Mbona
unaonekuna kuwa na mawazo mengi sana vipi, una matatizo gani Jojina? Aliuliza
na kuhoji, Monika huku
akimtazama Jojina ambaye alikuwa amejiinamia bila ya kusema chochote,
baada ya muda kidogo Jojina alinyanyua uso wake na kumtizama Monika kisha akasema “Unajua
katika maisha yangu sikuwahi kufikiria hata sikumoja , yaani hata maramoja
kama Mbuso angeweza kunifanyia hivi,
siamini na pia naumia sana, halafu kwanini amenitendea yote haya mimi
nilimpenda kwa moyo wangu wote nilimthamini sana inamaana kweli yote aliona kuwa hayatoshi
akaamua kuniumiza kiasi hiki, inaniuma sana, naumia Monika moyo wangu unaumia
sana”.
Aliongea Jojina huku machozi yakiwa yanambubujika kwenye paji
la uso wake mithili mtu aliyemwagiwa maji kichwani, na kwa wakati wote huo
Monika alikuwa akimsikiliza kwa umakini sana kisha alisogea na kuketi karibu na
Jojina aliyekuwa ameketi kwenye mkeka uliokuwa kibarazani nyumbani kwake, alisogea na kuketi kisha
akamshika mkono na kuuliza “Jojina, mbona sikuelewi kwani shemeji Mbuso
amefanya nini? Halafu ukiwa unalia hivi
unanichanganya kuna tatizo gani? .
Aliuliza Monika huku
Jojina akiwa anajifuta machozi
alinyamaza kimya na moyoni mwake akiwa anawaza “Ama kweli dunia siyo
mbaya walimwengu ndiyo wabaya, mimi nilikutana na Mbuso miaka mitatu iliyopita,
na baada ya mwaka mmoja tulifunga pingu za maisha, na katika safari yetu ya
maisha ya ndoa tulijitahidi sana ili tuweze kufanikiwa katika mambo mbalimbali
kweye maisha, na kweli Mungu alitujalia tukafanikiwa kujenga nyumba na kupata
mtoto mmoja , mwanangu Joyce ana mwaka mmoja na nusu bado ni mdogo sana, na hata siku moja sikuwahi
kufikiria kama mume wangu angekuja kuniumiza kiasi hiki tena yaani sijui kwakweli kama kidonda hiki kitapona” Alikuwa akiwaza
moyoni mwake Jojina bila yakuzungumza
chochote na wakati huo Monika bado
alikuwa akimtizama kwa uso uliojaa
maswali mengi ambapo alikuwa akisubiri Jojina amweleze ana matatizo gani.
Moja kwa moja Jojina
alishusha pumzi kisha akamtizama Monika na kusema “Usijali rafiki yangu, mimi nitakuwa sawa ,
wewe nenda, naomba uniache kwasasa kwani siwezi kukueleza chochote”
Aliongea kwa sauti ya unyonge huku
akimtizama Monika ambaye bado alikuwa
anataka kujua nini kimemsibu rafiki yake baada ya kumbembeleza sana ndipo
Jojina alipoamua kusema “Unajua Monika wewe ni rafiki yangu ambaye nakuona
zaidi ya rafiki kwani wewe ni kama ndugu
yangu kutokana na urafiki tulionao, mimi nina matatizo katika ndoa yangu mume
wangu amebadilika sana imefikia kipindi ananiambia anataka tutengane kwani
amenichoka, na pia anasema moyo wake unamuhijati mwanamke mwingine eti leo hii
mimi Mbuso ananiambia sina vigezo ambavyo alikuwa anavitaka kwa mwanamke, hivyo
anataka tutengane, yaani mwanzoni nilifikiri ni utani, lakini kumbe ni kweli
sasa ameondoka na kuniacha mimi na mwanangu nilijitahidi sana kumbembeleza
lakini alinijibu hawezi kuishi na mwanamke ambaye hana mapenzi naye, na tena
kama haitoshi anasema akiniona anasikia kichefuchefu, kweli leo hii Mbuso ni wa
kuniona mimi kama takataka, nilimpenda sana siamini mimi kama yote haya
yametokea nipo kama nimechanganyikiwa inauma jamani yaani naumia Monika”
Alikuwa akizungumza Jojina huku machozi
yakiwa yanamlengalenga, Monika alinyamaza kimya kidogo kisha akasema “Pole sana
rafiki yangu , unajua mapenzi yanachangamoto nyingi sana, lakini mimi
nikushauri kitu kimoja usiwaze sana
kwani utajiumiza , mshukuru Mungu huyo Mbuso ameondoka angalau amekuachia
nyumba yako, na wewe unafanya kazi hivyo utaweza kujikimu kimaisha yaani
familia yako haitatetereka na kingine kwanini umlilie mtu ambaye hana mapenzi na
wewe, Jojina rafiki yangu usijiumize
kichwa wewe fikiria maisha mapya na
mtoto wako” Aliongea Monika huku akimtizama Jojina kwa kumkazia macho na wakati wote huo Jojina alikuwa
akimsikiliza kwa umakini kisha akasema “Unajua
ni vigumu sana kuamini yote haya yametokea na pia nampenda sana mume wangu
hivyo ukiniambia niwaze maisha yangu mapya ni kitu kigumu sana kwangu hakuna
mtu ambaye anapenda familia yake
itengane, yaani naumia sana”.
Aliendelea kuzungumza Jojina kwa uchungu huku akimtizama Monika ambaye aliguna kidogo kisha
akasema “Unanishangaza sana rafiki yangu kumbuka maji ya kisha mwagika
hayazoleki, na pia mpende akupendaye asiyekupenda achana naye, sasa wewe
unataka kulazimisha mambo yasiyowezekana , usiwe mjinga kiasi hicho rafiki
yangu, Mbuso ameshakuacha tena amekutamkia wazi kuwa hakupendi sasa wewe
unacholazimisha ni kitu gani? Achana naye endelea na maisha yako
huo ndiyo ushauri wangu wa mwisho”
Aliongea Monika kwa msisitizo. Waliendelea
na mazungumzo lakini baadaye Monika aliamua kuaga na kuondoka huku
akimuacha Jojina akiwa mwingi wa mawazo “Huyu Monika, anafikiri haya mambo ni
madogo sana, yalaiti ingelikuwa ni yeye sizani kama angeweza kuvumila, unajua
maumivu ya kitu chochote anayajua muhusika yaliyomkuta lakini kwa Yule ambaye
hayajamtokea hawezi kuona maumivu, mimi hili jambo limeniumiza sana na siwezi
kujidanganya kuwa sijaumia Mungu naomba unisimamie”
Aliwaza Jojina na
baadaye aliingia ndani kwenda kupumzika, ilipita kama wiki moja mume wake
hakurudi kabisa nyumbani na hata alipomtafuta kwenye simu haikupatikana hewani,
kilasiku alikuwa ni mtu mwenye mawazo mengi sana baadaye alifikiria ni namna
gani anaweza kufanya ili aweze kuondokana na mawazo aliyonayo “Mimi sijui
nifanyeje , ama kweli Mbuso hanipendi tena na sasa nahisi hata namba yake ya
simu amebadilisha, ni wazi kuwa hataki kuniona tena na mimi bado naendelea
kumuwaza sana, ila nikiendelea hivi nitaumia zaidi ni bora nijaribu kumsahau
kabisa kama Monika alivyonishauri, na
sasa nimfikie mtoto wangu pekee”.
Alikuwa akiwaza Jojina na baadaye aliamua
kwenda nyumbani kwa Monika ili kumjulia hali na kumueleza kile alichoamua
kukifanya, alipofika nyumbani kwa Monika alimkuta dada mwingine mgeni ambaye
alijitambulisha kwa jina la Salima, walisalimiana na kisha alimuomba akamwite
Monika, ambapo Yule dada alimtizama na
kusema “Samahani dada mimi ni mpangaji
katika nyumba hii kwasasa Monika amehama
hapa kama wiki moja imepita ila naweza kukuelekeza anapoishi”.
Nilishangaa sana
kusikia kuwa Monika amehama tena bila ya kunipa taarifa ila Yule dada
alinielekeza na moja kwa moja nilienda nyumbani kwa Monika nilipofika tu Monika
alinikaribisha ndani vizuri, ilikuwa ni nyumba kubwa nzuri na ya kifahari tulisalimiana kisha nikamuuliza “Mwenzangu
mbona umehama bila ya kunipa taarifa,
mimi nimetoka kwenye nyumba ile ya zamani nikijua bado upo pale” Monika alimtizama kisha akasema “Hivi
Jojina kwani ni lazima mtu ukihama utoe taarifa, siyo kila jambo ni la kusema
mambo mengine tunafanya kimya kimya”
Aliongea huku akimtizama Jojina ambaye
alikuwa akipepesa macho huku na kule ghafla aliona picha ya Mbuso akiwa na
Monika imebandikwa ukutani, alishtuka na kusema “Hivi ni macho yangu au naona
vibaya, huyu si Mbuso, eeh wewe Monika, mbona sielewi halafu….” Kabla
hajamaliza kuongea Mbuso alikuwa ametoka chumbani akamuona na kusema “Wewe
mwanamke kinachokushangaza hapo ni nini, hivi mbona unapenda kunifuatafuata
nilishakuambia sikutaki sasa naona umeamua kuja kunivuruga katika maisha yangu
mapya”.
Aliongea Mbuso huku Monika akiwa ameketi na kutabasamu, na kwa wakati
huo Jojina alikuwa amebaki ameduwaa huku akisema “Ama kweli kikulacho ki nguoni
mwako, na rafiki yako ndiyo adui yako, kweli wewe Monika ndiyo chanzo cha kila kitu wewe umeamua kuingilia ndoa
yangu, siamini mimi jamani, rafiki yangu niliyekuwa namuona kama ndugu kumbe
unanichekea usoni, moyoni ulikuwa umepanga kuniangamiza, leo hii umeamua kuishi
na mume wangu tena unafurahi kuwa nimeachika, siamini ninachokiona wewe unaroho
mbaya tena unaweza kumuuwa mtu, yaani sijui, kweli ,,ah, aah”
Aliongea Jojina
kwa uchungu sana lakini Monika hakujali kitu alibaki akitabasamu kwa dharau na
kusema “Sikiliza nikuambie Jojina, ndiyo
maana nilikuambia mpende akupendaye asiyekupenda achana naye, Mbuso na mimi
tunapendana hivyo wewe tafuta atakayekupenda mapenzi hayalazimishwi” Aliongea Monika bila hata ya
huruma huku Mbuso akimfukuza Jojina “Naomba uondoke na kamwe usirudi hapa, nimesema
sikutaki, kama nilikupenda ilikuwa zamani, tena nahisi ilikuwa bahati mbaya
mimi siwezi kuwa na mwanamke kama wewe” Aliongea kwa msisitizo na kuacha Jojina
akitoka nje huku akiwa ameishiwa nguvu na machozi yakimbubujika “Asanteni sana
kwa yote mliyonitendea leo kwangu kesho
kwako Mungu yupo atanisimamia, asanteni sana ama kweli ubinadamu kazi sikuwahi
kufikiria kama ningekuja kuumia kiasi hiki”.
Aliondoka Jojina na kurudi nyumbani
alilia sana, kila kukicha alikuwa mwenye mawazo mengi baadhi ya watu
walimcheka na wengine walimpa matumaini ya kuendelea na maisha mapya, ambapo
baadaye aliamua kusahau yote yaliyotokea na kufanya kazi kwa bidii huku akimlea
mtoto wake peke yake maumivu ya mapenzi yalimfanya aogope kupenda tena siku
zote aliishi kwa kumuomba sana Mungu hata ikitokea akapenda tena basi awe ni
mwanamume sahihi katika maisha yake.WADAU MAONI YENU NDIYO YATAKAYONIFANYA NIENDELEE KUWALETEA SIMULIZI MBALIMBALI
Maoni 1 :
Hii hadithi ina mafundisho na mtiririko mzuri. Kwa kweli nitapenda kuona kitakachoendelea.
Chapisha Maoni