ILIPOISHIA
Baada ya kama
robo saa akatoka mchungaji kijana, Stephano. Nikamkimbilia na kumwangukia
kifuani mimi na Jonas, akaizungusha mikono yake nikalipata lile joto la upendo.
Akanikaribisha ndani sebuleni, nikaingia huku nikiwa nalia kilio cha kwikwi, akaniuliza kulikoni. Huku akiwa ananitazama katika hali ya kutia matumaini na upendo mkuu.USIKOSE SEHEMU YA 22
INAPOENDELEA
Ningeweza kusita kumweleza mtu yeyote yule juu ya maisha yangu lakini si mtu ambaye anaaminiwa na maelfu kama mtu wa Mungu, na alishiriki katika kuijenga imani yangu. Na alinifanya kila jumapili niione kuwa ya thamani kwa sababu tu alikuwa akiniambia maneno mazuri, Stephano alichangia kwa kiasi kikubwa kurejesha ushirikiano kati yangu na Mungu ambaye niliwahi kusema kuwa amenisahau ama anashiriki katika kunisulubu.
Nikamweleza
historia yangu ngumu kwa ufupi sana, nikamweleza jinsi nilivyofika nyumbani kwa
mzee Aswile na kisha nikagusia kiundani juu ya taarifa ya tetesi aliyonipa
shamba boi juu ya hisia za mama Aswile kwangu mimi kuwa nina mahusiano na
mumewe. Mchungaji akaduwaa, lakini nikafikia hadi hatua ya kumweleza kuwa
nahisi mama Aswile anahusika katika kumuua mumewe.
Hapa akaungana nami kwa
hisia hiyo, akatazama juu akawa kama anayenena kwa lugha nisizozijua. Bila
shaka alikuwa kiroho zaidi. Pia nikamgusia juu ya Jonas ambaye mama Aswile
alidhani ni mtoto wa mume wake, hapa nikamtaja Jesca kwa mara ya kwanza baada
ya muda mrefu na nikamweleza mchungaji nkuwa nina tatizo la uzazi na sijawahi
kuwa na mtoto. Akanipa pole!!
“Mchungaji!
Mimi nimeondoka katika familia ile kwa sababu nachukiwa, na mbaya zaidi
nimefanya fujo pale nyumbani. Nipo hapa kwa kitu kimoja tu…uwezo wangu kiakili
umefika mwisho, sijui nini cha kufanya na nimechanganyikiwa kabisa. Naomba
unisaidie kutatua jambo hili, ni wewe pekee uliyebaki katika maisha yangu, ni
wewe waweza kusema neno nami nikajiona ni mwanadamu tena. Tafadhali baba
mchungaji!!” nilimsihi kwa sauti ya chini. Na hapo nikayangoja majibu yake.
“Mariam!!
Bwana ni mwema na humulika taa kwa watu wake na kamwe hawatajikwaa, malaika
wamewazunguka na kuwalinda kwa mabawa yao. Mungu yu pamoja nawe, haujayapita
hayo yote kwa uweza wako. Sijisikii vyema sana usiku huu baada ya taarifa hii,
sasa nakuomba ulale, mimi ninaingia katika maombi, na nitakesha kukuombea usiku
mzima na asubuhi bwana ninayemuamini atatoa majibu.” Aliniambia huku kama
kawaida akirusha mikono huku na kule kisha kunena kwa lugha za kigeni.
Mwisho
akanipeleka katika chumba maalumu kwa ajili ya wageni.
“Watoto na
mama yao wamesafiri nimekuwa mpweke sana, angekuwepo Suzan ungelala naye humo.
Lakini hayupo sasa.” Aliniambia kwa kusihi, sikujali., nikaingia chumbani,
nilitamani kuoga lakini ile baridi ikanisaliti nikaghairisha na kujitupa
kitandani.
Blangeti zito
likamfunika Jonas, sasa alitabasamu kidogo, kisha akapotea usingizini. Nami
nikawa katika kusinzia. Lakini si hoi kama Jonas, baada ya muda kidogo nikiwa
sijasinzia bado nikasikia sauti ikiniita, alikuwa ni mchungaji. Nikajifanya
sisikii vyema, akaita tena bado sikuitika. Sijui kwanini sikutaka kuitika,
labda ni msongamano wa mawazo kuwa mchungaji ameingiwa tamaa za kimwili ama
vipi. Hatimaye akaondoka. Nami nikasinzia kweli.
Nilikuja
kushtuka usingizini Jonas alikuwa analia, kilio chake kilitaka kufanana na kile
cha usiku ule kisha asubuhi mzee Aswile akafariki. Nilitaka kupuuzia baada ya
Jonas kusinzia tena kwani kilio kile hakikudumu. Lakini nikakumbuka kuwa mimi
ni Nadia niliyelaaniwa, Nadia mwenye mwonekano wa mwanadamu lakini nikiishi
kama kivuli, Nadia mwenye hofu wakati wote. Nadia asiyeaminika, Nadia
asiyetakiwa kumwamini mtu.
Nikasimama na
kuufungua mlango kisha nikajongea katika sebule, nikijifanya naenda kutafuta
maji ya kunywa katika friji. Nikaisikia sauti ikiunguruma kwa chini chini, bila
shaka katika simu. Nikaganda katika friji na sasa nikaweza kusikia maneno
baadhi, lakini muongeaji akaendelea kujisahau na mwisho akawa anazungumza kwa
sauti ya juu.
“Ameshasinzia
nimeenda chumbani alipo nimemuita haitiki, amechoka kwakweli. Sasa sika wewe
kitu cha msingi kama unafahamiana na bodaboda yeyote yule akupeleke kituoni
asubuhi, si umeshachukua RB….wewe wape hela ya mafuta mje na difenda yao
mtamkuta hapa…..
….wewe
usijali kuhusu hilo, nitakifunga kile chumba mtamkuta kama alivyo. Tena
jitahidi sana maana mambo aliyoniambia ni balaa, wewe naye ujifunze kuwa na
siri mbona anajua mambo mengi hivyo, je angeenda kwa mtumishi mwingine unadhani
tungeonekanaje mpenzi wangu.
……sio kama
nakulaumu mamangu, mi nakwambia ukweli mpenzi. Haya hayo yaishe maana hukawii
kukasirika. Wewe asubuhi sana uje umchukue halafu mimi nitamalizana na mkuu wa
upelelezi afanye tunayotaka. Mbaya sana huyu binti, na niliwahi kukwambia
kabisa haya mambo ya kufuga viumbe usiowafahamu ipo siku utafuga
majini………(kimya akisikiliza upande wa pili)
…..kuhusu
mtoto usijali hata cha msingi huyu paka kwanza. Alfajiri nakifunga chumba
mtawakuta wote. Alijifanya mjuaji sana kukupigeni na kukimbia hii Mbeya yetu
asingeweza, wewe nilikwambia ukajifanya kukata tamaa…..wewe saa kumi na mbili
fika hapa…”
Nilibaki kama
sanamu nimeganda pale katika friji. Alikuwa ni mchungaji Stephano, mtu pekee niliyekuwa
namwamini kuwa atanisaidia katika tatizo hili linalonikabili, sasa anazungumza
na mama Aswile, yaani mama Aswile na mchungaji kumbe ni wapenzi. Mungu wangu!!
Nilipagawa, mbaya zaidi alikuwa amesisitiza kuwa asubuhi polisi wanakuja
kunishika, na kuhusu Jonas watajua cha kumfanya. Nilitetemeka sana, nikaondoka
kwa kunyata nikaelekea chumbani, Jonas alikuwa anapepesa macho huku na kule, na
yeye alikuwa ametoka usingizini tena. Ukutani kulikuwa na saa, ilikuwa ni saa
nane na dakika hamsini hivi. Sikutakiwa kulala tena, lakini ningetoka vipi
katika nyumba ile.
Nadia mimi
nilikuwa nimetupiwa pepo la kusalitiwa na kukataliwa, hata kiongozi wa kiroho
alikuwa amenisaliti!!!! Hakika niliumia sana, na hapa nikajiona nisiyekuwa na
ujanja tena.
Majira ya saa
kumi na moja chumba kile kilifungwa kwa
nje.
Saa kumi na
mbili kama nilivyoyasikia mazungumzo kwenye simu ndo muda ambao askari
walitakiwa kufika pale kunikamata. Jonas abaki na kufanywa wanavyotaka.
Milango ya
jela nikaiona ikifunguka na Nadia mimi nikitakiwa kuingia. Nikaona akina
Desmund wakitabasamu huku mzee Matata na wenzake wakinicheka, Bryan alikuwa
akinizomea na familia yangu nzima ikipiga makofi, hata mama yangu akiwa mmoja
wao katika orodha.
Nitafanya
nini nikwepe mtego huu, kumwamini mtumishi wa kiroho kumeniponza. Muda nao
ukazidi kusogea dakika kwa dakika………..mwandishi umewahi kuusikia moyo wako
ukiwa wa moto huku ukidunda pigo moja baada ya jingine kwa kasi isiyohesabika.
Basi nilikuwa namna ile. Sikuona dalili yoyote ya kujiokoa kutoka pale. Mlango
mkuu wa kutokea nje ulikuwa umefungwa na mbaya zaidi mlinzi atakuwa amezuiwa
asiniruhusu kutoka nje……..nilimwomba Mungu ile laana iishie kwangu lakini sasa
alikuwa kwa mara nyingine amenihukumu na kunipa kisogo, Jonas alikuwa anaishi
katika laana yangu, Jonas alsiyejua hili wala lile anahangaika
nami..Jonas…Jonaa….asiyeweza hata kusema neno lolote la ubaya kwa mtu
anahukumiwa na wanaojitambua, walimuita mwanaharamu sasa watamuua.” akasita
kuzungumza, kilio cha kwikwi kilikuwa kimelikamata koo lake. Akalia kwa
kujibana bana lakini hakuweza. Alikuwa anatetemeka sana.
Nikamchukua
shingo yake na kumlaza begani mwangu, akaendelea kulia.
“USILIE
NADIA….machozi yako bado yana thamani sana usiyaruhusu yamwagike zaidi ya hapa
Nadia, nilikuahidi tangu siku ya kwanza kuwa sitakusaliti kamwe na
nitakupigania upate unachokitafuta. Niamini, na nilikwambia tukifika Dar utajua
nini namaanisha….” Nilimsisitiza lakini bado alilia kwa uchungu sana.
Nikamlaza
kitandanbi kwangu, nikamfunika na shuka langu, mimi nikakaa katika kochi, Nadia
akiwa analia pekee katika shuka.
Katia makochi
mimi nikazidi kuchanganyikiwa.
Nadia
alikamatwa ama alifanikiwa kuwashawishi wakamwachia?
Kama
alikamatwa ilikuwaje akaachiwa huru wakati alikuwa na siri nzito kifuani mwake?
Na Jonas
mwisho wake ulikuwa upi?
Vipi kuhusu
Desmund?
Vipi mkewe
Desmund?? Vipi mama mzazi wa Desmund na yule mzee Matata naye vipi?
Jesca
hajulikanai alipo, na yeye hatima yake vipi?
Hakika
maswali yalikuwa mengi kuliko majibu…nikatamani Nadia ajue jinsi gani maswali
yale yananiumiza kichwa anyanyuke na kuendelea kunijibu. Lakini Nadia hakuwa
anajua hilo….akasinzia pale kitandani.
*****
Nilisinzia
katika yale makochi pale bila kujitambua kama nilisinzia, nilikuja kushtuka
baada ya kusikia napapaswa. Nilipofumbua macho alikuwa ni Nadia, alikuwa
anatabasamu pana usoni.
“Utaibiwa
wewe!!” aliniambia huku akirejea kukaa kitandani.
“Mh!! Hivi
saa ngapi sasa hivi?” nilimuuliza, akanieleza kuwa tayari ilikuwa saa kumi na
mbili asubuhi. Nililala kwenye kochi na yeye alilala kitandani.
“Duh mgongo
unauma kweli…umenilazaa kwenye kochi we mtoto.” Nilimtania Nadia wakati huo
nikijinyoosha.
Nadia
alinitazama kisha akajiweka katika namna ya kuchukua egemeo ukutani. Na hapo
akaanza kuzungumza.
“Walaah!!
Ungekuwa wewe usingeweza kudumu hata saa zima kumbe, yaani hadi Jonas anakuzidi
kumbe, yule mtoto alikuwa jasiri sana, niliamini kabisa kuwa lazima ataniumbua
tu usiku ule, lakini ya Mungu mengi kwakweli Jonas alivumilia. Nilimbeba akiwa
katika usingizi nikamuhamishia nyuma ya kochi kubwa katika sebule ya kifahari
ya mchungaji Stephano, nikamtandikia kitambaa chepesi tu nikamlaza katika
vigaye vile, bila shaka unajua jinsi gani vigaye vinakuwa na baridi kali, pale
kitandani nikaacha mashuka yakiwa katika namna ya kufunika viumbe hai. Ni hilo
lilikuwa jaribio langu la mwisho kabla mchungaji hajachukua uamuzi wa kukifunga
kile chumba kama alivyokuwa amesema katika simu.
Hakika baada
ya kutoka mle chumbani na kujificha nyuma ya kochi lile mimi na Jonas wangu
nilimsikia mchungaji akinyata hadi akaufikia mlango ule wa kitasa, akaingiza funguo kwa tahadhari
bila hata kujihakikishia kama bado nilikuwa ndani ya chumba kile. Akaufunga
mlango!! Baada ya hapo akampigia simu mama Aswile na kumweleza kuwa amekifunga
chumba tayari.
Niliendelea kubaki
nyuma ya kochi kubwa pale sebuleni huku nikiomba dua zote Jonas asije kushtuka
na kuanza kulia. Jambo ambalo kwangu
mimi lilikuwa hatari sana, na jinsi
mchungaji yule alivyokuwa anazungumza kwa hasira na chuki basi angeweza kunitoa
roho kama angegundua nimemchezea shere katika jambo hilo.
Niliendelea
kuwa pale, Jonas alikuwa amelala lakini mimi nilikuwa nimejikunja katika namna
ambayo mwanadamu wa kawaida katika mazingira ya kawaida asingeweza kudumu walau
kwa nusu saa, lakini Nadia mimi kwa wakati ule sikuwa mwanadamu wa kawaida na
kubwa zaidi sikuwa katika mazingira ya kawaida. Nilikuwa katika hatari na nilitakiwa
kuchukua maamuzi ya haraka, maamuzi ambayo yangeniamulia kuwa aidha naendelea
katika harakati zangu za kulipiza kisasi na kukomboa mali zangu kutoka kwa
Desmund huku nikimfanya aione dunia chungu, ama kuzembea kidogo na kujikuta
nikiishia jela ambapo nitakuwa katika machungu, labda kupita haya ya awali.
Hali hiyo
ilinipa ujasiri na kuendelea kujikunja pale, sio siri mgongo ulikuwa unaniuma
sana, ulichemka na kuwa wa moto, lakini kipi kingekuwa bora kwangu, aidha
kuuumia kwa muda ama kuja kuteseka maisha yangu yote. Hali ilikuwa tete.
Majira ya saa
kumi na mbili kwa mujibu wa saa iliyokuwa ukutani nilisikia kile ambacho
Stephano alikuwa ameahidi, niliisikia gari ikisimama nje na geti likafunguliwa. Baada ya hapo chumba
cha Stephano kilifunguliwa alipofika sebuleni, nikasikia vishindo vingine.
“Mh…..nikumbatie
kwanza la sivyo simtoi..” nilimsikia mchungaji akisema, kimya kikatanda, na
mara wawili hao ambao niliisikia miguno ya kimahaba ikiwatoka wakaangukia
katika lile kochi ambalo mimi nilikuwa nimejificha nyuma yake, kishindo cha
kuliangukia lile kochi mara Jonas naye akafumbua macho, Mungu wangu!! Nikajua kifuatacho ni kutokwa na kilio, nikaundaa
mkono wangu iwapo Jonas atathubutu kutoa kilio niweze kumziba mdomo, hekaheka
ziliendelea katika lile kochi bila shaka walikuwa wakibusiana, na walikuwa
wamenogewa hadi pale honi ilipopigwa.
“Ndo hao
uliokuja nao.” Stephano aliuliza.
“Nimekuja naye
mmoja tu mbona, tumechukua teksi tu walishauri hivyo.” Alijibu mama Aswile sasa
niliweza kuisikia sauti yake vizuri.
“Mpenzi yaani
nd’o alikukwangua hivi?” mchungaji aliuliza.
“Mwendawazimu
sana yule mtoto, namfunga maisha haki ya Mungu!!” aliapa kwa hasira, nami
nikazidi kutetemeka lakini sikuhamisha macho kutoka machoni mwa Jonas. USIKOSE SEHEMU YA 23
Maoni 1 :
Jamani Nadia...
Chapisha Maoni