Mwalimu Nyerere alisema " Ukimchana Mtanzania kidogo tu utapata damu
ya ukabila na udini ipo karibu sana." Mwl alikuwa sahihi maana umoja
wetu uliletwa na kitu kimoja tu, nacho ni "Siasa Safi." Kwa majirani
zetu wa Kenya ambao ukabila umeshamiri, mkoloni hakuacha ukabila. Odinga
Snr ndie alikuwa awe Waziri Mkuu wakati huo kenyatta akiwa kizuizini
lakini akakataa na akasema wazi kuwa lazima Kenyatta aachiwe na yeye
atakuwa Makamu wake.
Kungekuwa na ukabila asingeacha kukamata madaraka
na kumfunika Kenyatta. Baadae kukaanza siasa chafu za " Jaluo hawezi
kuwa Rais." Kilichotokea ni Wajaluo kuhujumiwa na kutengwa na mwishowe
walivyoona wanaonewa kana kwamba si wakenya kamili wakaanza kujenga
umoja kwa ajili ya kushinikiza maslahi yao na kujilinda pia. Hii dhana
ikaenea kwa makabila mengine na ndio Kenya tunayoiona leo.
Hapa
Tanzania, huko nyuma zilitolewa kauli za baadhi ya wana CCM kuwa Rais wa
Tanzania hawezi kutoka Kaskazini. Sijui kwamba Kaskazini si watanzania
au wamefanya dhambi gani. Kwa masikitiko kabisa chama hakikutoa kauli
rasmi kukanusha au kuipinga kauli hii.
Yaliyotokea Dodoma
tumeyaona. Kwa ufupi kabisa ukiisoma Katiba ya CCM inasema kikao cha
mwanzo cha kuchuja majina ya wagombea urais ni Kamati Kuu. Na moja ya
kazi za Kamati Kuu kwa mujibu wa Ibara ya 109 (6)(b) ni kufikiria na
kutoa mapendekezo yake kwa H/K majina ya wanachama wasiozidi 5 kwa
nafasi ya mgombea urais. Kwa makusudi kabisa K/K ilinyang'anywa mamlaka
yake ya kikatiba ya kufikiria.... Kamati Kuu ingefikiriaje kama
haikupelekewa baadhi ya majina?
Chama cha Mapinduzi kina haki ya
kumkataa mtu asigombee. Lakini lazima zitolewe sababu za kukata jina la
mtu lakini pia jina linapaswa kukatwa na kikao chenye mamlaka ya
kikatiba ya kufanya hivyo. Hatuwezi kujenga umoja wa nchi kwa kuishi kwa
hisia kwamba mtu fulani ni fisadi wakati hajawahi kuambiwa rasmi kuwa
yeye ni fisadi ili ajipime kama bado anaweza kugombea urais kwa tiketi
ya CCM. Mwalimu Nyerere alivyompinga Malecela aliuelezea umma udhaifu wa Malecela na akamwandikia hadi kitabu kueleza kwanini
Malecela hafai.
Malecela hakuondolewa kwa hila bali alitakiwa ajipime na
aone kama kweli anaweza kupeperusha bendera ya CCM pamoja na udhaifu
wake. Malecela baada ya kujipima aliamua kujiondoa mweyewe kwanye mbio
za urais. Je, unadhani Malecela angeondolewa kwa hila bila kuambiwa kwa
uwazi madhambi yake angeridhika?
Tumekuwa tunasikia kwa
chinichini kuwa Lowassa ni fisadi. Kwa miaka nane ya umbea hakuna
kiongozi wa juu wa CCM aliyetoka hadharani akataja ufisadi wa Lowassa
upo wapi. Hakuna aliyesema Lowassa ameiba kiasi gani. Hatukuambiwa kama
Lowassa ni mwizi kwanini asipelekwe mahakamani kama wengine. Tumebaki
tunabweka kama mazuzu kwamba fulani fisadi bila hata kusema hasa ufisadi
wake ni nini. Kujiuzulu pekee hakutoshi kusema mtu ni fisadi maana hata
Mzee Mwinyi alijiuzulu kwa kuwajibika na baadae aliteuliwa kugombea
urais.
Na ukihesabu utakuta mawaziri waliojiuzulu Tanzania ni wengi ila
kwa sababu ambazo hazieleweki Lowassa ndie amekuwa "victim" wa siasa za
kuchafuana. Kama nilimwelewa alisema kwa vile nchi ilikuwa gizani
ilikuwa lazima hatua za haraka zichukuliwe kutafuta umeme na hivyo
utaratibu wa kawaida wa tender ambao ungechukua muda mrefu usingeweza
kufanyika katika hali ya dharura. Lakini pia alisema wenzake serikalini
waliambiwa na hivyo hakufanya kwa siri. Mwisho wa siku hatukuambiwa
aerikali ilipata hasara ya shilingi ngapi kwa maamuzi yaliyofanywa.
Kwa maoni yangu CCM imefanya makosa makubwa ambayo yanaweza
kuigharimu nchi kwa kumwondoa Lowassa kwa hila. Wangemweleza makosa yake
na akaambiwa ajipime na akaondoka huku akijua makosa yake na watanzania
wakaambiwa ukweli ulivyo, asingepata nafasi ya kulalamika. Kwa vita
aliyopigwa ikiambatana na kuvunja katiba ili kuhakikisha anaondolewa
inaimarisha hoja ya "Rais hatatoka Kaskazini" maana watu wameanza
kujenga hisia hizo kwamba kwa vile hatukuelezwa makosa ya EL huenda
aliondolewa kwa ukaskazini wake. Huwezi kuwakataza watu kufikiri hivyo
isipokuwa pale watakapopata majibu ya kutosha.
Madhara yake ni
nini? Watu wa kaskazini wata fight back kuwa tunaonewa na matokeo yake
zitaanza taratibu kujengeka siasa ya ukanda huku zikinyemelewa na udini.
Yaliyotokea Monduli si ya kupuuza hata kidogo. Nini kifanyike? CCM
itoke hadharani iwaombe radhi wanachama wake kwa ukiukwaji mkubwa wa
katiba na kanuni za chama. Pili, itueleze bila kumung'unya maneno,
tatizo la kimaadili analoshutumiwa nalo Lowassa ni lipi. Baada ya hapo
yeye atapata nafasi ya kujitetea lakini angalao yeye na watanzania
wengine wataridhika na kuendelea na siasa za umoja.
Tukiendeleza vijembe
badala ya kutatua tatizo kwa uwazi na ukweli nchi itatumbukia kwenye
siasa mbaya za ukanda ambazo zitatuathiri wote. Nasisitiza, hapa hakuna
uchama. Wale wanaoonewa watasahau vyama vyao watajikuta wapo kwenye
chama fulani kwa convenience tu ili wapiganie maslahi yao kwa pamoja. Haya ni maoni yangu tu wala hayana uhusiano na siasa za vyama.
OK. Na Dk. Onesmo Kyauke mhadhiri kutoka chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Maoni 1 :
Masuali anayouliza mwandishi na dukuduku zake ni muhimu. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, bali naafiki kauli kwamba vyama vifuate taratibu na katiba zao kikamilifu. Hata hivi, kama CCM wanahujumiana, ni tatizo lao, si tatizo la nchi. Ingawa CCM wenyewe wanajiona sana, ni muhimu wakumbushwe kwamba CCM sio nchi na nchi sio CCM.
Chapisha Maoni