Hii ni baada ya kukusanya mapato ya Sh. trilioni 1.3 Novemba, mwaka
jana ambayo pia ilikuwa rekodi serikali ya awamu ya tano ilipongia
madarakani na kufanya mabadiliko kwenye uongozi wa TRA na kudhibiti
ukusanyaji mapato.Ni jambo la kupongezwa kwani ni miaka mingi viongozi walijenga dhana kuwa Tanzania ni maskini isiyoweza kujitegemea.
Matokeo yake wananchi wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa kwa
kuaminishwa kuwa nchi kama Tanzania ni maskini na ilipaswa kutegemea
misaada ya nchi za nje.
Na hiyo ndiyo ikawa staili ya viongozi wengi kuhalalisha safari za
kwenda nchi za kigeni kusaka misaada `eti’ kwa kuwa nchi yetu ni
maskini.
TRA imepata mafanikio haya baada ya serikali kubana eneo moja tu la
bandari katika kuhakikisha watu wanalipa kodi kihalali. Mamlaka hiyo
imevunja rekodi ya kukusanya mapato ya awamu ya nne, ambayo kiwango
chake cha juu kilikuwa kati ya Sh. bilioni 800 na bilioni 900.
Tunaupongeza uongozi wa TRA na serikali katika kuhakikisha kuwa kiwango kikubwa cha mapato kinakusanywa.
Fedha hizo tayari zimeanza kutumika kupunguza makali ya maisha kwa
Watanzania mathalani, zile zilizokusanywa Novemba zimeelekezwa kusaidia
utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli, ya kutoa elimu bure.
Katika kutekeleza mpango huo wa elimu bure, serikali ilitenga Sh.
bilioni 131 ambazo zitatumika katika shule mbalimbali. Mpango huo wa
kutoa elimu bure unahusisha kutoa vitabu na kugharimia chakula.
Tunaamini katika serikali na TRA wakiendeleza kasi hii ya kukusanya
mapato, kuna uwezekano kabisa wa kuifanya nchi yetu kujitegemea.
Waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na
hayati Abeid Karume, ndoto yao kubwa ilikuwa kuifanya nchi yetu
ijitegemee.
Ndiyo Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika kilimo na ujenzi wa
viwanda kwa kuamini vingechochea maendeleo na kuifanya nchi yetu
kutotegemea misaada kutoka nje.
Hayati
Karume naye alitumia zao la karafuu kuiendeleza Zanzibar na ndipo
alipoanza mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wake na
miundombinu.
Bahati mbaya katika miaka ya karibuni, viongozi wengi waliopewa
dhamana ya kuongoza nchi yetu walijielekeza zaidi katika kujineemesha.
Kwa sasa, si jambo la ajabu kusikia viongozi wakitumia mabilioni ya
fedha kwa kisingizio cha kwenda kusaka fedha za misaada nchi za nje
badala ya kuandaa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani
ili kuondokana na aibu ya kuomba omba misaada nchi za nje.
Mathalani, serikali ikianza kubana mapato yanayokusanywa na
halmashauri mbalimbali nchini ina maana mapato ya serikali yatapanda
maradufu.
Bado hatujazungumzia kampuni mbalimbali ya uwekezaji, ambazo
zimekuwa zikipewa misamaha ya kodi na mengine yanayolalamikiwa kama ya
masuala ya gesi na madini.
Kwa mafanikio haya ya muda mfupi ya Serikali ya awamu ya tano,
inadhihirisha kuwa umaskini wa Tanzania unachangiwa zaidi na mipango
mibovu.
Tunaamini serikali ya awamu ya tano ikiendelea na kasi hii
itafanikiwa katika kipindi kifupi kutimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere ya
Tanzania kujitegemea na kuachana na kuomba omba misaada.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni