Jumatano, Julai 01, 2015

HALI SI SHWARI "Jamii ichukue hatua kudhibiti magonjwa ya moyo, saratani."

NI MUHIMU KUWA MAKINI NA UTARATIBU WA VYAKULA TUNAVYOKULA

Kuna taarifa za kustusha kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo ya moyo, saratani na kisukari. Inaelezwa kuwa maradhi haya yanazidi kuongezeka kwa kasi na ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo nchini na kwingineko duniani.
 
Taarifa mojawapo iliyoripotiwa na gazeti la Nipashe jana ilieleza kuwa ugonjwa wa kisukukari peke yake umeathiri maisha ya watu milioni 371 duniani kote, huku asilimia 80 ya waathirika hao wakiishi katika nchi zenye uchumi wa kati na maskini kama Tanzania.
 
Aidha, utafiti uliowahi kufanywa na Taasisi ya Kisukari nchini mwaka 2012 ulionyesha kuwa asilimia tisa ya Watanzania waligundulika kuwa na kisukari na kwamba, mtu mzima mmoja kati ya watatu anakabiliwa na shinikizo la juu la damu. 
 
Hakika, hizi siyo taarifa njema. Ni janga jingine kwa taifa, sawa na ilivyo kwa maradhi ya kuambukiza kama ukimwi na kifua kikuu. Sisi tunaona kuwa sasa kuna kila sababu ya kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na maradhi haya yasiyoambukiza.
 
Hivi sasa, jitihada nyingi huelekezwa katika kuyakabili maradhi yanayoambukiza, baadhi yakiwa ni ukimwi, kifua kikuu na malaria. Maradhi haya hufahamika zaidi miongoni mwa wananchi na tena, ndiyo ambayo kwa kiasi kikubwa hupigwa vita kupitia kampeni mbalimbali za kitaifa na kimataifa. Maradhi yasiyoambukiza huonekana kana kwamba siyo tishio. 

Yanachukuliwa kuwa ni ya kawaida, licha ya ukweli kuwa ndiyo yanayoua watu wengi zaidi duniani. Siyo watu wengi wanaofahamu kiundani kuhusu chanzo cha maradhi yasiyoambukiza, dalili, tiba zake na pia juu ya namna ya kujikinga. 
 
Hata hivyo, maradhi haya yasiyoambukiza yana athari kubwa kwa jamii. Hugharimu maisha ya maelfu ya watu. Huathiri pia uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa. Kwa sababu hiyo, sisi tunaona kwamba sasa kuna ulazima wa kila mmoja kutambua uwapo wa magonjwa haya na tishio lililopo kwa maisha yao na uchumi wao.
 
Mathalan, takwimu zinaonyesha kuwa mbali na kusababisha vifo, magonjwa yasiyoambukiza pia hugharimu kiasi kikubwa cha rasilimali fedha kwa taifa. Mwaka 2010 pekee, Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa jumla ya gharama zinazohusiana na maradhi ya kisukari duniani kote zilifikia dola za Marekani bilioni 378 na kwamba, kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia dola bilioni 490 ifikapo mwaka 2030. Hali hii inatishia ustawi wa uchumi wa nchi nyingi maskini, ikiwamo Tanzania ambayo hukabiliwa na changamoto kubwa ya fedha za kukabiliana na maradhi kama ya kisukari, moyo na saratani.
 
Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa sasa kuna haja ya kuwapo kwa jitihada za ziada za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza. Kwamba, badala ya kujielekeza zaidi katika magonjwa ya kuambukiza peke yake kama ukimwi, malaria na kifua kikuu, serikali ishirikiane na wadau wote wa afya kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa wa kutosha na mwishowe kushiriki kivitendo katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
 
Tunatambua kuwa hivi sasa, zipo jitihada kadhaa zinazoendelea kufanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kukabiliana na maradhi haya. Na baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kampeni za uelimishaji umma kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, mojawapo ikiwa ni kushirikiana na Taasisi ya Kisukari Tanzania kuandaa kitabu kinachoeleza kwa kina juu ya kisukari na namna ya kuepukana na ugonjwa huo.
 
Ni jitihada nzuri. Hata hivyo, sisi tunadhani kwamba bado kuna haja ya kuwekeza zaidi katika eneo hili. Kwa mfano, inaelezwa kuwa kwa kiasi kikubwa, maradhi yasiyoambukiza kama ya moyo, kisukari na saratani huweza kudhibitiwa kwa kubadili mfumo wa maisha wa kila mmoja. Kuzingatia aina ya vyakula na kujiwekea ratiba ya mazoezi husaidia kudhibiti maradhi haya kirahisi. 
 
Matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi, visivyoandaliwa vizuri na kutofanya mazoezi huchangia mwili kuongezeka uzito kupita wastani unaopendekezwa kitaalam na mwishowe huwa chanzo cha maradhi kama ya shinikizo la damu na kisukari. Yote haya ni mambo rahisi kutekelezwa ikiwa jamii itaelimishwa bila kuchoka kuhusiana na maradhi yasiyoambukiza na kisha kila mmoja kuwa tayari kuchunga nyendo zake katika kula, kunywa na kushiriki mazoezi. 
 
Shime, jamii iamke sasa na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na magonjwa ya moyo, saratani, kisukari na maradhi mengine yasiyoambukiza. 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom