KICHOMI CHA MOYO
Baada ya kutoka katika mihangaiko ya kazi, Ngonyani alirudi nyumbani, na
kumkuta mke wake akiwa anamsubiri, wakati huo yalikuwa ni majira ya saa sita za
usiku, Ngonyani alikuwa amechoka sana, alimtizama mke wake kwa macho ya upole
na kusema "Pole sana mke wangu Sitinde, yaonekana umenisubiri kwa muda
mrefu , naomba unisamehe kwani nimeshindwa kuwahi kama nilivyokueleza kuwa
tutatoka pamoja kusherekea siku yako ya kuzaliwa, nilitingwa sana na kazi,
ndiyo maana nimechelewa, nisamehe kipenzi changu, Mama watoto, nyonga mkalia
Ini wewe ndiyo furaha yangu".
Aliongea Ngonyani huku taratibu akiwa anamsogelea mke wake ambaye
alimtizama huku akionekana kukosa furaha Sitinde alisimama na kumsogelea Ngonyani kisha
alimkumbatia huku akisema "Nakupenda sana mume wangu, pole na kazi, yaani
nilitamani sana leo tungetoka pamoja, lakini hakuna shaka, nilipoona muda
unazidi kwenda nikajua tutashindwa kutoka pamoja hivyo nimeandaa chakula kizuri
kwa ajili yetu".
Ngonyani alitabasamu na kusema "Ndiyo maana nakupenda
mke wangu, nafurahi kuwa na mwanamke mrembo na muelewa, asante sana mpenzi,
ngoja basi niingie ndani nikaoge halafu nije tujumuike pamoja kula chakula
kizuri ulichoandaa, maaana kwa ninavyofahamu ujuzi wako katika mapishi huwa
haukosei, unajua sana kupika mke wangu" Aliongea Ngonyani huku akiwa
anaelekea chumbani kwenda kuoga.
Kwa wakati huo Sitinde aliendelea
kuandaa vizuri mezani na kisha aliketi na kumsubiri mume wake, akiwa anaendelea
kumsubiri ilipita kama nusu saa nzima lakini Ngonyani hakutokea, Sitinde aliamua kumuita huku akiwa amesimama na
kutembea kuelekea chumbani "Darling (mpenzi), mume wangu jamani, mbona
unachelewa hivyo mwenzio njaa inaniuma sana" Aliongea Sitinde huku akiwa anafungua mlango wa Chumbani,
alipoingia tu ndani alimuona mume wake akiwa amelala kitandani fofofo huku
akiwa amevalia bukta, na pembeni ameshikilia taulo.
Alisogea karibu na kuanza
kumgusa taratibu katika paji la uso wake na kusema "Jamani mpenzi,
inamaana umechoka kiasi kwamba hata kula huwezi, daaah nilitamani sana
tungejumuika na kula pamoja ila sasa ndiyo umekwisha pumzika na kesho unawahi
kwenda kazini, yaani mimi mwenyewe siwezi kula chakula peke yangu, jamani mume
wangu amka basi angalau ukale chakula kidogo, au nikakuletee ule hapahapa
chumbani, eeh mpenzi, nisikilize basi mpenzi".
Alikuwa anaongea Sitinde na
machozi yakiwa yana mlengalenga, lakini Ngonyani alikuwa amelala fofofo bila ya
kumjibu chochote, zaidi ya kuguna na kujigeuza kutokana na uchovu na usingizi
mzito aliokuwa nao, wakati huo ilikuwa tayari ni majira ya saa nane kasorobo za
usiku.
Sitinde alinyanyuka pale kitandani na kuelekea mezani ambapo aliketi huku
akiwa anakitizama kile chakula bila ya kukigusa moyoni mwake alikuwa akiwaza
“Yaani leo ni siku yangu muhimu sana, nashindwa kuelewa kwanini Ngonyani
anakuwa hivi kila wakati ninapohitaji tuwe pamoja tufurahi mwenzangu anakuwa ni
mtu wa kujisahau na wala hanifikirii
hata kidogo inaniuma sana, aah ni bora niende zangu nikalale, nimepika chakula
kizuri sana lakini hata sikitamani tena, yaani naumia sana moyoni basi tu sina
namna” Alikuwa akiwaza Sitinde, huku
akisikitika sana moyoni.
Hatimaye aliamua kukiacha chakula pale mezani bila hata ya kuondoa vyombo na
kurudi chumbani kupumzika, akiwa kitandani alishindwa kabisa kupata usingizi
muda wote alikuwa akimtizama Ngonyani ambaye alikuwa amelala fofofo wala
asielewe kama Sitinde alikuwa akimtizama, kwa macho yake malegevu mithili ya
mtu aliyekula kungu, taratibu Sitinde alimsogelea Ngonyani nakumshika katika
paji la uso wake, kisha alimkumbatia na kumbusu, katika paji la uso huku
akisema.
“Nakupenda sana mume wangu, wewe ni barafu ya moyo wangu, natamani
ungekuwa haujachoka unipoze moyo wangu, ila fahamu tu nakupenda ulale unono
mpenzi” Baada ya muda Sitinde alipitiwa na usingizi hadi asubuhi
kulipopambazuka, alishtuka kutoka usingizini na kutizama pembeni ambapo
hakumuona Ngonyani, haraka alinyanyuka kutoka pale kitandani na kuelekea
sebuleni huku akiita “Darling (mpenzi),
uko wapi?” Aliita lakini Ngonyani hakuitika kwani muda huo tayari alikuwa
amekwishaondoka, kwenda kazini.
Sitinde alirudi chumbani huku akiwa
amekosa raha kabisa alisogea kitandani na kuketi ndipo alipokutana na kadi
ikiwa imeambatanishwa na ua la rangi nyekundu ambapo ndani yake kulikuwa na
ujumbe mfupi uliokuwa umeandikwa katika karatasi “Naomba unisamehe mke wangu jana sikukutendea haki, ilikuwa ni siku yako
muhimu sana, ila nilikuwa nimechoka, kutokana na kazi nyingi nilizokuwa nazo,
ila nakuahidi, nitandaa siku nzuri kwaajili yetu mimi na wewe tufurahi pamoja,
nakupenda sana mke wangu ubaki salama tutaonana baadaye”.
Baada ya kumaliza kusoma ule ujumbe Sitinde
alitabasamu na kusema “Nakupenda pia asali wa moyo wangu, ila nakukosa sana,
yaani natamani kuwa karibu na wewe lakini inashindikana kwasababu ya kazi zako
kuwa nyingi, nimekuelewa mpenzi, nakupenda sana naisubiri hiyo siku utakayopata
nafasi tufurahi pamoja.” Sitinde alikuwa akizungumza peke yake kana kwamba kuna
mtu ana zungumza naye.USIKOSE SEHEMU YA PILI.
Maoni 1 :
Mwanzo mzuri tuko pamoja dada
Chapisha Maoni