chriss kwa mara ya mwisho,
ukungu wa machozi ulikuwa umenitanda sikuweza kujua kama alikuwa anatabasamu
ama alikuwa ananisikitikia.
Lakini nilichoweza kukiona kwa uhakika, ni saa ya
ukutani.
Ilikuwa saa kumi kasorobo usiku!!
Naenda wapi mimi Nadia!! Nilijiuliza sana na
sikuyapata majibu, nilitarajia walau wale wanawake wenzangu watapatwa na huruma
na kuniita walau nilale hadi asubuhi lakini haikuwa hivyo hakuna aliyenionea
huruma hata kidogo.
Nilikuwa nimetengwa tena na dunia!! Chriss aliyekuwa
kila kitu kwangu alikuwa amenisaliti.
Naam!! Nikayafuta rasmi yale mawazo kuwa huenda
mama yangu alikuwa ameifuta ile laana aliyonipa akiwa Saudi Arabia, ile laana
ilikuwa inaishi bado!!
Nilikuwa nimelaaniwa!!
Kutoka pale Kariakoo ya Musoma hadi barabara ya
lami hapakuwa na umbali sana, nilijikongoja taratibu hadi nikaifikia barabara
huku nikiwa sijui nini cha kufanya. Na magari yalikuwa yameipumzisha lami!!
Kimya kikuu!!
Hakika Chriss alikuwa ameninunulia nguo nyingi, ni
kama kuna kitu fulani alikuwa akiwaza juu yangu, labda kuwa mkewe siku moja ama
kuwa nami milele. Lakini sasa sikuhitaji kujua hayo. Zile nguo zikaniwia nzito
sana, ukiongezea na yale maumivu makali katika mwili wangu lile begi lilikuwa
adhabu!! Nikaamua kulitua chini. Nikajisogeza katika kichaka kidogo nikaliweka
hapo!! Kisha nikaondoka peke yangu hadi barabara ya lami!!
Hapo sasa uoga ukaanza tena!! Uoga mkuu. Nikahofia
watu wabaya wangeweza kunidhuru usiku ule. Ni hapo ndipo nikayakumbuka maneno ambayo Chriss
alininong’oneza wakati akinipatia lile begi. “Kwenye zipu ya kushoto!!”…naam
aliniambia juu ya zipu ya kushoto.
Nikatimua mbio huku nikichechemea kurejea kule
ambapo niliacha lile begi. Dakika kadhaa nilizotoweka pale hazikuleta tofauti.
Nikalikuta lipo salama, upesi nikapekua katika zipu ya kushoto. Pesa!! Nikakutana na burungutu la pesa!! Machozi ambayo sikujua kama ni ya uchungu ama
furaha yakanitoka huku nikijikuta nakosa maamuzi sahihi juu ya hukumu gani
alikuwa anastahili Chriss, je? Nimsamehe ama ni lipi la kufanya!! Nikaamua
kumsahau Chriss huku nafsi ikisema nami kuwa Chriss alikuwa ananipenda lakini
tatizo alikuwa chini ya uongozi wa mwanamke. Chris alikuwa amewekwa kinyumba!!!
Nguvu zikarejea tena, nikalitwaa lile begi, pesa
nikazisunda katika kifua changu. Nikajikongoja hadi katika nyumba ya kulala
wageni.
Nikapata chumba pale!!
Nikapumzika!!!
Ulikuwa usiku wa aina yake ambao hakika
sikuutarajia, kutoka katika penzi mwanana na kuangukia katika ukimbizi tena.”
Nadia akasita kisha akaniambia kwa upole, “Mwandishi haya maisha hayana
ramani….na kama ipo basi Nadia mimi siwezi kuisoma ramani vizuri.” Akasita
kisha akaendelea, “ningeweza vipi kukubali kubaki Musoma wakati nilikuwa
nimetengwa tayari…ningekubali vipi huruma ya wananchi wakati niliamini kuwa
huruma hizo zimeniponza na moyo wangu mwepesi umenigharimu!! Nilikuwa mjinga
sana kubakia Musoma, lakini si mjinga wa mwisho labda hata Desmund naye alikuwa
mjinga vilevile. Cha muhimu ninachoweza kusema kwa asilimia kadhaa kubaki kule
kulinisaidia lakini kosa kubwa nililofanya ni kuhitaji huruma kutoka kwa
wananchi wa ardhi ambayo ilikuwa imenisaliti. Mwisho wa jina la Nadia na
kuzaliwa kwa jina la Mariam kulinisaidia kidogo, lakini afadhali yale magumu
aliyoyapitia Nadia kuliko huu mkasa ambao Mariam alikumbana nao!!!” Nadia
akanitazama akanikonyeza kisha akasema, “Yeah ni hivyo ule ulikuwa mwisho wa u
Nadia nikabadilika kuwa Mariam. Lakini kubadilika kwa jina hakukumaanisha kuwa
ule ulikuwa mwisho wa mateso yangu wala haikumaanisha mimi kuwa Mariam
ilimaanisha mama Nadia ataifuta laana….laana ile ingefutika iwapo tu kama Nadia
ningeuwawa. Naam asingekuwepo wa kunirithi mateso yangu. Lakini sasa ningekufa
vipi iwapo kuna mtu namdai mali zangu, nife vipi wakati Desmund anaishi??”
kauli za Nadia ziliniacha njia panda, nikashangaa sana maana kweli siku ya
kwanza aliniambia anaitwa Mariam tulipokutana katika mazingira tatanishi,
nikatambua kuwa ni mambo ya wasichana tu kupenda kudanganya majina lakini sasa
nilikuwa nimelipata jibu lakini halikuwa jibu sahihi. Kivipi sasa anaitwa
Mariam wakati alikuwa akiitwa Nadia??
“Kwa hiyo wewe ni Maria mama Nadia?” hatimaye
nikajikuta namuuliza swali kwa mara ya kwanza kabisa tangu nianze utafiti wa
kisa hiki cha aina yake.
Badala ya kunijibu aliniangalia kwa makini kama
anayeisoma akili yangu. Kisha akaanza kusimulia kwa sauti ya chini.
“Ilifikia kipindi nikakimbilia vituo vya watoto
yatima wakanambia kuwa hairuhusiwi na hawapokei mtu juu ya miaka kumi na nane
nikakataliwa, nikakimbia huku na kule kama kichaa. Mwisho nikakimbilia katika
shule ya sekondari ya wasichana Songe! Sijui unaijua??.....shule moja hivi
Musoma ni ya wasichana, nikalazimika kuwa napita mchana wakati wa chakula cha
mchana na majira ya jioni kuokota mabaki ya ugali na maharage wanayobakiza,
mwanzoni walinishangaa lakini mwisho wakanizoea nami wakaniunganisha katika
kundi maarufu kwa jina la ‘waloko’. Hayo yakawa maisha yangu!!
Naam! Nilikuwa katika kutimiza lile neno alilosema
Desmund kuwa mimi ni chokoraa. Tena chokoraa mzoefu.
Nilikula mabaki na kulala popote!! Sasa nikakibariki
rasmi kifo changu maana nilijua lazima nitakufa tu!! Nikaamini kuwa laana ni
kitu kimoja kibaya sana, laana ya mzazi haikwepeki. Nilikonda sana na mwili
kuwa kama motto mdogo, sikuwa na nywele kichwani. Hakika nilikuwa
nimekongoroka!!
Nilikuwa nalia moyoni nikiwaona wasichana waliokuwa
wanasoma shule ile wakitoroka na kuchukuliwa na wanaume wenye pesa zao huku
wengine wakichukuliwa na wanafunzi wenzao wa shule jirani ya Musoma ufundi.
Nilitamani kuwahadithia maisha yangu ili wajifunze kitu lakini ningeanzia wapi
mimi!! Nikabaki kuwasikitikia tu bila kuwaambia lolote. Na maisha yakaendelea.
Nilidumu pale kwa miezi kadhaa huku nikiwa
nimeizoea ile hali na hatimaye nikasahau kile kisa matata kilichonifanya mimi
kupoteza ramani na kujikuta nikiangukia katika uchokoraa rasmi!! Nikiwa sina
ndugu wala rafiki!!.......hatimaye ukafika ule muda wa kupata rafiki mpya
aliyesababisha nibadilike kutoka katika u Nadia na kuingia katika u Mariam.”
Akasita akatwaa maji na kunywa kisha akaendelea!!
“Kipindi cha mitihani hakuna asiyekijua, kipindi hicho kila mwanafunzi hutingwa
na mambo yake akijaribu kujikwamua aweze kufaulu.
Kila mtu huwa na mbinu zake
za ufaulu lakini mbinu maarufu ni kuangaliziana ama kuingia na majibu katika
chumba cha mitihani, siku hiyo mchana kama kawaida tulikuwa tunarandaranda huku
na kule katika ile shule, tukingojea muda wa chakula cha mchana ufike. Ndipo
nilipokutana na Jesca, niliwahi kuwa mwanafunzi hivyo nilijua kila kitu, Jesca
hakuwa na nia ya kuja chooni lakini nia yake ilikuwa kufuata majibu aliyokuwa
ameyahifadhi chooni, nilimuona alipoyahifadhi na hata alipoenda kuyachukua
nilimuona pia. Lakini licha ya kumuona yeye pia kuna kitu nilikigundua, kuwa
kuna mwalimu alikuwa ameyaona yale majibu na alikuwa anategea amwone
aliyeyaweka, nilimtambua mwalimu Temba maana alikuwa anaogopwa sana na kuna
wakati alikuwa akitugeuzia kibao hata sisi ambao aliamini tunaokota mabaki ya
chakula kile kwa ajili ya bata nyumbani, hakujua mimi nilikuwa nakula chakula
kile.
Yule binti alivyotoka darasani nami nikasimama
ilimradi tu nipishane naye, nikajifanya namuulizia kitu, akanitazama kwa hasira
kali. Bila shaka hakuvutiwa na ombi langu!! Sikutaka apige hatua mbele zaidi,
“dada mwalimu Temba amekutegea ameyaona majibu yako!! Usiende!” nilimwambia na
kuhakikisha amesikia kisha nikachukua hamsini zangu nay eye nikamwacha bila
kumtazama tena……sikujua nini kiliendelea lakini jioni Jesca alinitafuta!! Huo
ukawa mwanzo wa urafiki wetu, urafiki ulioniingiza katika jina jipya na MATESO
MAPYA!!
MATESO MATAKATIFU!!! MATESO NISIYOTAKA
KUYAKUMBUKA!!.....Usiku mwema Gerlad!!” Nadia alinikatisha ghafla wakati
nilikuwa nimejiweka makini sasa kusikiliza ni kitu gani kilitokea.
Kukatishwa huko kukaniacha katika njia panda.
Nikabaki na maswali ambayo hata ungekuwa wewe lazima ungejiuliza.
MOJA: Nadia alilala gesti siku alipofukuzwa nini
kilijiri sasa?
MBILI: Nadia akabadilika kuwa MARIAM…nini chanzo.
TATU: JESCA anahusika vipi katika mkasa huu?
NNE: Nadia anadai mateso ya MARIAM ni makali kuliko
haya ya NADIA…..inawezekana vipi? Na ilikuwaje?
TANO: Nini hatma ya Desmund maana Nadia hajawahi
kumsamehe!!
Ni maswali hayo yaliyoniumiza kichwa lakini sikuwa
na jinsi nikalazimika kumjibu Nadia, “USIKU MWEMA PIA”…kisha nikaondoka na
kuufunga mlango!!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni