Jumapili, Novemba 23, 2014

KICHOMI CHA MOYO SEHEMU YA KWANZA

KICHOMI CHA MOYO
Baada ya kutoka katika mihangaiko ya kazi, Ngonyani alirudi nyumbani, na kumkuta mke wake akiwa anamsubiri, wakati huo yalikuwa ni majira ya saa sita za usiku, Ngonyani alikuwa amechoka sana, alimtizama mke wake kwa macho ya upole na kusema "Pole sana mke wangu Sitinde, yaonekana umenisubiri kwa muda mrefu , naomba unisamehe kwani nimeshindwa kuwahi kama nilivyokueleza kuwa tutatoka pamoja kusherekea siku yako ya kuzaliwa, nilitingwa sana na kazi, ndiyo maana nimechelewa, nisamehe kipenzi changu, Mama watoto, nyonga mkalia Ini wewe ndiyo furaha yangu".

 Aliongea Ngonyani huku taratibu akiwa anamsogelea mke wake ambaye alimtizama huku akionekana kukosa furaha Sitinde  alisimama na kumsogelea Ngonyani kisha alimkumbatia huku akisema "Nakupenda sana mume wangu, pole na kazi, yaani nilitamani sana leo tungetoka pamoja, lakini hakuna shaka, nilipoona muda unazidi kwenda nikajua tutashindwa kutoka pamoja hivyo nimeandaa chakula kizuri kwa ajili yetu".


 Ngonyani alitabasamu na kusema "Ndiyo maana nakupenda mke wangu, nafurahi kuwa na mwanamke mrembo na muelewa, asante sana mpenzi, ngoja basi niingie ndani nikaoge halafu nije tujumuike pamoja kula chakula kizuri ulichoandaa, maaana kwa ninavyofahamu ujuzi wako katika mapishi huwa haukosei, unajua sana kupika mke wangu" Aliongea Ngonyani huku akiwa anaelekea chumbani kwenda kuoga.

Kwa wakati huo Sitinde  aliendelea kuandaa vizuri mezani na kisha aliketi na kumsubiri mume wake, akiwa anaendelea kumsubiri ilipita kama nusu saa nzima lakini Ngonyani hakutokea, Sitinde  aliamua kumuita huku akiwa amesimama na kutembea kuelekea chumbani "Darling (mpenzi), mume wangu jamani, mbona unachelewa hivyo mwenzio njaa inaniuma sana" Aliongea Sitinde  huku akiwa anafungua mlango wa Chumbani, alipoingia tu ndani alimuona mume wake akiwa amelala kitandani fofofo huku akiwa amevalia bukta, na pembeni ameshikilia taulo.

 Alisogea karibu na kuanza kumgusa taratibu katika paji  la uso wake na kusema "Jamani mpenzi, inamaana umechoka kiasi kwamba hata kula huwezi, daaah nilitamani sana tungejumuika na kula pamoja ila sasa ndiyo umekwisha pumzika na kesho unawahi kwenda kazini, yaani mimi mwenyewe siwezi kula chakula peke yangu, jamani mume wangu amka basi angalau ukale chakula kidogo, au nikakuletee ule hapahapa chumbani, eeh mpenzi, nisikilize basi mpenzi".

 Alikuwa anaongea Sitinde na machozi yakiwa yana mlengalenga, lakini Ngonyani alikuwa amelala fofofo bila ya kumjibu chochote, zaidi ya kuguna na kujigeuza kutokana na uchovu na usingizi mzito aliokuwa nao, wakati huo ilikuwa tayari ni majira ya saa nane kasorobo za usiku.

Sitinde alinyanyuka pale kitandani na kuelekea mezani ambapo aliketi huku akiwa anakitizama kile chakula bila ya kukigusa moyoni mwake alikuwa akiwaza “Yaani leo ni siku yangu muhimu sana, nashindwa kuelewa kwanini Ngonyani anakuwa hivi kila wakati ninapohitaji tuwe pamoja tufurahi mwenzangu anakuwa ni mtu wa kujisahau  na wala hanifikirii hata kidogo inaniuma sana, aah ni bora niende zangu nikalale, nimepika chakula kizuri sana lakini hata sikitamani tena, yaani naumia sana moyoni basi tu sina namna” Alikuwa akiwaza Sitinde, huku  akisikitika sana moyoni.

Hatimaye aliamua kukiacha chakula pale mezani bila hata ya kuondoa vyombo na kurudi chumbani kupumzika, akiwa kitandani alishindwa kabisa kupata usingizi muda wote alikuwa akimtizama Ngonyani ambaye alikuwa amelala fofofo wala asielewe kama Sitinde alikuwa akimtizama, kwa macho yake malegevu mithili ya mtu aliyekula kungu, taratibu Sitinde alimsogelea Ngonyani nakumshika katika paji la uso wake, kisha alimkumbatia na kumbusu, katika paji la uso huku akisema.

“Nakupenda sana mume wangu, wewe ni barafu ya moyo wangu, natamani ungekuwa haujachoka unipoze moyo wangu, ila fahamu tu nakupenda ulale unono mpenzi” Baada ya muda Sitinde alipitiwa na usingizi hadi asubuhi kulipopambazuka, alishtuka kutoka usingizini na kutizama pembeni ambapo hakumuona Ngonyani, haraka alinyanyuka kutoka pale kitandani na kuelekea sebuleni huku akiita “Darling (mpenzi), uko wapi?” Aliita lakini Ngonyani hakuitika kwani muda huo tayari alikuwa amekwishaondoka, kwenda kazini.

 Sitinde alirudi chumbani huku akiwa amekosa raha kabisa alisogea kitandani na kuketi ndipo alipokutana na kadi ikiwa imeambatanishwa na ua la rangi nyekundu ambapo ndani yake kulikuwa na ujumbe mfupi uliokuwa umeandikwa katika karatasi “Naomba unisamehe mke wangu jana sikukutendea haki, ilikuwa ni siku yako muhimu sana, ila nilikuwa nimechoka, kutokana na kazi nyingi nilizokuwa nazo, ila nakuahidi, nitandaa siku nzuri kwaajili yetu mimi na wewe tufurahi pamoja, nakupenda sana mke wangu ubaki salama tutaonana baadaye”. 

 Baada ya kumaliza kusoma ule ujumbe Sitinde alitabasamu na kusema “Nakupenda pia asali wa moyo wangu, ila nakukosa sana, yaani natamani kuwa karibu na wewe lakini inashindikana kwasababu ya kazi zako kuwa nyingi, nimekuelewa mpenzi, nakupenda sana naisubiri hiyo siku utakayopata nafasi tufurahi pamoja.” Sitinde alikuwa akizungumza peke yake kana kwamba kuna mtu ana zungumza naye.USIKOSE SEHEMU YA PILI.

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Mwanzo mzuri tuko pamoja dada

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom